Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bitcoin: Elon Musk apoteza taji la mtu tajiri zaidi duniani baada ya thamani ya hisa za Tesla kushuka
Mkuu huyo wa Tesla Elon Musk amepoteza taji lake la kuwa mtu tajiri zaidi duniani baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo ya kutengeneza magari duniani kushuka .
Hisa za Tesla zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 20 tangu zilipopanda kwa zaidi ya $880 mapema mwezi Januari. Zilishuka kwa kiwango kikubwa wiki hii kufuatia hatua ya kampuni hiyo kuwekeza hivi majuzi $1.5bn (£1bn) katika sarafu ya kidijitali ya Bitcoin.
Kushuka kwa thamani ya Musk kunamrudisha Jeff Bezos katika orodha ya mtu tajiri zaidi duniani.
Hatari ya kuhusishwa na sarafu ya Bitcoin - ambayo thamani yake imeshuka kwa kiwango kikubwa hivi majuzi huenda ndio iliwashinikiza baadhi ya wawekezaji wa Tesla kuuza hisa zao licha ya kwamba kampuni hiyo ilikuwa haijaathiriwa na kushuka kwake, alisema mchanganuzi wa kampuni ya Wedbush Securities Dan Ives.
''Kufuatia hatua ya Musk na Tesla kuwekeza katika sarafu hiyo ya kidijitali, wawekezaji wanashirikisha wawili hao'', alisema.
Uuzaji wa sarafu ya Bitcoin katika saa 48 zilizopita na utata unaokumbwa na sarafu hiyo umewafanya baadhi ya wawekezaji kujiondoa.
Ni nini kinachosababisha uuzaji wa Bitcoin?
Thamani ya Bitcoin ilipanda kwa asilimia 50 katika wiki zilizopita baada ya Tesla kufichua kwamba iliwekeza $1.5bn katika sarafu hiyo na kupanga kuikubali kama sarafu inayoweza kutumika katika malipo. Lakini tangu ilipopanda juu ya $57,000 siku ya jumapili , sarafu hiyo ya kidijitali imeshuka thamani kwa asilimia 20%. Ilikuwa inauzwa chini ya $48,000 siku ya Jumanne - bado ikiwa ni juu ya wakati Tesla ilipowekeza.
Licha ya bwana Musk kupewa sifa kwa kusaidia sarafu hiyo ya mtandaoni kupanda thamani, huenda akajilaumu mwenyewe kutokana na kushuka kwa thamani yake.
Katika majibizano ya mtandao wa Twitter wikendi hii, bwana Musk aliandika kwamba bei ya Bitcoin ''ilionekana kuwa juu lol''.
Suala jingine lililoishusha thamani sarafu hiyo ni matamshi ya waziri wa fedha nchini Marekani Janet Yellen , ambaye alitoa onyo kwa Bitcoin siku ya Jumatatu .
Aliitaja kuwa "njia isiyofaa kabisa ya kufanya biashara".
Matamshi yake yanafuatia kupanda kwa hamu ya Bitcoin , baada ya makampuni makubwa ya Marekani kama vile Mastarcard na Bank of NY Mellon kufuata uongozi wa Tesla katika kutangaza mipango ya kuishirikisha sarafu hiyo ya Bitcoin katika operesheni zao.
Je ni nini chengine lkinachoiathiri Tesla?
Bwana Musk ameipatia Muda mwingi Bitcoin wakati ambapo Tesla inakabiliwa na changamoto nyingine.
Kampuni hiyi hivi majuzi ilisitisha muazo mengi ya gari jipya aina ya Y SUV , huku bwana Musk akiwa na lengo la kuimarisha muundo wa gari hilo.
Mapema mwezi huu, maafisa nchini China waliitisha kikao na wakuu wa kampuni hiyo wakihoji masuala ya usalama na ubora wa gari hilo kufuatia ripoti za betri kushika moto huku gari hilo likiongeza kasi isiyo ya kawaida.
Wapinzani wa kampuni hiyo ya magari kama vile General Motors na Volkswagen wameanza kufikiria kuunda magari ya kutumia umeme katika miezi ya hivi karibuni. Hatua hiyo inafuatia kupanda kwa hisa za Tesla 2020 ambapo bei zake zilipanda kutoka $90 hadi $700.
Ongezeko hilo lilimfanya bwana Musk kumpiku mkuu wa Amazon Jeff Bezos kuwa mtu tajiri zaidi duniani kwa mara ya kwanza tangu mwezi Januari , huku pia akizua maswali kuhusu iwapo thamani hiyo ilikuwa na umuhimu katika kampuni ambayo inatoa kiwango kidogo cha magari ikilinganishgwa na wapinzani wake.
Mabilionea hao wawili wamekuwa wakipigania taji hilo la kuwa mtu tajiri zaidi duniani katika wiki zilizopita.
Kushuka kwa asilimia 8 ya thamani ya hisa za Tesla kulikuwa kukubwa tangu mwezi Septemba na kufuta zaidi ya $15bn za thamani ya Elon Musk , kulingana na Bloomberg.
Hisa hizo zilishuka thamani kwa zaidi ya asilimia 2 siku ya Jumanne.