Rwanda: Manusura wa mauaji ya kimbari wanaoishi nyumba moja na 'waliotekeleza mauaji'

Claudine Mukagahima na Faustin Munyanziza wanaishi nyumba moja iliyojengwa na 'Tume inayosimamia Umoja na Maridhiano', nyumba maalum mnamoishi familia mbili ; mmoja aliyetekeleza mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 huku jirani yake akiwa ni manusura wa mauaji hayo.

Jirani Boniface Nyabyenda anasema "hakujua kuwa hili linawezekana."

Mukagahima, manusura wa mauaji ya kimbari na watoto wake wawili, wanapoishi, mlango wao unaangaliana na wa Munyanziza, ambaye amekuwa gerezani kwa miaka 9 kwa makosa ya mauaji ya kimbari na baadaye akaachiwa huru.

Wanaishi katika kijiji cha Nyamiyaga eneo la Nyanza katika nyumba ambazo zinafahamika kama 'Two in One' zilizojengwa na serikali kwa wasiojiweza.

Zaidi ya Watutsi 800,000 na Wahutu waliuawa katika mauaji ya kimbari, lakini pia kilichosalia kuwa changamoto zaidi baada ya vita, ni chuki kati ya waliotekeleza mauaji hayo na manusura kutoka makabila mawili makubwa.

Mukagahima, 48, anasema alipitia mchakato wa kidini wa kuponya roho kwa misingi ya umoja na maridhiano ambapo walifundishwa kusamehe ikiwa moja ya miradi ya kidini iliyoungana na serikali kuhamasisha raia wa Rwanda juu ya umuhimu wa maridhiano na kusamehe.

Serikali inasema katika mpango wake unaozingatia kusamehe umefikia asilimia 92 pamoja na ule wa 'Mimi ni raia wa Rwanda' unaolenga kuhakikisha kwamba raia wamerejea katika hali ya kawaida ambao ufanikishaji wake umefikia asilimia 91 kulingana na taarifa iliyotolewa mwaka 2020.

Baadhi ya wanaharakati wa mashirika yasio ya serikali, hata hivyo, wanasema kuwa asilimia hizo sio ukweli wa hali ilivyo nchini humo na kuwa serikali inafanya kila inaloweza kuthibitisha kwamba ubaguzi na maridhiano sio tena tatizo kubwa nchini humo.

"Hapo kabla, nilikuwa nikiwaangalia kwa hofu, sikuwahi kufikiria ni kwa namna gani ninaweza kuishi na muuaji," manusura huyo amesema.

Je kuna aliyemlazimisha kusamehe?

Munyanziza, 62, baada ya kuwa gerezani kwa miaka 9 na kufanya kazi muhimu kwa jamii kwa zaidi ya miaka 5, anasema awali hakuamini macho yake kama anweza kuishi na mtu aliyenusurika na mauaji hayo.

"Ilipofika wakati nikawa naingiwa na hofu, nilikuwa nikijiuliza, 'Je nitaweza kuishi na mtu yule?' Nilikuwa nikijiambia hivyo mara ya kwanza ninaanza kuishi na manusura wa mauaji hayo. Pia nilikuwa nikijiuliza, 'Je pengine itafika wakati waje kuniteka nyara , lakini hilo halijawahi kutokea.

Mukagahima anasema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ambacho wamekuwa wakiishi katika nyumba hiyo, wameshirikiana na kuishi kwa wema bila matatizo yoyote.

"Kuna siku nilimwambia, 'Twende tukasikilize radio na tuzungumzie historia,'" anasema.

Boniface Nyabyenda, jirani aliyezunguza na BBC alisema kuwa ameona wanaishi vizuri tu na jirani yake lakini hakujua kama hilo linawezekana.

"Kusema kuwa mtu aliyetuua anaishi hapa? Mimi mwenyewe nilishutuka. Sikudhania kama inawezekana.