Uchaguzi Uganda 2021: Mambo muhimu unayopaswa kujua

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Kinyang'anyiro cha nafasi ya urais nchini Uganda ndicho chenye mvuto zaidi kuliko kingine kikiwa kimebeba hekaheka nyingi, ufuasi mkubwa, matumaini, na hamasa miongoni mwa wapigakura kote nchini humo.
Uganda ni taifa la pili la Afrika mashariki kufanya uchaguzi mkuu wake wa Januari 14 mwaka 2021 baada ya Tanzania iliyokamilisha uchaguzi wake Oktoba 28 mwaka huu, huku Kenya likiwa taifa lingine linatakalofuatia katika mlolongo huo ifikapo mwaka 2022.
Nchini Uganda jumla ya wagombea 11 wanachuana kwenye nafasi ya urais huku wakifanya mikutano ya kampeni katika Kaunti 353, sawa na wilaya 134, majiji 8 pamoja na mji mkuu wake wa Kampala kwa muda wa siku 60 pekee, lakini taswira ya uchaguzi huo imekuwa yenye kuashiria hali hasi na chanya.
Matukio ya kukamatwa wagombea wa upinzani, hamasa ya wapigakura, kuibuka kwa wagombea binafsi nafasi ya urais, kampeni zilizojaa vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola.
Kifo cha muungano wa upinzani pamoja na mgomo wa vyombo vya habari kurusha matangazo ya mikutano ya kampeni ya mgombea wa chama cha NRM Yoweri Museveni ni miongoni mwa mambo yanayoangaziwa katika kukua ama kudidimia kwa siasa za vyama vingi nchini Uganda.
Ajenda za wagombea wa urais nchini humo zimejikita katika rushwa, umasikini, miundombinu, kuboresha huduma za jamii, kuzalisha ajira kwa vijana,kusimamia uhuru wa kujieleza, kulinda usalama wa raia na mali zao.
Na haya ni mambo ya kuzingatia yenye athari katika uchaguzi huo:
Kiongozi anayetaka kusalia madarakani kwa miaka 40
Rais Museveni ni mmoja wa marais waliosalia madarakani kwa muda mrefu barani Afrika. Aliingia madarakani kupitia chama chake cha National Resistance Movement mwaka 1986 at baada ya kumalizika kwa vita vya miaka mitano na ameongoza Uganda kutoka wakati huo.
Wafuasi wake wanampongeza kwa kuleta amani nchini, na hususan sera yake ya afya. Alisaidia kudhibiti kusambaa kwa virusi vya HIV, na hivi karibuni kuweka amri ya kutotoka nje- iliyosababisha shule na biashara kufungwa, kupiga marufuku usafiri wa magari ya umma na utumizi wa lazima wa barakoa katik amaeneo ya umma mwezi Mei- anapongezwa kwa kukabiliana vikali na virusi vya corona.
Kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Uganda imethibitisha visa vichache vya maamukizi chini ya 40,000 na vifo karibu 300 kutokana na ugonjwa huo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya kwamba wakati mmoja alipongezwa na nchi za magharibui kuwa kuwa kizazi kipy acha viongozi wa Afrika, wakosoaji wake wanamlaumu kwa kugeuka kuwa kiongozi wa kiimla .
Bw. hana mrithi katika chama chake, na mwaka 2017 alitia saini sheria ya kutoa ukomo wa miaka 75 kwa mgombea urais hatua iliyomwezesha kugombea tena urais.
Utawala wake umepingwa kwa miaka kadhaa, hususana na kiongozi wa upinzani Kizza Besigye, ambaye alikamatwa mara kadha japo aliamua kutogombea tena urais mwaka 2021.
Japo Bw. Museveni bado anafurahia uungwaji mkono mkubwa, hasa katik amaeneo ya vijijini, anakabiliwa na upinzani kutokana ana ongezeko la ukosefu wa usawa na udhibiti wake mkali wa nchi.


Mwenendo wa vyombo vya dola na vikundi vya kisiasa
Matukio mbalimbali yanaonesha kuwa vyombo vya dola hasa Jeshi la Polisi nchini Uganda limekuwa likivuruga mikutano ya kampeni ya wagombea wa upinzani.
Matukio kama vile ya kuzuia kufanya mikutano ya hadhara na kumkamata mgombea wa Robert Kyagulanyi, ambaye aliwekwa rumande katika kituo cha polisi cha Nalufenya , vurugu zilizotokea kati ya Novemba 18 na 19 jijini Kampala ambapo polisi walivuruga mikutano ya kampeni ni mambo ya kufuatiliwa.
Mgombea mwingine Patrick Amuriat ameripotiwa kukutana na vizuizi vya vyombo vya dola wakati anaingia katika jiji la Arua kupitia mji wa Lemerijoa, ambako idadi kubwa ya askari walizingira njia za kuingia na kutoka maeneo hayo.
Aidha, jambo lingine ni kuibuka kwa vikosi vinavyofanya fujo dhidi ya vyama vya upinzani au chama tawala.
Vikundi hivyo vimetajwa na duru za usalama kuwa vinafanya kazi ya kuvuruga mikutano ya kampeni ya wapinzani wao.
Kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu kwa jirani zao Tanzania, nako nchini Uganda mabango yenye matangazo ya wagombea wa nafasi mbalimbali kutoka vyama vya upinzani yamekuwa yakiondolewa na askari hali ambayo imelalamikiwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kutokuwa na mizani sawa ya kufanya shughuli za kampeni za uchaguzi mkuu.
Mabango yaliyolengwa zaidi ni yale ya mgombea wa NUP, Robert Kyagulani.
Mgomo wa vyombo vya habari

Ingawaje haikutarajiwa lakini imeripotiwa kuwa vyombo vya habari nchini Uganda vimegoma kutangaza habari za kampeni za mgombea wa chama cha NRM.
Hili ni jambo ambalo limeleta gumzo kubwa nchini Uganda, ambapo msimamo wa vyombo hivyo ni kushinikiza uwanja sawa katika kampeni za uchaguzi nchini humo.
Mijadala kupitia mitandao ya kijamii, tovuti, vyombo vya habari vya ndani na nje vimeripotiwa kugoma kurusha matangazo ya moja kwa moja (Live) ya redio na runinga mikutano ya kampeni ya mgombea wa NRM, Yoweri Museveni.
Hatua ya vyombo vya habari kugoma kurusha matangazo hayo ni kutokana na kukamatwa kwa mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi na baadaye kuachiliwa huku baadhi ya wafuasi na wananchi wengine wakijeruhiwa wakati wa zoezi hilo.
Baadhi ya raia wa Tanzania wanaoishi na kusoma vyuo mbalimbali nchini Uganda wamemwambia mwandishi wa makala haya, "kulikuwa na jambo la kushangaza, televisheni zinarusha vipindi vya muziki wakati Museveni alikuwa akihutubia watu kule Moroto.
Unajua hapa Uganda wagombea wanafanya kampeni wilaya 134 sawa na majimbo 353, kote huko ni ndani ya siku 60 za kampeni.
Sasa fujo hizi wanazofanyiwa wapigakura na wanasiasa kunaswa na vyombo vya dola ni mtihani kwa wanahabari na mwelekeo wa taifa lenyewe. Wamezima kabisa mikutano ya Museveni,"
Uganda bila muungano wa upinzani wa mwaka 2016

Nguvu kubwa ya ushindi wa Museveni imetajwa kutoka ufalme wa Buganda katikati ya taifa hilo.
Kulinda na kuheshimu utawala wa kifalme wa Buganda ni miongoni mwa eneo muhimu linalotengeneza nguvu ya Museveni licha ya madai kuwepo mzozo baridi baina ya pande hizo mbili.
Upande wa kambi ya upinzani nguvu zao zilitegemea umoja wao. Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2016, muungano wa vyama vya upinzani ulimuunga mkono mgombea Amama Mbabazi ambaye alionekana kuwa na nguvu zaidi wakati wa uchaguzi huo.
Kwenye uchaguzi huo Mbabazi aligombea baada ya kuachana na chama cha NRM, lakini uchaguzi wa mwaka 2021 mwanasiasa mwenye nguvu amejijenga binafsi kupitia muziki.
Lakini kuelekea uchaguzi wa mwaka 2021, mwanasiasa mwenye nguvu ni Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bob Wine.
Mwanasiasa huyu anazidi kumpa changamoto Museveni kuliko wakati wowote wa uchaguzi wa Uganda.
Uhuru wa Tume ya Uchaguzi na Mahakama

Kama zilivyo nchi zingine linapofika suala la uchaguzi mkuu, Uganda nayo imekuwa ikishuhudia malumbano makali juu ya uaminifu wa Tume yao (EC).
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kumekuwa na uhaba wa uhuru katika tume yeneywe na miongoni mwa viongozi wake. Taswira waliyonayo baadhi ya wapigakura na wanasiasa kwa ujumla ni mashaka juu ya mwenendo wa tume kusimamia uchaguzi huru na haki.
Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016 asilimia 89 za kura za maoni zilitaka mabadiliko katika Tume na michakato yote ya uchaguzi mkuu.
Aidha, tume hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukata kutokana na bajeti hafifu,udanganyifu wa majina ya wapigakura na vituo vya kupigia kura na uhesabuji wake.
Uchaguzi huo unahusisha wagombea 11 walioanza kampeni tangu Novemba 19 mwaka huu; John Katumba, Robert Kyagulanyi Ssentamu, Mugisha Muntu,Henry Tumukunde, Norbet Mao, Joseph Kabuleta Kiiza, Patrick Amuriat Oboi, Fred Mwesigye, Nancy Linda Kalembe, Willy Mayambala na Yoweri Museveni.
Mwaka 2001, Kizza Besigye alishindwa kufurukuta katika Mahakama ya Rufani baada ya jaribio la kupinga ushindi wa Yoweri Museveni.
Mwaka 2006, 2011 kesi nyingine ya kupinga ushindi wa Museveni ilifunguliwa, licha ya Mahakama kukiri dosari kwenye baadhi ya taratibu za uchaguzi, lakini haikufuta matokeo ya uchaguzi.
Msuguano wa mwaka 2016 ndani ya mhimili huo wa dola unatajwa kuwa huenda ukawa chachu ya kufanya uamuzi wa kupingwa matokeo ya uchaguzi mwaka huu ikiwa utatokea.
Hofu ya ugonjwa wa corona
Kampeni za uchaguzi mkuu zinafanyika huku kukiwa na tishio la ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Corona, ambapo Mkurugenzi wa Shirika la Afya barani Afrika, Dk. Matshidiso Moeti akibainisha kuwa ugonjwa huo unatarajiwa kusambaa zaidi kutoka na mikusanyiko ya kampeni na kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka kama vile krismasi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtandao wa gazeti la kila siku la Daily Monitor umeripoti kuwa baada ya miezi 8 kupitia serikali ya Uganda imeruhusu safari za Mabasi kutoka nchi hiyo kwenda nchini Tanzania.
Vilevile limeripoti taarifa ya kijana Baroda Kayanga Watongola mwenye umri wa miaka 27 kuwania ubunge jimbo la Kamuli huku kukiwa na kumbukumbu ya mzazi wake Hajat Rehema Watongola kufariki kwa ugonjwa wa corona mnamo Novemba 14 mwaka huu.
Baroda ameomba kugombea nafasi hiyo kuziba pengo la mzazi wake ambaye alikuwa na ndoto za kuwania jimbo hilo.
Tafsiri yake ni kwamba ipo hofu ya ugonjwa wa corona ambayo imesababisha Tume ya uchaguzi nchini humo kutoa angalizo kwa viongozi wote wa timu za kampeni kuzingatia masuala muhimu ya kuepukana na ugonjwa huo.















