Donald Trump: Tunafahamu nini kuhusu maisha yake baada ya 'kung'olewa' White House?

Donald Trump

Chanzo cha picha, Reuters

Je ushawahi kufikiria ukipata nafasi ya kushilikia wadhifa wa juu serikalini, kipi utafanya baada ya kumaliza hatamu yako ya uongozi?

Kuna uwezekano mkubwa jibu lako likaegemea upande wowote ule lakini hali inakuwaje kwa rais wa nchi? Mfano, kwa Marekani, kulingana na 'sheria ya marais wastaafu' iliyopitishwa mwaka 1958, inaruhusu kupata malipo ya uzeeni, kuwa na wafanyakazi binafsi na ofisi, bima ya afya na ulinzi kwake na familia yake. Hayo yakiwa na baadhi tu yale anayopata baada ya kuondoka madarakani kama rais.

Baada ya hilo, ni muhimu kujua kuwa kuna marais waliomaliza utawala wao na kushika mkondo mwingine wa maisha.

Rais Barack Obama aliamua kuingia kwenye utengenezaji wa filamu, George Washington akawa ana miliki moja ya kampuni ya kuuza mvinyo, George W. Bush akiamua kuegemea upande wa ubunifu wake na kuwa mchoraji.

Watu wengi kwa sasa wanajiuliza, Donald Trump yuko wapi siku hizi baada ya kuondoka madarakani mapema mwaka huu?

Wakati wake wa uongozi wake Trump alikuwa tofauti kidogo na watangulizi wake, akidhihirisha kutumia zaidi mitandao ya kijamii hasa mtandao wa Twitter na Instagram katika kutoa taarifa zake rasmi kwa wanahabari, wananchi, wafuasi wake na kadhalika.

Mambo yalionekea kumwendea sawa hadi wakati wa uchaguzi mwaka jana, mtandao wa Twitter ulipoweka onyo chini ya chapisho lake kwa mara ya kwanza. Trump alituma ujumbe uliosema kuwa: "Haiwezekani kwamba makaratasi ya kupigia kura yaliotumwa kwa njia ya posta yanaweza kukosa kufanyiwa udanganyifu.""

Lakini onyo hilo lilionekana kama sikio lisilosikia dawa na saa 12 baada ya Trump kutoa wito kwa wafuasi wake kuvamia bunge ambao aliwaita "wazalendo", Bwana Trump alifungwa kabisa kutumia mtandao wa Twitter.

Katika mtandao huo, Trump alifahamika kwa kuwa na wafuasi wake karibu milioni 89 waliokuwa wanafuatilia matukio yake. Mitandao mengine iliyoonekana kumfungia Trump ni pamoja na Facebook, Youtube, Snap Chat, Tik Tok na mingineo iliyoonekana kuwa mwanzo wa kunyamazisha sauti ya mwanasiasa maarufu Marekani.

Mfano tu wa jinsi ilivyo, mtandao wa Facebook, kuna wakati ulifungia hata mahojiano aliyokuwa amefanyiwa Trump na kuchapishwa kwenye ukurasa wa mkwe wake.

Trump anawasiliana vipi na dunia sasa hivi?

Baada ya kuonekana kuwa pigo kwake katika njia ya mawasiliano aliyokuwa ameitegemea zaidi kipindi chake cha uongozi, na kuondoka madarakani, Donald Trump bado ameonekana kuwa na ushawishi kisiasa, wakati huu akiwa anategemea zaidi nyumba yake ya kifahari ya Mar-a-Lago huko Florida.

Kipindi anakaribia kuondoka madarakani huku mijadala ya kura aliyopigiwa ya kutokuwa na imani naye ikiwa inaendelea, Bwana trump alionekana kidogo kujikunyata lakini mambo yakaonekana kubadilika tangu bunge Seneti liliposhindwa kumpata na hatia na kuonekana kurejea tena kuwa na sauti kubwa kama ilivyokuwa awali.

Kulingana na gazeti la The Atlantic, amekuwa akiendelea kuzungumza hadharani ikiwemo wakati wa kikao cha taifa cha chama cha Republican.

Maelezo ya video, Uchaguzi wa Marekani 2020: Tazama jinsi waandamanaji walivyovamia bunge Marekani

Huku gazeti la TRT World likisema kwamba amekuwa kwenye jumba lake la kifahari akipanga atakavyorejea kwa kishindo kwenye siasa huku akiwa kama kinara wa chama cha Republican.

Baadhi ya wanasiasa wa Republican pia wameonekana wakimtembelea Trump kwenye kasri lake wengi wakionekana kwa picha zao walizoziweka katika mtandao wa Instagram.

Na kama haitoshi gazeti la Guardian liliandika: ''Machi 13 wa wajumbe wa Republican huko Alabama, pia waliwasilisha azimio nyumbani kwake, ambalo lilimtangaza kama mmoja kati ya marais waliokuwa bora katika ya miaka 245 wa Republican.''

Kilicho wazi ni kwamba pia amekuwa akipata mahojiano kadhaa na vyombo vya habari anavyovipenda huku akikubali mahojiano na waandishi wa vitabu kuhusu urais wake. Na pengine, kuna wakati huwa anatamani vyombo vya habari kuendelea kumpa umaarufu ambavyo amekuwa akivitia dosari katika kipindi chake cha uongozi.

Wakati uwepo wake kwenye vyombo vya habari ukionekana kupungua kiasi, kumekuwa na tetesi kwamba hivi karibu aliyekuwa Rais Donald Trump, atarejea katika mtandao wa kijamii "mtandao wake mwenyewe", kulingana na mshauri wake ambaye alisema "mtandao huo utakuwa unaovuma kati ya mitandao ya kijamii" na "utabadilisha kabisa mitandao".

Huku pengine wafuasi wake wakiendelea kuwa na kiu ya kuona ndoto hiyo itatumika vipi na lini? Bado wataendelea kusubiri vyombo vya habari kupeperusha taarifa zake.