Idriss Déby: Suitafahamu yaikabili Chad baada ya rais wake kufariki vitani

Chanzo cha picha, AFP
Kufariki kutokana na majeraha aliyoyapata akiogoza vita dhidi ya waasi waliokuwa wameteka eneo la kusini kupitia jangwa la Sahara kutoka apande wa Libya, kumethibitisha Rais Idriss Déby Itno alikuwa mwanajeshi mpambanaji hadi mwisho wake.
Chanzo cha kifo chake kinaashiria taaluma yake aliyoanza kama afisa wa kawaida na kujiimarisha kupitia mafunzo mafupi aliyopata katika chuo cha mafunzo ya ulinzi cha École de Guerre nchini Ufaransa.
Baadaye, alianzisha uasi wake mwenyewe, kumuondoa dikteta Hissène Habré mwaka 1990.
Tangu wakati huo, ameongoza kwa mkono wa chuma.
Chad ilikuwa na misingi rasmi ya taifa lenye demokrasia ya vyama vingi. Lakini mamlaka halisi yalikuwa yanashikiliwa na utawala, na Déby hakuruhusu upinzani wa kisawa sawa katika miongo mitatu ya utawala wake.
Na mara kadhaa alikabiliwa na uasi, wakati mwingine akisaidiwa juhudi za kijeshi za mshirika wake Ufaransa- ambayo iliweka kambi yake kubwa ya kikanda katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena.

Chanzo cha picha, AFP
Mwezi Februari mwaka 2008 wanamgambo walikaribia kuvamia lango la makao ya rais.
Uasi huo, mara nyingi huchangiwa na mahasimu wa ndani ya ukoo wa Déby wa Zaghawa, waliojitenga kusini mwa Libya- eneo lililo nje ya udhibiri wa serikali ya Tripoli.
Mara hii walijitenga zaidi na kufuka kusini ya mbali, kufika hadi eneo la Kanem, kaskazini mwa Ziwa Chad kilomita chache tu kutoka mji mkuu.
Ijapokuwa vikosi vya serikali kwa mara nyingine tena vilijitangazia ushindi, vimepoteza kamanda wao muhimu.
Kiungo mkuu wa kisiasa
Kifo chake kimeacha pengo kubwa ambalo litakuwa vigumu kujaza.
Kwa kweli alikuwa na ubishi, na wakati mwingine alikuwa mkatili, Déby alikuwa mtu mashuhuri katika siasa za Afrika magharibi na kati.
Na ushawishi huo ulikuwa uendelee, kufuatia ushindi wake wa uchaguzi wa urais wa mwezi huu uliotabiriwa na wengi, akiwa na asilimia 79.3 ya kura. Uchaguzi huo ulisusiwa na baadhi ya wagombea huku wapinzani wakuu wakiondolewa katika kinyang'anyiro hicho katika hali ya kutatanisha.
Sasa mwana wa kiume wa Déby'aliye na umri wa miaka 37, Mahamat, kamanda wa ngazi ya juu na aliyekuwa mlinzi wa rais anaongoza utawala wa muda wa kijeshi ambao umefunga mipaka ya Chad na kusitisha utawala wa katiba.
Swali ni je, siasa za Chad zinazotawaliwa na kiongozi imara zitaweza kujisimamia bila kuwa na kiungo muhimu aliyebuni utawala huo?
Saleh Kebzabo, mwanasiasa wa upinzani wa ngazi ya juu, ametoa wito wa majadiliano ya kupata mwafaka kuelekea uchaguzi mpya.
Lakini maswali yameibuka ikiwa utawala huu uliopo madarakani uko tayari kushiriki kikamilifu katika majadiliano yenye tija.
Siasa za ndani na uhasama katika ukoo wa Déby wa Zaghawa pia zitazingatiwa.
Chad imekabiliwa na changamoto kadhaa za kisiasa, kijamii na kimaendelea ambazo zilidhibitiwa kutokana na utawala wa Déby wa kimabavu na bila shaka suluhisha halikupatikana.
Katika kiwango cha kikanda, kifo chake pia kimeibua maswali makubwa.
Alikuwa amejinadi kama kiungo mkuu muhimu wa kikanda, kupeleka vikosi vyake kusaidia Nigeria katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa Kiislam wa kundi la Boko Haram.

Chanzo cha picha, AFP
Wanajeshi wa Chad walio na sifa ya kuwa wapiganaji mahiri walishirikiana na wenzao wa Nigeria, Cameroon na Niger, kufanya oparesheni ya mpakani dhidi ya wanamgambo.
Japo ushirikiano huo ulizaa matunda, eneo hilo lilisalia kuwa tete kutokana na ghasia zilizokithiri huku jamii za ndani zikiathiriwa vibaya katika mzozo huo.
Huku hayo yakijiri, ndani ya Afrika Magharibi, majeshi ya Chad yalimpatia Déby jukumu la kuwa mmoja wa washikadau wakuu wa usalama katika ushirikiano wake na mataifa matano yenye uwezo mkubwa katika eneo la Sahel.
Aliwajumuisha wanajeshi wake katika kikosi cha kulinda usalama cha Umoja wa Mataifa nchi Mali, ambako walipigana vita vikali jangwani, pia aliwapeleka wengine kusaidia Mali, Burkina Faso na Niger "maeneo matatu hatari zaidi" ambako mipaka inakutana.
Déby pia alikuwa na historia ya muda mrefu ya kushawishi, kisiri au dhahiri, majiraji wa kusini wa Chad wanaokabiliwa na hali ngumu, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hali ilivyo kwa sasa Chad inakabiliwa na msukosuko mkubwa.
Je utawala mpya wa kijeshi unaoongozwa na mwanawe wa kiume utafanikiwa kuendeleza mfumo wa utawala wa driss Déby?
Je utawala huo utashauriana na mahasimu wengine miongoni mwa Zaghawa? Au utawala huo utajaribu kutanua wigo wake wa kisiasa na kuanzisha mdahalo wa jinsi ya kuendelea mbele?
Wakati Déby alipochukua madaraka mnamo 1990 hakukuwa na msimamo wowote wa Kiafrika juu ya uhalali wa mapinduzi ya kijeshi. Hilo sasa limebadilika.
Matakwa ya Afrika
Bila shaka, kifo cha Déby ghafla cha kinamaanisha Muungano wa Afrika na nchi zingine za eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara zitaupatia muda utawala mpya wa kijeshi kutoa muelekeo.
Hatahivyo, uongozi wa Afrika wa mwaka 2021 utashinikiza kurejelewa kwa utawala wa kikatiba, na nafasi ya kuwa na siasa ya vyama vingi, hata kukiwa na vizuizi. Na katika jukwaa la kikanda, watu watakuwa wanafuatilia kwa makini kuona ikiwa jeshi la Chad lina uwezo wa kuendeleza na kufanikisha juhudi za usalama zilizoanzishwa na Déby.
Serikali mpya inafahamu fika umuhimu wa kushirikiana kijeshi na majirani zao na hali kadhalika Ufaransa.
Hasa ikizingatiwa kwamba, mapambano ya dhidi ya Boko Haram ni suala ambalo linahusu moja kwa moja usalama wa Chad na masilahi yake ya kiuchumi.












