Meghan na Harry: Ubaguzi ndio sababu kubwa kwanini tuliondoka Uingereza

Mwanamfalme Harry amesema ubaguzi wa vyombo vya habari uliopenyeza hadi jamii zingine ndio sababu kubwa yeye na mke wake waliondoka Uingereza.

Mwanamfalme Harry alimwambia Oprah Winfrey kwamba vyombo vya habari Uingereza vina ubaguzi na hutengeneza "mazingira yasioweza kuvumilika" ya "udhibiti na hofu".

Alisema alifikiria kwamba Mwanamfalme Charles wa Wales alilazimika "kuhakikisha amani navyo".

Hata hivyo wahariri wanasema kuwa vyombo vya habari havina ubaguzi badala yake vinahakikisha kuwa familia ya "kitajiri na yenye nguvu inawajibika".

Meghan amesema kuwa mitandao ya kijamii ilifanya uhusiano na vyombo vya habari kuwa kama "mwituni, uhayawani" na kusema usimamizi wa vyombo vya habari wa familia ya kifalme ulishindwa kumtetea yeye na Harry kutokana na simulizi za uongo.

Katika mahojiano na Oprah, Harry na Meghan waliangazia mengi ya kibinafsi ikiwemo ubaguzi wa rangi, afya ya akili na uhusiano wao na vyombo vya habari na misukumo mbalimbali ya Familia ya Kifalme.

Mahojiano hayo ya saa mbili yalipeperushwa hewani jana usiku nchini Marekani na kuoneshwa katika vyombo vya habari vya Uingereza kupitia ITV Jumatatu Usiku kwa ushirikiano na shirika la habari la CBS.

•Meghan anasema aliona maisha katika Familia ya Kifalme kuwa magumu sana kiasi kwamba kuna wakati "hakutaka kuendelea tena kuwa hai"

•Alisema Harry alikuwa ameulizwa na baadhi ya familia yake mtoto wao Archie atakuwa mweusi kiasi gani

•Baadaye, Oprah alisema kuwa mwanafamilia huyo hakuwa Malkia wala Mwanamfalme Duke wa Edinburgh

•Wanandoa hao walitangaza kuwa wanatarajia mtoto wao wa pili mwaka huu ambaye ni msichana

•Walikula kiapo katika sherehe iliyoongozwa na Askofu wa Canterbury uani kwao siku tatu kabla ya kuoana rasmi mbele ya umma mnamo mwaka 2018 mwezi Mei

•Harry alisema kaka yake na baba yake "walinaswa katika mfumo" wa Famila ya Kifalme

•Alisema familia yake iliacha kabisa kumsaidia kifedha mwanzoni mwa mwaka jana na baba yake akaacha kupokea simu zake

•Lakini Harry anasema kwamba "anampenda sana kaka yake" na alitaka kuboresha mahusiano naye na baba yake

•Meghan anasema alimpigia simu Malkia baada ya Mwanamfalme Philip kwenda hospitali mwezi uliopita

Msimamizi wa taarifa wa Rais Joe Biden nchini Marekani, Jen Psaki alisema ilichukua "ujasiri mkubwa" kwa Harry na Meghan kuzungumzia simulizi zao binafsi pamoja na changamoto zao za afya ya akili.

Alipoulizwa kuhusu madai kwamba Familia ya Kifalme ilishindwa kufuatilia tatizo la afya ya akili na kwamba mmoja wa familia alikuwa na mashaka na rangi ya mtoto atakayezaliwa, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alikataa kuzungumza lolote kuhusiana na hilo zaidi ya kusema kwamba "amekuwa akimpongeza sana Malkia na jukumu lake la kuleta watu pamoja ambalo amekuwa akitekeleza".

Alisema "linapokuja suala la Familia ya Kifalme, sahihi analoweza kusema waziri mkuu ni kunyamaza kimya", baada ya kuulizwa ikiwa anaamini kwamba Familia ya Kifalme ina ubaguzi.

Katika mahojiano ya saa tatu na dakika 20, Oprah alimuuliza Mwanamfalme ikiwa wanandoa hao waliondoka Uingereza kwasababu ya ubaguzi. Mwanamfalme Harry alijibu: "ulichangia kwa kiasi kikubwa".

Alisema kwamba muda mfupi baada ya wanandoa hao kutangaza kwamba wataachana na majukumu ya kifalme, mtu ambaye alikuwa "rafiki na wahariri wengi" alimuonya kuhusiana na uamuzi wao wa kukabiliana na vyombo vya habari: "Tafadhali usifanye hivi kwa vyombo vya habari, vitaharibu maisha yako."

Mazungumzo hayo yalifanyika wakati wa hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuchangisha pesa mnamo mwezi Januari 2020, miezi michache baada ya Meghan kushitaki gazeti la Mail Jumapili juu ya barua ya kibinafsi na Mwanamfalme Harry akisema kwamba anahofia mke wake huenda "akawa mwathirika wa vyombo hivyo vyenye nguvu" vilivyochangia yeye kumpoteza mama yake.

Rafiki wa mahariri alimwambia: "Unahitajika kuelewa Uingereza ina ubaguzi sana." Lakini duke akajibu: "Uingereza haina ubaguzi, vyombo vya habari Uingereza vina ubaguzi, hasa magazeti."

Akizungumza na Oprah, Mwanamfalme aliongeza: "Lakini, kwa bahati mbaya, ikiwa chanzo cha habari kimekuwa na ufisadi au ubaguzi au upendeleo, chombo hicho kitachochea jamii nyingine iliosalia."

Aliongeza kuwa inasikitisha kuwa hakuna mtu wa familia ambaye amewahi kuomba msamaha kwasababu ya kuwa wanandoa hao walihisi ni lazima waishi kando na familia ya kifalme kwa kuhisi hakuna anayewaunga mkono.

"Hisia ni kwamba huu ulikuwa uamuzi wetu, hivyobasi athari zake ziko kwetu."

Alisema kwamba "ilikuwa vigumu kwasababu mimi ni sehemu ya mfumo na wao, ambao nimekuwepo".

Mwanamfalme Harry alisema "anafahamu fikra" kwamba kaka yake Mwanamfalme William "hawezi kuachana na mfumo huo lakini mimi nimeachana nao".

Alipoulizwa ikiwa William angetaka kuachana na mfumo huo, alijibu: "Sijui, Siwezi kumzungumzia."

Harry alisema kwamba "uhusiano na udhibiti na hofu ya vyombo vya habari vya Iingereza, ni kweli, ni mazingira mabaya".

Duke alisema "atamuunga kaka yake mkono kila siku" na wengine wa familia na amejitahidi kuwaonesha "kilichotokea".

Baba yake, Mwanamfalme wa Wales, "alilazimika kuhakikisha amani inapatikana" na uhusiano na vyombo vya habari.

Lakini Meghan amesema yeye na duke walishindwa kufikia amani hiyo, akisema kwamba "ilikuwa tofauti" kwasababu ya mitandao ya kijamii, akiielezea kama "Mwituni" Uhayawani".

Vyombo vya habari Uingereza havijawahi kusita kuangazia waliopo kwenye nafasi zenye nguvu, watu mashuhuri, wenye ushawishi, ikiwa wakati mwingine maswali yanayoulizwa yanaonekana kuwa yasio ya kawaida na aibu, na iwe hivyo lakini vyombo vya habari bila shaka havina ubaguzi," amesema mkurugenzi mtendaji Ian Murray.