Salmonella: Jinsi kuwabusu kuku kunavyoweza kueneza mlipuko wa bakteria

File picture of chickens on a farm

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kuku wanabeba vimelea vya bakteria salmonella hata kama wanaonekana ni wasafi na wenye afya

Kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (CDC) kimewataka watu waache kuwabusu kuku hai huku kukiwa na mlipuko wa bakteria aina ya salmonella.

CDC pamoja na maafisa wa afya ya umma wanachunguza mlipuko wa baketeria aina ya salmonella baada ya watu 163 kuripotiwa kuugua katika majimbo 43.

Maambukizi hayo yamekuwa yakihusishwa na watu wanaofuga kuku majumbani mwao.

"Msiwabusu au kuwakumbatia kuku, kwani hii inaweza kusambaza vimelea kwenye mdomo wako na kukufanya uugue," kimetahadharisha kituo hicho.

Ilionya kuwa kuku pamoja na bata, wanaweza kubeba vimelea wa salmonella hata kama wanaonekana kuwa wenye afya na wasafi, na vimelea hawa wanaweza kusambaa kwa urahisi katika maeneo wanamoishi na kuzunguka.

Maambukizi ya Salmonella yanaweza kusababisha kupanda kwa joto la mwili, kuhara, maumivu ya tumbo na kutapika. Watu wengi wanaopatwa na maambukizi haya hupona bila matibabu, lakini yakiwa makali yanaweza kusababisha kifo

Kulingana na CDC, theluthi moja ya watu walioripotiwa kuugua katika mlipuko wa hivi karibuni wamekuwa ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano

Wagonjwa wapatao 343 wamepelekwa hospitalini tangu katikakati ya mwezi wa Februari, lakini hakuna kifo kilichosababishwa na maradhi hayo kufikia sasa.

Ushauri wa CDC pia unajumuisha kjnawa mikono baada ya kuwahudumia au kuwashika kuku, na kuzuia watoto kuwagusa ndege.

Inakadiriwa kuwa bakteria aina ya salmonella - ambao wanaweza kupatikana katika nyama mbichi au ambazo hazijaiva, mayai au bidhaa za chakula-huwapata watu wapatao milioni 1.35 nchini Marekani kila mwaka, na vifo 420.

CDC ambalo ni shirika la umma la Marekani lenye jukumu la kutoa ushauri wa kiafya na namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, wiki iliyopita kwa mfano, lilibadili muongozo wake kuhusu barakoa, likisema watu ambao wamepata chanjo kamili dhidi ya Covid-19 hawahitajiki tena kuzivaa katika maeneo mengi.