Akaunti ya Twitter ya Trump yafungwa kabisa

Donald Trump

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Donald Trump ameandika tena ujumbe kwenye mtandao wa Twitter licha ya kwamba akaunti yake ilikuwa imefungwa kwa muda

Rais wa Marekani Donald Trump amefungiwa kabisa akaunti yake ya Twitter kwasababu ya hatari ya kuchochea vurugu zaidi", kampuni hiyo imesema.

Kampuni ya Twitter imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kufuatiliwa kwa karibu kwa ujumbe wa Twitter wa akaunti ya @realDonaldTrump.

Baadhi ya wabunge na watu mashuhuri wamekuwa wakitoa wito kwa miaka mingi mtandao wa Twitter umpige marufuku Bwana Trump.

Aliyekuwa mama wa taifa wa Marekani Michelle Obama aliandika ujumbe kwenye Twitter Alhamisi akisema kituo cha ubunifu wa teknolojia duniani Silicon Valley kinastahili kuzuia uendelezaji wa tabia mbaya za Bwana Trump na kumfuta kabisa kama mtumiaji wa huduma hizo.

Kwanini Trump alipigwa marufuku?

Bwana Trump alifungiwa akaunti yake ya Twitter kwa saa 12 Jumatano baada ya kutoa wito kwa wafuasi wake kuvamia bunge ambao aliwaita "wazalendo".

Mamia ya wafuasi wake walivamia bunge wakijaribu kuvuruga kikao cha kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden kama rais. Vurugu hizo zilisabbaisha vifo vya raia wanne na afisa mmoja wa polisi.

Mtandao wa Twitter baadaye ukaonya kuwa unaweza kumpiga marufuku Bwana Trump kuutumia kabisa ikiwa atakiuka tena kanuni za jukwaa hilo la mawasiliano.

Baada ya akaunti yake ya Twitter kuwezeshwa tena, Bwana Trump alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter Ijumaa kuwa kampuni hiyo ilikuwa ya mwisho kuchochea.

Katika moja ya ujumbe wake aliandika: "Wamarekani 75,000,000 Wazalendo walionipigia kura, Marekani Kwanza na Fanya Marekani kuwa Bora Tena, watakuwa na sauti inayosikika siku zijazo. Hawatakosewa heshima au kuchukuliwa kwa uonevu kwa namna yoyote ile!!!"

Mtandao wa Twitter umesema ujumbe huo "unatafsiriwa kama ishara zaidi ya kuwa Rais Trump hana mpango wa kuhakikisha kunafanyika 'mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani'".

Katika ujumbe mwingine rais aliandika: "Kwa wote ambao wameuliza, sitahudhuria hafla ya kuapishwa Januari 20."

Mtandao wa Twitter umesema kuwa ujumbe huo "umechukuliwa na wafuasi wake kadhaa kama thibitisho la kwamba uchaguzi huo haukuwa halali".

Mtandao wa Twitter umesema ujumbe wote huo alioandika "unakiuka sera na kanuni katika uhamasishaji wa vurugu".

Tazama jinsi waandamanaji walivyovamia bunge Marekani

Maelezo ya video, Uchaguzi wa Marekani 2020: Tazama jinsi waandamanaji walivyovamia bunge Marekani

Trump amesema nini baada ya kufungiwa?

Baada ya akaunti yake ya @realDonaldTrump kufungwa kabisa, Trump alituma ujumbe kwa kutumia akaunti rasmi ya rais wa Marekani @Potus akisema kuwa "ataangalia uwezekano wa kuwa na mtandao wao utakaowezesha mawasiliano siku za usoni" na kukosoa Twitter.

Hata hivyo, ujumbe wake ulifutwa katika jukwaa hilo la mawasiliano muda mfupi baada ya kuwekwa.

Donald Trump's tweets from @POTUS account, 8 January 2021

Chanzo cha picha, Twitter

Akijibu baada ya kupigwa marufuku, mshauri wa kampeni ya Trump 2020 Jason Miller ameandika kwenye Twitter "Inachukiza... ikiwa hujafikiria kwamba wewe ndio wa pili watakaekufuata, umekosea."

Kwanini Twitter ulikuwa mtandao maarufu sana kwa Trump?

Bwana Trump alitumia mtandao wa Twitter kutukana wapinzani wake, kushabikia washirika wake, kuwafuta kazi maafisa, kukanusha "taarifa za uongo" na kutoa malalamishi yake, mara nyingi akiandika kwa kutumia herufi kubwa na alama za mshangao kusisitizia anachozungumzia.

Ingawa wakosoaji wake wamesema mara nyingi ujumbe wake ulikuwa wa kupotosha, mtandao huo ulimsaidia kukabiliana na mengi na mara moja angefanikiwa kuwasiliana na wafuasi wake karibu milioni 89.

Pia ujumbe wake mara kadhaa ulikuwa na makosa ya herufi na wakati mwingine aliacha wafuasi wake kukisia tu kile alichomaanisha.

Idara ya sheria ilisema mwaka 2017 kuwa ujumbe wa Bwana Trump ulikuwa "mawasiliano rasmi ya Rais wa Marekani".