Shambulio la mji wa Palma Msumbiji: Watu walivyo hatarisha maisha yao kutoroka shambulio la kigaidi

Chanzo cha picha, AFP
Manusura wa shambulizi la hivi karibuni lililotokea kaskazini mwa Msumbiji ambalo lilitekelezwa na wanamgambo wa Kiislam, wamekuwa wakielezea namna walivyonusurika licha ya risasi na mabomu yaliyokuwa yanarushwa.
Wanahabari wa BBC Catherine Byaruhanga na Kyla Herrmannsen wametuandalia taarifa ifuatayo:
Eusebio Alves Pinto alikuwa anamaliza zamu yake katika hoteli ya Amarula alipoona watu wakitorokea eneo uwanja.
"Nikawauliza nini kinaendelea? Nao wakanijibu kwamba hali si nzuri," alizungumza na kituo cha televisheni cha eneo TVM.
"Muda mfupi baadaye nikaanza kusikia risasi zinarushwa." Akarejea ndani haraka sana.
Na huo ndio uliokuwa mwanzo wa shambulizi lililokuwa limepangwa Machi 24 katika mji wa Palma.

Chanzo cha picha, Dyck Advisory Group/Handout via REUTERS
Mji huo wenyewe tayari ulikuwa umekuwa hifadhi kwa maelfu ya wakimbizi waliotoroka ghasia katika eneo lililo karibu la kaskazini mkoa wa Cabo Delgado ambao umekuwa ukishambuliwa na wanamgambo kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.
Milio ya risasi na mabomu yalirushwa hotelini
Amarula - kitovu cha shambulizi lililotokea ni maarufu kwa wanakandarasi wengi.
Lakini wanamgambo wenye kuhusishwa na kundi la Islamic State wamebadilisha eneo lengwa hadi mji wa Palma ambako wenyeji wa eneo la karibu walikuwa wameomba hifadhi.

Chanzo cha picha, AFP
Awali watu walikuwa wanaweza kuwasiliana na familia zao lakini sasa hivi mawasiliano na mtandao vimekatwa.
Richard Davis, ambaye jina lake limebadilishwa kwasababu za kiusalama, ni mkandarasi wa Afrika Kusini ambaye kawaida huwa yuko Pemba.
Anaamini takriban watu 190 walikuwa wametafuta hifadhi katika eneo la Amarula, na kwamba wengi wao walikuwa wenyeji.
Bwana Davis alikuwa amewasili Palma saa kadhaa tu kabla ya kuanza kwa shambulio hilo na anaelezea kuwa ndege iliyowasili baada ya yake, ilitua na kupaa tena mara moja kwasababu ya milio ya risasi.
Serikali ilisema wanamgambo wamevamia mji huo na wamelenga maeneo matatu moja wapo ikiwa ni uwanja wa ndege.
Siku ya kwanza, Bwana Davis anakumbuka akisikiliza "uvamizi huo uliokuwa unaendelea siku nzima mchana na usiku. Siku ya pili mabomu yalikuwa yakianguka kwenye uzio wa alipokuwa huku risasi zikirushwa kwenye hoteli yao."

Chanzo cha picha, EPA
Wapiganaji kutoka kampuni ya kibinafsi ya Dyck Advisory Group, ambayo ilikuwa imekodiwa na serikali ya Msumbiji kupambana na wanamgambo, walikuwa wakipambana na wanamgambo hao karibu na hoteli.
Bwana Davis ni miongoni mwa waliokuwa na bahati.
Alhamisi yeye pamoja na wengine 19 walitolewa kwenye hoteli hiyo kwa kutumia ndege aina ya helikopta.
Lakini ukweli ni kwamba haikuwezekana kumuondoa kila mmoja kwa mjia hiyo.
Kutoka Johannesburg nchini Afrika Kusini, Gracie Alexander, 21, alielezea BBC ujumbe aliokuwa anaupokea kutoka kwa baba yake Nick Alexander ambaye anaendesha kampuni ya ujenzi eneo la Palma.
Bwana Alexander pia alikuwa katika hoteli ya Amarula.
"Alituma video iliyorekodi milio ya risasi wakati inaendelea na akatuambia tumuombee na tumfikirie wakati akiwa na matumaini ya kuhamishwa hadi eneo salama haraka iwezekananvyo," binti yake alisema.
'Kujaribu kukimbia'
Wakiwa hawajui la kufanya baada ya siku mbili za mabadilishano ya risasi, bila chakula wala maji, kukawa na mpango wa kuhamisha watu 170 waliosalia katika hoteli ya Amarula kwa njia ya msafara hadi kwenye ufukwe ulio karibu ambapo boti zingewachukua hadi mji wa Pemba, ambako Bwana Davis anasaidia kuratibu juhudi za uokozi.
"Wakaamua kuhatarisha maisha yao kwa kutoroka," anasema.
"Kulikuwa na gari moja la kivita - linaloweza kubeba watu 10 nyuma. Hilo lilibeba wanawake na watoto kutoka kijijini."
Karibu gari 17 zikafanikiwa kutoka hotelini lakini muda mchache baada ya hapo msafara huo ukavamiwa na magari 10 hayakufanikiwa kufika ufuoni.

Bwana Pinto mfanyakazi wa hoteli alikuwa kwenye msafara huo na anajihisi kama mwenye bahati leo hii kuwa hai.
"Niliona miili ya waliofariki dunia nilipoondoka hotelini. Watu wengi walikuwa wameaga dunia," amesema.
Nelson Matola, ambaye alikuwa akifanyakazi mji wa Palma pia naye alijificha katika hoteli ya Amarula lakini akapatikana msituni.
"Yalikuwa ni mauaji ya halaiki. Nafkiri hakuna kati yetu anayetaka kurejea tena huko."
Serikali ya Msumbiji imesema kuwa takriban watu 7 waliuawa katika uvamizi huo lakini Bwana Matola anasema idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi.
"Sio saba tu! Wengi walifariki dunia, baadhi ya wenzetu kutoka nchi za nje walipoteza maisha yao kipindi wanatoroka kwenda ufuoni."

"Uvamizi uliopotokea, Alexanderhe alitoroka msafara huo na kurejea ndani ya hoteli kisha akaona bunduki na kutoroka msituni alikojificha."
Baada ya siku mbili alionekana na helikopta iliyokuwa inatafuta manusura.
"Akiwa ana tiririkwa na machozi, aliona simu iliyotumia setilaiti na papo hapo akatufahamisha kwamba amenusurika," mke wa Alexander alisema.
Na waliofanikiwa kufika ufukweni walilazimika kujificha usiku mzima dhidi ya wavamizi.













