Aung San Suu Kyi: Mfahamu mpiganiaji wa Demokrasia aliyepinduliwa Myanmar

Alijulikana kama mpiganiaji wa haki za kibinadamu - mwanaharakati ambaye alitoa uhuru wake kupambana na majenerali wakatili wa jeshi ambao walitawala Myanmar kwa miongo kadhaa.

Mwaka 1991, Aung San Suu Kyi alikabidhiwa tuzo ya amani ya Nobel akiwa chini ya kifungo cha nyumbani, na alisifiwa kwa kuwa mfano mzuri wa kutetea wanyonge.

Mwaka 2015 , aliongoza chama chake cha National League for Demoracy NLD kupata ushindi katika uchaguzi wa wazi uliokuwa na ushindani mkali nchini Myanmar katika kipindi cha miaka 25.

Lakini aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi 2021 wakati jeshi lilipochukua udhibiti na kumkamata yeye na viongozi wake.

Huku sura yake ikiwa imechafuliwa kimataifa kutokana na jinsi alivyokabiliana na mzozo uliokumba Waislamu wa Rohingya walio wachache, aliendelea kuunga mkono watu wa Budha walio wengi.

Jinsi alivyojipatia madaraka

Bi Suu Kyi alihudumu miaka 15 akiwa kizuizini kati ya mwaka 1989 na 2010. Harakati zake za kuleta Demokrasia katika taifa ambalo limekuwa likitawaliwa kijeshi zilimfanya kuonekana kama nembo ya kimataifa ya upinzani wa amani wakati wa ukandamizaji.

Licha ya ushindi wake mkubwa mwaka 2015 , katiba ya Myanmar ilimzuia yeye kuwa rais kwasababu ana watoto ambao ni wa mataifa ya kigeni . Lakini Bi Suu Kyi , aliye na umri wa miaka 75 hivi sasa alionekana kuwa mshauri mkuu wa serikali .

Wadhfa wake rasmi ulipatiwa jina la mshauri mkuu wa serikali ya Myanmar.

Rais wa taifa hilo hadi mapinduzi hayo ya 2021, Win Mint alikuwa mshauri wake wa karibu.

Mwaka 2020, chama chake cha NLD kilishinda kwa wingi wa kura kikijipatia kura nyingi zaidi ya mwaka 2015. Jeshi lenye uwezo mkubwa lilipinga matokeo hayo likidai kwamba kulikuwa na udanganyifu.

Katika siku ambayo bunge lilitarajiwa kuwa na kikao cha kwanza, Jeshi lilimkamata bi Suu Kyi pamoja na viongozi wengine wengi wa kisiasa. Baadaye likatangaza hali ya dharura likikabidhi mamlaka kwa mwaka mzima.

Mizizi yake ya kisiasa

Bi Suu Kyi ni mwana wa kike wa shujaa wa uhuru wa taifa hilo Jenerali Aung Sun. Aliuawa alipokuwa na miaka miwili pekee , kabla Myanmar kujipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1948.

Mwaka 1960 alielekea India na mamake Daw Khin Kyi , ambaye alikuwa ameteuliwa kuwa balozi wa Myanmar mjini Delhi.

Miaka minne baadaye alielekea katika chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza ambapo alisomea filosofia , siasa na uchumi. Alipokuwa huko alikutana na mumewe , msomi Michael Aris.

Baada ya kuishi na kufanya kazi nchini Japan na Bhutan , aliishi nchini Uingereza ambapo alikuwa akiwalea wanawe wawili, Alexander na Kim, lakini Maynmar haikuwa mbali na fikra zake.

Wakati alipowasili katika eneo la Yangon mwaka 1988 - ili kumwangalia mamake aliyekuwa akiugua - Myanmar ilikuwa katikati ya machafuko ya kisiasa.

Maelfu ya wanafunzi , wafanyakazi wa ofisini na watawa walifanya maandamano wakitaka mabadiliko ya kidemokrasia.

''Sikuweza kupuuza kile kilochokuwa kikiendelea'' , alisema katika hotuba aliyoitoa katika eneo la Yangon tarehe 26 Agosti 1988.

Aliendelea na kuongoza upinzani dhidi ya dikteta wakati huo jenerali Ne Win.

Kifungo cha nyumbani

Akipatiwa msukumo na kampeni ya amani ya mwanaharakati wa haki za kibinadamu nchini Marekani Martin Luther King na Mahatma Gandhi wa India, alipanga mikutano na kusafiri nchi nzima akipigania mabadiliko ya amani ya kidemokrasia na uchaguzi huru.

Lakini maandamano hayo yalinyamazishwa na jeshi , ambalo lilichukua utawala kupitia mapinduzi ya tarehe 18 Septemba 1988.

Bi Suu Kyi aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani mwaka uliofuatia.

Serikali ya kijeshi iliitisha uchaguzi mwezi Mei 1990, ambapo chama cha Suu Kyi kilishinda kwa wingi wa kura lakini Junta ikakataa kukabidhi madaraka. Bi Suu Kyi aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani katika eneo la Yangon kwa miaka sita , hadi alipoachiliwa Julai 1995.

Aliwekwa tena chini ya kifungo cha nyumbani mwezi Septemba 2000 alipojaribu kusafiri kuelekea katika mji wa Mandalay akikiuka masharti ya kutosafiri.

Aliachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka mwezi Mei 2002, lakini baada ya mwaka mmoja alifungwa baada ya mzozo kati ya wafuasi wakena kundi lililokuwa likiungwa mkono na serikali.

Baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani - lakini chini ya masharti ya kifungo cha nyumbani.

Wakati mwengine alifanikiwa kukutana na maafisa wa chama chake cha NLD na baadhi ya wajumbe , lakini katika miaka ya awali hakuruhusiwa kukutana na wanawe wawili ama mumewe ambaye alifariki kutokana na saratani Machi 1999.

Mamlaka ya jeshi ilijitolea kumruhusu kwenda Uingereza kumuona wakati alipokuwa mgonjwa kupitia kiasi, lakini alikataa akihofia kwamba hatoruhusiwa kurudi katika taifa hilo.