Lisa Montgomery: Mwanamke pekee anayekabiliwa na adhabu ya kifo kunyongwa Marekani

Lisa Montgomery in jail

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Lisa Montgomery natarajiwa kunyongwa Januari 12, 2021

Mahakama ya rufaa nchini Marekani imeondoa kizuizi cha kunyongwa kwa mwanamke pekee anayesubiri adhabu ya kifo.

Lisa Montgomery alimnyonga mwanamke mjamzito huko Missouri kabla ya kumkata na kumteka nyara mtoto mnamo 2004.

Ikiwa uamuzi uliyotolewa na mahakama dhidi yake itatekelezwa, atakuwa mfungwa wa kwanza wa kike nchini Marekani kunyongwa karibu miaka 70 iliyopita.

Tarehe ya kunyongwa kwa Montgomery ilikuwa imepangwa kuwa mwezi uliyopita lakini ikaahirishwa baada ya wakili wake kupatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Baadae idara ya haki ilibadilisha tarehe hiyo hadi Januari 12 mwaka 2021. Lakini mawakili wa Montgomery wamepinga tarehe hiyo wakidai kwamba ilitolewa kabla ya kizuizi cha kunyongwa kwake kuondolewa.

Mahakama ilikubaliana na hoja ya mwakili wake na kusimamaisha agizo la mkurugenzi wa magereza la kutaka kubadilishwa kwa tarehe ya kunyongwa kwake.

Lakini siku ya Ijumaa jopo la majaji liliamua kwamba mkurugenzi wa magereza alifuata sheria, kuruhusu mfungwa huyo kunyongwa.

Wanasheria ya Montgomery wamesema watawasilisha ombi kwa majaji kutafakari uamuzi wao.

Mwanamke wa mwisho kunyongwa na chini Marekani alikuwa Bonnie Heady, ambaye alikufa katika chumba cha gesi huko Missouri mnamo 1953, kulingana na Kituo cha Habari cha Adhabu ya Kifo.

Hukumu ya kifo ilikuwa imeseitishwa kwa miaka 17 kabla ya Rais Donald Trump kuamuru irejelewe tena mapema mwaka uliyopita.

Ikiwa wafungwa wanaokabiliwa na hukumu ya kifo watanyongwa, Bw. Trump atakuwa rais wa Marekani alitekeleza hukumu hiyo zaidi kwa zaidi ya karne moja.

Kunyongwa kwa Montgomery kutafanyika siku kadhaa kabla ya Rais mteule Joe Biden kuingia rasmi madarakani.

Bwana Biden, ambaye kwa miongo kadhaa alikuwa akiunga mkono adhabu ya kifo alipokuwa seneta wa Delaware, sasa amesema atatafuta njia ya kukomesha utekelezaji wa adhabu kifo mara tu atakapoanza kazi.

Lisa Montgomery ni nani?

Mnamo Desemba 2004, Montgomery aliendesha gari kutoka Kansas hadi nyumbani kwa Bobbie Jo Stinnett, huko Missouri, ikidaiwa kununua mtoto wa mbwa, kulingana na taarifa iliyotolewa na idara ya Sheria kwa vyombo vya habari.

"Mara baada y akuingia nyumbani, Montgomery alimshambulia na kumnyonga Stinnett - ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi nane - hadi mwathiriwa akapoteze fahamu," ilisema taarifa.

Montgomery alimkata tumbo mwasiriwa na kumtoa mtoto ambaye alimchukua katika jaribio la kudai kwamba ni wake.

Mwaka 2007, majaji walimpata Montgomery na kosa la utekaji nyara uliosababisha kifo, mna kwa kauli moja kutoa hukumu ya kifo dhidi yake.

Lakini mawakili wake wamesema alipata dosari kwenye ubongo kutokana na kupigwa akiwa mtoto na anaugua ugonjwa mbaya wa akili.

line

Wafungwa wengine wanaotarajiwa kunyongwa

  • Cory Johnson alihukumiwa kwa mauaji ya watu saba, kuhusiana na kuhusika kwake na biashara ya dawa za kulevya huko Richmond, Virginia. Timu ya kisheria ya Johnson imesema kuwa ana shida ya kiakili, inayohusiana na unyanyasaji wa mwili na mihemko aliyopitia akiwa mtoto. kifo chake kimepangwa kutekelezwa tarehe 14 Januari.
  • Dustin John Higgs alihukumiwa baada ya kuhusika na vitendo vya utekaji nyara na mauaji ya wasichana watatu mnamo mwaka 1996 Washington, DC. Higgs hakuua mwathiriwa wake yeyote, lakini alimwagiza mshtakiwa mwenzake Willis Haynes kufanya hivyo. Haynes amesema katika nyaraka za mahakama kwamba Higgs hakumtishia, au kumlazimisha afyatue risasi. Higgs amepangiwa kunyongwa tarehe 15 Januari.