Dustin Higgs: Adhabu ya mwisho ya kifo yatekelezwa chini ya utawala wa Trump

Bill Breeden, an anti-death penalty advocate, protests the execution of Dustin Higgs, outside the United States Penitentiary in Terre Haute, Indiana

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mahakama iliwahi kumpatia Higgs kinga ya kutekelezwa kwa adhabu hiyo dhidi yake baada ya mfungwa huyo kupatikana na ugonjwa wa Covid-19

Dustin Higgs, mfungwa aliyekuwa amehukumiwa kifo katika gereza la Indiana, amenyongwa katika utekelezaji wa mwisho wa adhabu hiyo chini ya utawala wa wa Rais wa Marekani Donald Trump siku chache kabla aondoke madarakani.

Higgs alipewa hukumu hiyo baada ya kuwaua wanawake watatu waliokuwa wamejifichwa katika mbuga ya wanyama mwaka 1996, lakini hadi kifo chake alikana kutoa amri ya mauaji hayo.

Alifariki baada ya kudungwa sindano ya sumu saa saba na dakika ishirini na tatu majira ya mji huo sawa na (06:23 GMT) siku ya Jumamosi.

Mauaji yake ni 13 kutekelezwa tangu mwezi Julai baada ya Marekani kusitisha utekelezaji wa hukumu ya kifo miaka 17 iliyopita.

Hatua hiyo inajiri siku chache kabla ya Rais Mteule Joe Biden, ambaye anapinga adhabu ya kifo, kuapishwa.

Utawala wa Trump umekosolewa kwa kuharakisha utekelezaji wa adhabu hiyo-

Dustin Higgs alifanya makosa gani?

Higgs alishtakiwa na kuhukumiwa adhabu ya kifo mwaka 2001 baada ya kuhusika katika vitendo vya utekaji nyara na mauaji ya wanawake watatu mwaka 1996: Tanji Jackson, Tamika Black na Mishann Chinn.

Wanawake hao walikuwa wametoka na Higgs na wanaume wengine. Higgs hakuua mwathiriwa wake yeyote, lakini alimwagiza mshtakiwa mwenzake Willis Haynes kufanya hivyo. Haynes amesema katika nyaraka za mahakama kwamba Higgs hakumtishia, au kumlazimisha afyatue risasi.

Haynes, ambaye alikiri kupiga risasi, alihukumiwa kifungo cha maisha katika kesi tofauti.

"Sio haki kumuadhibu vikali Bw. Higgs kuliko muuaji halisi," wakili wake alisema katika barua aliyomuandikia Rais Trump kuomba mteja wake apunguziwe adhabu.

Alexa Cave, sister of Dustin Higgs, talks about the moment she watched her brother being executed at the Federal Correctional Complex in Terre Haute, Indiana

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Alexa Cave, dada yake Dustin Higgs, alikuwepo wakati wa kuuawa kwake

Siku ya Jumanne mahakama ilikuwa imetoa kinga ya kutotekelezwa kwa adhabu y akifo dhidi ya Higgs na mfungwa mwingine , Corey Johnson, baada ya wawili hao kupatikana na ugonjwa wa Covid-19 wakiwa jela - baada ya mawakili wao kufahamisha mahakama jinsi mapafu yao yaliyoathiriwa na ugonjwa huo yangeliwasababishia machungu wakati wa kuuawa kwao.

Lakini idara ya haki ilikataa rufaa dhidi ya uamuzi huo na kushinda kesi. Johnson alinyongwa siku ya Alhamisi.

Jitihada za mwisho za kusitisha kuuawa kwa bwana Higg ziligonga mwamba siku ya Ijumaa baada ya majaji wa Mahakama ya Juu zaidi ya Marekani kupiga kura 6-3 kutoa idhini ya adhabu hiyo kutekelezwa.

"Hii sio haki," Jaji Sonia Sotomayor aliandika kupinga hatua hiyo. "Baada ya kusubiri kwa karibu miongo 20 kurejelewa kwa utekelezaji wa kifo, serikali ingelikuwa imeweka mikakati ya kuhakikisha hukumu hiyo inatekelezwakwamujibu wa sheria. Wakati ilikosa kufanya hivyo, mahakama hii ingelikuwa imefanya hivyo. Na haikufanya hivyo."