Virusi vya corona: Mitishamba ya Madagascar yashindwa kudhibiti maambukizi

Hospitali nchini Madagascar zimekuwa zikikabiliana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19 , huku rais akiendelea kunadi dawa ya mitishamba anayodai ina uwezo wa kutibu ugonjwa wa Covid 19.

Visa vya maambukizi vimeongezeka mara nne zaidi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita katika taifa hilo la kisiwani barani Afrika, huku zaidi ya watu 13,000 wakiambukizwa virusi na wengine na 162 kufariki kutokana na virusi vya corona, ambavyo vimesambaa karibu maeneo 22 ya nchi hiyo.

Licha ya ongezeka hilo la maambukizi, rais Andry Rajoelina amesimama na dawa hiyo ya kienyeji inayofahamika kama Covid-Organics, ambayo ilizinduliwa kwa kishindo mwezi Aprili.

Ilitengenezwana Taasisi ya utafiti ya Madagascar kutokana na mmea wa artemisia - chanzo cha dawa inayotumiwa kutibu malaria - na mimea mingine kutoka Madagascar.

Kinywaji hicho kilinadiwa kama tiba ambayo inaweza kuzuia na kutibu corona miezi minne iliyopita na imekuwa ikitumiwa na watoto shuleni

Mapema mwezi huu rais alionekana akigawanya dawa hiyo pamoja na bidhaa zingine muhimu kama vile mchele, mafuta na sukari kwa watu masikini katika mji mkuu, Antananarivo.

Bwana Rajoelina alikosolewa vikali kwa kusababisha mkusanyiko wa watu wakati wa amri ya kutotoka nje lakini, mtazamo wake kuhusu janga la corona haijabadilika: "Janga hili halitachukua muda mrefu, ni wingu linalopita na tutaishinda."

Pia alidai kuwa idadi ya watu walioambukizwa haikua juu viungani mwa mji mkuu ambako dawa hiyo ilikua imeanza kusambazwa miezi kadhaa iliyopita.

Shirika la Afya Duniani WHO, inaunga mkono dawa za mitishamba lakini linataka uchunguzi wa kisayansi kufanyiwa dawa hizo kabla ya kuanza kutumiwa

Kufikia sasa hakuna matokeo ya majaribio ya kimatibabu iliyotolewa kwa umma - japo hilo halijazuia dawa hiyo kutajwa kuwa chanzo cha fahari ya tiba asilia katika baadhi ya mataifa ya Afrika. Dawa hiyo imeagizwa na nchi kadhaa za Afrika

Pia unaweza kutazama:

Serikali ya Madagascar imekua ikikabiliana na ukosoaji ndani na nje ya nchi kuhusu tiba hiyo y amitishamba.

"Ni sawa na vile utumizi wa mipira ya kondomu, haimaanishi usiwe mwangalifu kuhusu ugonjwa wa UKIMWA au inamaana ugonjwa huo haupo tena? Huu ni mtazamo sawia unaotakiwa kuwa nao kuhusu dawa hii," alisema mkurugenzi wa mawasiliano katika ofisi ya rais Rinah Rakotomanga.

"Idadi kubwa ya watu waliotumia dawa hiyo na ambao hawakua wagonjwa sana wamepona kabisa, tunajivunia kwamba hii ni tiba dhidi ya coronae. Ni asili yetu watu Wamadagascar kutumia dawa za mitishamba… alimradi inafanya kazi, hatuhitaji majaribio ya kisayansi ya matibabu."

Hata hivyo, watu wengi walio na virusi vya corona wanaanza kupona baada ya kupumzika kwa siku kadhaa- ni wale tu walio na changamoto zingine za kiafya walio katika hatari ya kupata ya kuzidiwa na maambukizi ya virusi.

Lakini Wizara ya Afya imekuwa ikitoa wito wa kuzingatia uangalifu katika mpango huo - na kushauri hospitali kuwa Covid-Organic inaweza kumsaidia mgonjwa aliye na dalili kiasi na wala sio wale walio na magonjwa mengine kama kisukari.

Ridhaa ya wale wanopewa tiba hiyo pia inatakiwa, kama inavyoshauri katika muongozo wa tiba.

Japo rais Andry Rajoelina ana matumaini ugonjwa wa Covid-19 utadhibitiwa, vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaripotiwa kila siku.