Utekaji nyara Nigeria: Mateka wa Chibok aliyekaidi kundi la Boko Haram

Utekaji nyara wa watoto wa shule nchini Nigeria umekuwa ukigonga vichwa vya habari siku za hivi karibuni na imekuwa vigumu kwa mwanamke kijana aliyetekwa nyara katika uvamizi wa shule ya Chibok kuendelea kusalia kimya.

Naomi Adamu ni mkimya. Wakati anazungumza ni nadra sana kumtazama mtu kwa macho na sauti yake iko chini kila wakati.

Wakati unakutana naye, huwezi kushuku kwamba ni manusura wa moja ya tukio baya zaidi la utekaji nyara ambalo mwanamke kijana anaweza kupitia.

Naomi alikuwa umri wa miaka 24 wakati uvamizi huo unatokea, ambapo wanafunzi 270 wa shule ya wasichana ya sekondari inayosimamiwa na serikali walitekwa nyara na kundi la wanamgambo wa Boko Haram Aprili 2014.

Wanafunzi wenzake wanamuita Maman Mu, yaani mama yetu. Elimu yake imetatizika na matatizo ya kiafya akiwa mtoto.

Na sasa hivi ni mhusika mkuu katika kitabu kinachojulikana kama "Chibok girls".

'Ujumbe wa Krismasi kwa baba yake'

Kitabu cha Bring our Girls kilichoandikwa na mwandishi Joe Parkinson na Drew Hinshaw kinazingatia mahojiano ya mamia ya wasichana waliotekwa nyara, familia zao na wengine wenye kuhusika katika simulizi hiyo.

Kitabu hicho kinaangazia wasichana hao walipotekwa nyara na pia inaonesha vile kampeni katika mitandao ya kijamii ambayo iliwafanya kuwa maarufu pia ilifanya kuachiliwa kwao kuwa vigumu zaidi.

Umaarufu wao uliwafanya kuwa adhimu yaani haingewezekana kuachiwa huru.

Kipindi cha miaka mitatu alichokuwa akiishi na wanamgambo wa Boko Haram, Naomi alikataa kutumbukia katika shinikizo la kuolewa na mmoja wa wapiganaji au kubadili dini na kuwa Muislamu.

Badala yake yeye pamoja na mwanafunzi mwengine waliandika matukio yao ya kila siku kisiri katika kitabu cha ziada waliochokuwa wamepewa kuandika aya za Kiislamu.

Na matukio hayo aliyaficha katika kipochi kilichokuwa kimefungwa mguuni.

"Tuliamua kuandika simulizi zetu," anasema, "ili ikiwa mmoja wetu atafanikiwa kutoroka, ataelezea watu kilichokuwa kinaendelea".

Moja ya aliyoandika ni barua iliyoandikwa kabla tu ya krismasi ya mwaka waliotekwa nyara kwa baba yake.

"Baba yangu mpendwa, Nakutamani sana kipindi hiki.

"Dad, Nataka nikuone tu, Nina wasiwasi sana juu yako na mama na wengine nyumbani.

"Sikuwahi kufikiria kwamba hili linaweza kunitokea, hakuna kati yetu tuliotekwa nyara aliwahi kufikiria hili. Kwa uwezo wa Mungu Baba, Nakutamani sana.

"Nataka unisaidie katika maombi ili nimshinde shetani kila anapokuja kunifadhaisha. Baba, ningependa kukomea hapa.

"Nakutamani sana. Kwaheri na Wakati mwema.

"Ni mimi binti yako mpendwa, Naomi Adamu. Nakutakia Krismasi Njema."

Mbali na kutengwa na wapendwa wao bila kujua walivyokuwa wanaendelea au hata kama walikuwa hai, wasichana hao walipitia changamoto nyingi.

Walikuwa wanahamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine kila wakati na vikosi vilivyokuwa vimejihami ikiwemo jeshi la Nigeria, vikosi vya usalama vya nje ya nchi na hata ndege zisizo na rubani za Marekani.

Mbali na muda kidogo tu walipokuwa katika mji wa Gwoza uliokuwa umetekwa na kundi la Boko Haramu mwishoni mwa mwaka 2014, muda wao mwingi walikuwa kambini katika msitu wa Sambisa, eneo ambalo ni maficho makuu ya kundi hilo.

"Tulikuwa na wakati mgumu sana," Naomi anaelezea, "hakukuwa na chakula wala maji. Ilifika wakati tulikuwa tunatumia mchanga kujisafisha wakati tuko kwenye hedhi."

Boko Haram walimshawishi aolewe na mmoja wao

Wanamgambo wakuu wa Boko Haram kila mara walikuwa wanajaribu kumuoza Naomi kwa mmoja wa wapiganaji.

Waliamini kwamba iwapo angeolewa kungesaidia kushawishi wasichana wengine wadogo kufuata nyayo zake.

Kila wakati angekataa, walimchapaa kweli na kumtishia kumuua.

Shekau alituambia kwamba hakututeka nyara ili tuolewe lakini kwasababu alitaka kushinikiza serikali iachie huru wanamgambo wake" amesema

Naomi Adamu.

Na baada ya kutambua sababu ya wao kukamatwa, aliendelea kusimamia uamuzi wake.

Wakati wanamgambo walimtenga yeye na wanafunzi wenzake walioonekana kuwa wasumbufu mbali na wengine, huku wale walioonekana wanyonge wakinyimwa chakula kuwashinika wakubali kuolewa, Naomi na rafiki zake waliiba chakula na kuwapelekea.

Na hatimaye mwaka 2017 aliachiwa huru pamoja na wasichana wengine 81, baada ya majadiliano kati ya timu ndogo ya waliojitolea nchini Nigeria na mwanadiplomasia wa Uswizi.

"Sikuwahi kufikiria kwamba kundi la Boko Haram, bado litaendelea kuwa na nguvu hii leo kwasababu tulipoondoka wakati ule, walikuwa wanagawanyana makundi mawili, na tukafikiria kwamba limesambaratika. Wengine walikuwa Sambisa, huku wengine wakiwa Kangaroua."

Lakini kampeni ya mitandao katika mitandao ya kijamii ya kuachiwa huru kwa wasichana hao, iliyoongozwa na watu mashuhuri kama vile mke wa rais Michelle Obama, kulifanya wawe maarufu na kuonesha kundi la Boko Haram vile kuteka nyara wanafunzi ni kitu muhimu.

Utekaji nyara wa sasa unarudisha kumbukumbu za awali

Chini ya mwaka mmoja baada ya kuachiwa huru, kundi la wanamgambo liliteka nyara wasichana wengine tena 100 kutoka mji wa Dapchi, jimbo la Yobe. Mwezi mmoja baadaye, wote walichiwa huru.

Hivi karibuni, watoto wa shule wamekuwa wakitekwa sana nyara nchini Nigeria.

Kumekuwa na utekaji nyara katika shule mara nne maeneo ya kaskazini mwa Nigeria katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita na karibu watoto 800 wamechukuliwa.

Utekaji nyara wa hivi karibuni ukitokea eneo la kaskazini magharibi mwa Nigeria, maili mia kadhaa kutoka ngome muhimu za Boko Haram kaskazini mashariki.