Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mapinduzi Myanmar: Polisi watumia maji ya kuwasha kuwadhibiti maelfu ya wanandamanaji
Polisi nchini Myanmar katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw wametumia maji ya kuwasha dhidi ya wafanyakazi wanaofanya maandamano kote nchini humo dhidi ya mapinduzi ya kijeshi.
Maelfu ya raia wanashiriki maandamano kwa siku ya tatu wakitoa wito wa kuachiwa huru kwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo Aung San Suu Kyi na kurejeshwa kwa demokrasia.
Hatua hiyo inawadia baada ya Myanmar kushuhudia maandamano makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi.
Wiki iliyopita, jeshi lilipindua serikali ya nchi hiyo baada ya kudai kwamba uchaguzi uliokuwa umefanyika awali, ulikumbwa na udanganyifu bila kutoa ushahidi wowote.
Pia jeshi lilitangaza hali ya tahadhari kwa kipindi cha mwaka mmoja nchini Myanmar ambayo pia inafahamika kama Burma, na mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing amechukua uongozi wa nchi hiyo.
Bi. Suu Kyi na viongozi waandamizi wa chama cha National League for Democracy (NLD), akiwemo Rais Win Myint, wamewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani.
Wanaoandamana ni kina nani?
Kufikia Jumatatu asubuhi, makumi ya maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika katika mji wa Nay Pyi kushiriki maandamano huku miji mingine, Mandalay na Yangon pia nayo ikishuhudia maandamano hayo kulingana na idhaa ya BBC Burmese.
Waandamanaji ni pamoja na walimu, mawakili, maafisa wa benki na wafanyakazi wa serikali,
Takribani walimu elfu moja wamekuwa wakiandamana katika mji wa Yangon kuelekea Sule Pagoda kitovu cha mji mkuu wa Myanmar.
Hakuna taarifa zozote za ghasia zilizotolewa muda huo.
"Leo ni siku ya kufanyakazi, lakini hatutaenda kazini hata kama tutakatwa mshahara wetu," mwandamanaji mmoja, 28, anayefanyakazi katika kiwanda cha kutengeneza nguo, Hnin Thazin, amezungumza na shirika la habari la AFP.
Je maandamano hayo yamekuwa ya amani?
Inasemekana kuwa idadi ndogo ya waandamanaji wamejeruhiwa.
Katika mji wa Nay Pyi Taw, polisi walitumia maji ya kuwasha dhidi ya waandamanaji katika jaribio la kuwatawanya.
Video moja mtandaoni imeonesha waandamanaji wakifuta macho yao na kusaidiana baada ya kurushiwa maji ya kuwasha.
Kyaw Zeyar Oo, aliyechukua video hiyo, ameiambia BBC kuwa maji ya kuwasha yalirushwa dhidi ya waandamanaji bila onyo lolote kutolewa wakati wanafanya maandamano yao kwa njia ya amani mbele ya polisi.
Mitandaoni pia kumekuwa na wito unaotaka wafanyakazi kutoenda kazini na badala yake washiriki maandamano.
Wikendi, nchi hiyo ilishuhudia maandamano makubwa kuwahi kutokea tangu wakati wa mapinduzi yaliyojulikana kama Saffron mwaka 2007, pale maelfu ya watawa walipofanya maandamano dhidi ya utawala kijeshi.
Kulingana na mwandishi wa BBC Kusini Mashariki mwa Asia, Jonathan Head amesema maandamano makubwa yaliyofanyika wikendi yamechochea upya wale ambao walikuwa wanapinga mapinduzi ya kijeshi wiki iliyopita, ingawa bado hakuna waliojitokeza hasa kuongoza maandamano hayo.
Polisi pia wanaonekana kuchanganyikiwa kuhusu namna wanavyostahili kushughulikia waandamanaji hao ambao idadi yao inaonekana kuwa kubwa,, amesema mwandishi huyo.
Jeshi limesema nini?
Jeshi halijawahi kutoa taarifa yoyote moja kwa moja tangu lilipochukua hatamu.
Hata hivyo, limekuwa likidhibiti vyombo vya habari vya eneo, ambavyo vilitoa onyo kidogo dhidi ya waandamanaji hao Jumatatu.
Taarifa hiyo ilitolewa kwa njia ya bango lenye maandishi wakati wa vipindi vya kawaida kwenye televisheni na halikuwa linaonesha kusimamiwa na shirika lolote lile.
Wanajeshi hao wamechukua udhibiti kwa kuchukua nafasi za mawaziri kama wa fedha, afya, mambo ya ndani na mambo ya nje lakini marufuku ya mtandao imeondolewa.
Pia ilifunga mtandao wa Facebook, ambao ndio unaotumika kwa kiasi kikubwa kote nchini humo, mtandao wa Twitter na Instagram.
Hali hii ilianzaje?
Wiki iliyopita, Myanmar ilichukua uongozi wa taifa hilo kufuatia uchaguzi mkuu ambapo chama cha NLD kilipata ushindi mkubwa.
Vikosi vya jeshi vilikuwa vimeunga mkono upinzani ambao ulidai kurudiwa kwa uchaguzi kwa madai ya wizi wa kura.
Hata hivyo, tume ya uchaguzi ilisema madai hayo hayana ushahidi wowote.
Mapinduzi hayo yametokea wakati kikao kipya kinatarajiwa kufunguliwa.
Pia unaweza kutazama: