Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Viatu vya yebo yebo vyarejea tena kwenye fasheni
Kuna wakati hungeweza kufikiria kuwa viatu vya yebo yebo vitarejea tena kuwa fasheni.
Lakini amini usiamini katika tuzo za Oscar mwaka huu ndivyo vilivyotia fora baada ya mwelekezi wa muziki Questlove kutamba kwenye zulia jekundu la Oscar akiwa amevaa viatu vya yebo yebo vilivyokuwa vimepakwa rangi ya dhahabu kwa ajili ya tukio maalum.
Ama uwe ulikuwa unavipenda au unavichukia, yebo yebo zimerejea tena kwenye fasheni.
Jumanne, mtengenezaji wa viatu aliripoti kwamba amekuwa na mauzo ya juu katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka na kuongeza mapato yake mwaka 2021.
Mauzo yalipanda kwa asilimia 64 hadi dola milioni 460 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka akilinganisha na kipindi sawa na hicho mwaka jana.
Pia faida kabla ya kutozwa ushuru iliongezeka hadi dola milioni 122.5 kati ya mwezi Januari na Machi ikilinganishwa na mwaka uliotangulia dola milioni 18.7.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya utengenezaji viatu hivyo vya yebo yebo, Andrew Rees, amesema sasa hivi mauzo ya mwaka mzima yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 50, ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 25 ililokadiriwa na kampuni hiyo mwezi Februari.
Hitaji la kiatu cha yebo yebo limeongezeka sana kote dunia, amesema Bwana Rees.
Na pia kampuni ya Marekani tayari imeanza kushirikiana na watu maarufu na nyota wa muziki wa pop kuimarisha umaarufu wake tena.
Mwaka 2018 kampuni hiyo ilishirikiana na mwanamuziki wa rapa Post Malone ambaye alienda kiatu chake mwenyewe.
Ushirikiano na nyota wa pop Bad Bunny na mwanamuziki Justin Bieber ukafuata ambavyo vyote viliuzwa kwa dakika kadhaa.
Viatu vya yebo yebo vinauzwa sana mtandaoni ambako mauzo yake yamepanda kwa asilimia 75.3 robo ya kwanza ya mwaka.
Mkakati wa kampuni hiyo unajumuisha kuvitangaza kwenye mitandao ya jamii huku viatu vya yebo yebo vikiwa vimetazamwa na watu bilioni 1.6 kupitia mtandao wa TikTok, ambako wale wanaofahamika kama washawishi kwenye video wanacheza kuzunguka viatu hivyo au kuonesha namna vinavyopendezesha mguuni.
Kusonga mbele miongoni mwa kile wanachopania kufanya ni kuangazia zaidi watu maarufu na kufanya kampeni barani Asia, ambako kampuni hiyo imetabiri uwepo wa fursa nzuri zaidi ya ukuaji kwa muda mrefu.