Bandari ya Bagamoyo: Ijengwe au isijengwe?

Mradi wa bandari ya Bagamoyo

Chanzo cha picha, NMG

Maelezo ya picha, Aliyekuwa Rais waTanzania Hayati John Pombe Magufuli alisema mradi wa bandari ya Bagamoyo ulikuwa na "masharti ya hovyo" ambayo serikali yake isingeweza kuyakubali.
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

MIAKA sita iliyopita, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo nchini Tanzania ulikuwa ukitajwa kama mmoja wa miradi ya kimkakati yenye fursa kubwa ya kuzimua uchumi wa taifa hilo. Midomoni kwa watumishi wa umma na viongozi wa serikali, neno bandari ya Bagamoyo halikutoka.

Hata hivyo, miaka miwili iliyopita, upepo ukaanza kubadilika. Aliyekuwa Rais waTanzania wakati huo, hayati John Magufuli, alizungumza hadharani kuhusu mradi huo na kusema ulikuwa na "masharti ya hovyo" ambayo serikali yake isingeweza kuyakubali.

Watanzania ni watu ambao kwa tabia wanapenda kuwaamini viongozi wao. Kauli hiyo kutoka kwa Kiongozi Mkuu wan chi ilizua mkanganyiko miongoni mwa wananchi; wengine wakiamini wale waliosema bandari hiyo ijengwe na wengine wakiamini mradi huo ni wa hovyo.

Hiyo ndiyo Tanzania ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameirithi linapokuja suala la ujenzi wa bandari hiyo. Kwenye kujibu swali kubwa la makala haya, ni muhimu kurudi nyuma kidogo kufahamu kuhusu mradi wenyewe.

Kuhusu mradi wa Bandari Bagamoyo

Kwa sadfa ya kijiografia, Tanzania imejikuta ikiwa nchi yenye bandari katika eneo ambalo wengi wa jirani zake hawana bandari. Miongoni mwa jirani zake nane; Malawi, Msumbiji, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia, ni Kenya na Msumbiji pekee ndiyo wenye bahari.

Bandari ya Dar es Salaam ndiyo imekuwa kama lango kuu la kupitishia bidhaa zinazokwenda katika nchi jirani zisizo na bahari

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Bandari ya Dar es Salaam ndiyo imekuwa kama lango kuu la kupitishia bidhaa zinazokwenda katika nchi jirani zisizo na bahari

Bandari ya Dar es Salaam ndiyo imekuwa kama lango kuu la kupitishia bidhaa zinazokwenda katika nchi jirani zisizo na bahari. Hata hivyo, ingawa huduma za bandari hiyo zinahitajika sana, bandari ya Dar es Salaam- kwa sababu tofauti ikiwamo udogo wa eneo lake na ongezeko la mahitaji ya huduma na teknolojia za kisasa za meli, imeanza kuzidiwa.

Iliyokuwa Mamlaka ya Bandari wakati huo, iliona changamoto hiyo na ndiyo ikapendekeza kujengwa kwa bandari nyingine kubwa zaidi katika eneo la Bagamoyo - umbali wa takribani kilomita 75 tu kutoka Dar es Salaam ili kuendelea kuwa kitovu cha usafiri wa maji katika eneo la Afrika.

Katika kutimiza azma hiyo, Mamlaka ya Bandari ikaja na Mpango Kabambe wa Miaka 20 wa Uendelezwaji wa Bandari za Tanzania - ambao, pamoja na mambo mengine, ulipendekeza Bandari ya Bagamoyo ijengwe katika miaka ya 2021/2022.

Sadfa nyingine ya kijiografia ni kwamba eneo la Bagamoyo ni mojawapo ya maeneo ambayo China imeyatambua kama ya kimkakati katika Mpango wake Kabambe wa Belt and Road - ambao kimsingi unaunganisha dunia kupitia njia ya maji.

Tanzania iko katika eneo la kimkakati kwa sababu inazungukwa na nchi nyingi zisizo na bahari, tayari ina reli mbili zinazounganisha na nchi jirani; TAZARA kwa maana ya Zambia na ile ya Kati inayokwenda mpaka Kigoma ambako ni jirani na Congo, Rwanda na Burundi pia.

Kama ujenzi wa Reli ya Mwendokasi (SGR) ukikamilika, Tanzania itakuwa na reli ya kisasa ya kusafirisha watu na mizigo kutoka Tanzania kwenda katika nchi jirani kwa haraka.

Kwa hiyo, wakati Tanzania ikipanga kuwa na Bandari ya Bagamoyo kubwa na imara, wawekezaji kutoka China na Oman waliona fursa ya Eneo la Uwekezaji wa Biashara (EPZ) katika mji huo kwa sababu ya urahisi wa kusafirisha bidhaa kutoka eneo la Maziwa Makuu kwenda kwingineko duniani.

Faida nyingine ya Bandari ya Bagamoyo ilikuwa kwamba kwa sababu ya ukubwa wake, itakuwa na uwezo wa kupokea mizigo zaidi ya mara 20 ya Bandari ya Dar es Salaam na pia kupokea meli kubwa za kisasa ambao kwa sababu ya ukubwa wake, haziwezi kuja Dar es Salaam.

Bandari ya Dar es Salaam ndiyo imekuwa kama lango kuu la kupitishia bidhaa zinazokwenda katika nchi jirani zisizo na bahari.

Ramani inayoonesha bandari mahala ilipo ya Bagamoyo na bandari nyingine katika nchi za Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, Empics

Maelezo ya picha, Ramani inayoonesha bandari mahala ilipo ya Bagamoyo na bandari nyingine katika nchi za Afrika Mashariki

Kupitia mradi wa EPZ, ilielezwa vitafunguliwa zaidi ya viwanda ya 700 na kuajiri takribani watu 250,000 - ukiwamo mradi wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano kutoka kwa wawekezaji kutoka Korea Kusini. Huu ulikuwa uwe mradi mkubwa zaidi katika historia ya Tanzania ambako wawekezaji hao kutoka China, Oman na Korea Kusini wangeingiza nchini mtaji wa zaidi ya dola bilioni 10 (zaidi ya shilingi trilioni 23).

Wawekezaji hao na nchi wanazotoka kwenye mabano ni China Merchants Ports Limited(China), Mfuko wa Uwekezaji wa Oman (OIA), na Science and Technology Policy Institute(STEPI)Korea Kusini.

Hofu ya Mradi wa Bagamoyo

Maneno ya Magufuli yalikuja katika wakati ambao kulikuwa na taarifa nyingi kuhusu namna China inavyotwaa mali zisizohamishika za nchi zilizokopa fedha kutoka kwake na zikashindwa kurejesha kwa wakati. Mifano iliyokuwa ikitolewa sana ilihusu nchi kama Zambia na Sri Lanka.

Katika mkutano wake na wafanyabiashara wa Tanzania, Magufuli alizungumza waziwazi kwamba kwa namna makubaliano yale ya Tanzania na wawekezaji yalivyokuwa, mkataba ule ulikuwa hauna maslahi na Tanzania naye asingekubali kuona mradi huo ukiendelea kwa namna hiyo.

"Yaani kwenye eneo lote kuanzia Tanga hadi Mtwara kusijengwe bandari yoyote. Bandari ya Kilwa tusiiendeleze, Bandari ya Mtwara ambayo itawezesha mikoa ya Kusini kupokea mafuta badala ya Dar es Salaam kisha yarudihuko, hatutakiwi kuiendeleza, barabara kutoka Mtwara hadi Bamba Bay ambayo itatuwezesha kusafirisha mizigo hadi Msumbiji tusiijenge," alisema Rais Magufuli.

Spika Job Ndungai aliwahi kulalama kwamba serikali inafanya makosa kutoendelea na mradi huo kwa vile una faida kubwa

Chanzo cha picha, Bunge

Maelezo ya picha, Spika Job Ndungai aliwahi kulalama kwamba serikali inafanya makosa kutoendelea na mradi huo kwa vile una faida kubwa

Rais huyo aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Makamu Rais wake, alisema masharti mengine ya kufanyika kwa mradi huo ni kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotakiwa kwenda kukusanya ushuru wala kodi katika eneo hilo, umiliki wa eneo hilo kwa miaka 33 na kufidiwa kwa gharama za uwekezaji wa ujenzi huo.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alizungumza katika nyakati hizo na kulalama kwamba serikali inafanya makosa kutoendelea na mradi huo kwa vile una faida kubwa na hizo ambazo zinaonekana kasoro zinaweza kuzungumzika.

Kuna ukweli kwenye madai ya "mkataba wa hovyo"?

Mmoja wa viongozi wa juu katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete ambao mradi huo ulikuwa unaelekea kukamilika, ameniambia mengi ya yanayoyosemwa kuhusu mradi huo hayana ukweli na kwamba kulikuwa na upotoshaji mkubwa.

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yake, kiongozi huyo alisema gharama pekee kubwa ambayo serikali ingetakiwa kuingia katika mradi huo ni ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaohamishwa kupisha ujenzi wa bandari hiyo ambao kwa makisio ya mwaka 2016 yalikuwa kiasi cha dola takribani dola milioni 20.9 (shilingi bilioni 43).

" Gharama yetu ni hizo dola milioni 20 za kulipa wananchi lakini mengine yote ni siasa tu. Wanaokuja wanaleta shilingi trilioni 23 na ni uwekezaji wala si mkopo. Ni sawa na kampuni zinazokuja kuchimba madini hapa kwetu. Huwezi kusema wanakuja kutukopesha hela za kuchimba madini. Ni biashara yao.

" Jambo la muhimu kuliko yote ni kwamba huo mpango wa kuwa na Bandari ya Bagamoyo tulikuwa nao hata kabla wawekezaji hawajaja. Na wala hakuna masharti ya kutuzuia kujenga barabara wala miundombinu mingine. Hilo suala la miaka 33 ni la kawaida, yaani mtu aweke shilingi trilioni 23 na halafu asiweke muda wa kurudisha hela zake? Mwisho kabisa, baada ya miaka 33, bandari na hivyo viwanda havitahamishwa Tanzania na nina imani nchi yetu itakuwepo bado," alisema kiongozi huyo.

Huku Lamu, kule Bagamoyo

Kenya, kwa muda mrefu, ilikuwa ikitegemea Bandari ya Mombasa kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo kwa wateja wake wa ndani na katika eneo la maziwa makuu. Kwa sababu ya ongezeko la mahitaji, yenyewe pia ikaamua kujenga Bandari ya Lamu - kwa sababu zilezile ambazo zimeifanya Tanzania kuwa na mpango wa Bagamoyo.

Hadi sasa, nchi hizi mbili zinashindana katika kuhakikisha ipi inakuwa ya kwanza kufanikisha mradi huo ambao unatarajiwa kuleta picha mpya ya ukuaji wa uchumi wa mataifa haya mawili jirani.

Bandari ni mojawapo ya maeneo ambayo yana fursa kubwa katika ukuaji wa uchumi na majirani hawa wote sasa wanatafuta wawekezaji katika miradi ya bandari lakini kwa kuiunganisha na ile ya miundombinu ya reli za kisasa.

Hata hivyo, kwa maana ya ukubwa na umuhimu, mradi wa Bandari ya Bagamoyo una faida kubwa na muhimu zaidi kwa Tanzania kwa sababu ya faida kubwa za viwanda na kilimo zitakazosababishwa moja kwa moja na uwepo wa bandari hiyo.

Rais Samia atafanya nini?

Katika muda wote aliowahi kuwa Makamu wa Rais, Samia hajawahi kutoa kauli yake rasmi kuhusu mradi wa Bagamoyo. Hata hivyo, sasa akiwa Rais, ni wazi washauri wake wa uchumi na wenzake ndani ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), watampa ushauri unaofaa kuhusu nini hasa anatakiwa kufanya sasa.

Akiwa Rais, huenda washauri wake wa uchumi na wenzake ndani ya Serikali na CCM , watampa ushauri unaofaa kuhusu nini hasa anatakiwa kufanya sasa.

Chanzo cha picha, TWITTER/@SULUHUSAMIA

Maelezo ya picha, Akiwa Rais, huenda washauri wake wa uchumi na wenzake ndani ya Serikali na CCM , watampa ushauri unaofaa kuhusu nini hasa anatakiwa kufanya kuhusu bandari ya Bagamoyo

Dhana ya hofu dhidi ya Wachina ina mashiko miongoni mwa Watanzania wengi na ukweli kwamba hofu hiyo ilitangazwa na Rais Magufuli hadharani na katika namna ambayo ilikuwa rahisi kueleweka kwa Watanzania, inampa Rais Samia fursa ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuondoa mambo ambayo yanaweza kuwa hayana maslahi kwa taifa lake.

Bahati nzuri ambayo Watanzania wanayo kwasasa ni kwamba Samia ana asili ya Zanzibar na anajua nini maana ya bandari - pengine kuliko viongozi waliozaliwa mbali na pwani.