Uchaguzi Uganda 2021: Kwanini uchaguzi huo ni muhimu kwa Afrika Mashariki?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Katika viongozi walio madarakani barani Afrika kwa sasa, ni wachache wanaweza kujigamba kuwa wafuasi wa Umajumui wa Afrika (Pan Africanism), kumzidi Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.
Wakati ugonjwa wa Corona ulipokuwa unapiga Afrika Mashariki katika wimbi kuu la kwanza katikakati ya mwaka huu, kila nchi ilichukua hatua zilizoshawishiwa na viongozi wake wakuu kwenye kujikinga na ugonjwa huo.
Nchini Uganda, mmoja wa waandishi wa habari rafiki zangu niliyozungumza nao wakati ule aliniambia uamuzi wa Museveni kutofunga mipaka yake ulichagizwa zaidi na Umajumui wake kuliko kitu kingine chochote. Ndani kabisa ya roho yake, Rais huyo wa Uganda anaamini Afrika Mashariki ni nchi moja na asingeweza kuwafungia Waganda, Wakenya au Watanzania wasitoke.
Wakati raia wa Uganda wakijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Januari 14 mwakani, swali kubwa la kujiuliza kwa wengi ni kwa vipi uchaguzi huu ni muhimu kwa taifa hilo na eneo zima la Afrika Mashariki kwa sasa na miaka mingi ijayo.
Museveni na ndoto ya Shirikisho la Afrika Mashariki
Si siri kwamba mmoja wa viongozi ambao wamekuwa wakizungumza - sirini na hadharani, kuhusu umuhimu wa Shirikisho la Afrika Mashariki ni kiongozi huyu wa Uganda kwa miaka 36 sasa.
Museveni anaamini kwamba Afrika ilitawaliwa kirahisi na wakoloni na inaendelea kunyonywa hadi sasa kwa sababu ya kukosa umoja. Jambo moja ambalo amekuwa akilipigania mara kwa mara ni kuundwa kwa Shirikisho hilo la kisiasa.
Kwa hali ilivyo sasa, hamu kubwa ya shirikisho hilo iko zaidi kwa Museveni kuliko kwa viongozi wengine kwa sababu tofauti. Kimsingi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, EAC inapita katika kipindi kigumu kwa sababu ya siasa za kikanda na kidunia ambazo sasa zinaangalia ndani ya nchi zaidi kuliko nje.
Shirikisho la Afrika Mashariki linamaanisha soko kubwa zaidi la bidhaa kwa wananchi wa eneo hilo, mzunguko mkubwa wa mitaji na utaalamu, uimara zaidi wa ulinzi na usalama na uhusiano imara zaidi baina ya nchi hizo.
Ni Umajumui huo wa Museveni ndiyo uliomfanya akubali Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) likafanye kazi za kulinda amani katika nchi kama Somalia na kwingineko.
Ushindi wa Museveni utamaanisha Uganda kuendelea kuwa mojawapo ya nchi zitakazokuwa zinaamini katika mambo ya kimajumui - yaliyo na faida kwa ukanda na bara zima la Afrika; hata kama wananchi wake watakuwa na uzoefu tofauti katika uongozi wake kwao.
Mradi wa Bomba la Mafuta wa Tanzania na Uganda

Chanzo cha picha, Ikulu ya Tanzania
Septemba mwaka huu, Tanzania na Uganda ziliingia katika makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta litakalotoka Hoima hadi bandari ya Tanga. Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilomita 1,445 na mradi mzima una thamani ya zaidi ya dola bilioni 3.5 za Marekani.
Kenya ilikuwa pia ikiutaka mradi huu lakini inaaminika kwamba mojawapo ya sababu zilizofanya Tanzania iupate na mahaba ambayo Museveni anayo kwa taifa la Julius Nyerere.
Museveni alianza kujipambanua kama mwanasiasa na mwanaharakati katika miaka ya 1960 wakati akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Aliishi Tanzania katika miaka ya 1970 na ni majeshi ya Tanzania ndiyo yaliyompa fursa ya kuja kuwa kiongozi wa baadaye wa Uganda.
Mradi huu wa bomba la mafuta ni mkubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki na unatarajiwa kuwa na athari chanya kiuchumi kwa nchi hizi mbili. Hata hivyo, hakuna uhakika sana kama mtawala mpya wa Uganda atakuwa na hamu ya kufanya hivyo na Tanzania.
Kwa sababu hiyo, kama Museveni ataendelea madarakani, mradu huo mkubwa unatarajiwa kubaki kama ulivyo na kuondoka kwake madarakani kunaweza kubadili mambo.
Mtihani kwa demokrasia na utawala bora
Endapo Museveni atashinda katika uchaguzi huu, atakuwa amefikisha miaka 40 madarakani wakati atakapokuwa amemaliza muda wake wa miaka mitano madarakani.
Ataweka rekodi ya kuwa kiongozi aliyedumu madarakani kwa muda mrefu zaidi katika eneo hili.
Museveni amefanya hivyo kwa kuondoa ukomo wa kikatiba wa kubaki madarakani. Endapo atashinda katika uchaguzi huu, itakuwa ni pigo kwa wale wanaoamini katika demokrasia ya viongozi kukaa madarakani kwa vipindi maalumu.
Kuna hatari ya dhahiri kuwa ushindi wake unaweza kufanya viongozi wengine wa nchi jirani kuamua kujiongezea muda wa kubaki madarakani kinyume cha matakwa ya Katiba ya nchi zao.
Rais Paul Kagame wa Rwanda, tayari amebadili Katiba ya taifa lake na kujiongezea muda wa kubaki madarakani, hayati Pierre Nkurunziza wa Burundi alifanya hivyo na miongoni mwa nchi wanachama wa EAC - ni Tanzania na Kenya, pekee ambapo viongozi wameonekana kuheshimu Katiba zao.
Hata hivyo, ushindi wa Museveni, utatuma ujumbe kwa nchi wanachama wa EAC na nchi nyingine za Afrika kuwa hakuna shida kutoheshimu Katiba.
Kushindwa kwake katika uchaguzi huu, kutatoa funzo kubwa kwamba kung'ang'ania madarakani kuna kadhia ya kushindwa kwa aibu na kuondoka madarakani ukiwa umeacha urithi wa aibu.
Kuamsha ari ya vyama vya upinzani
Bobi Wine anapitia kile ambacho wanasiasa wengi wa upinzani wanapitia barani Afrika. Anakumbana na vipigo, kesi zisizokuwa na kichwa wala miguu na ni kama anapigana na msuli wa dola nzima ya Uganda.
Hakuna anayempa nafasi kushinda katika uchaguzi huu kwa sababu ya uwezo wa kirasilimali, kimtandao na mbinu za kiuchaguzi za chama tawala cha NRM.
Kama, katika mazingira ya namna hii, Bobi ataibuka na ushindi, hili linaweza kutoa matumaini kwa vyama vingine vya upinzani katika eneo hili kuwa ushindi unawezekana pamoja na changamoto zote zilizopo.
Katika nchi za EAC, mara nyingi wapinzani huwa hawashindi katika chaguzi. Ndiyo sababu, uchaguzi huu wa Uganda unaweza kutoa kitu tofauti kwa washindani wengine.
Nguvu ya vijana

Uganda ni mojawapo ya mataifa yenye watu wengi wenye umri mdogo. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali, umri wa wastani wa Waganda ni miaka 16.
Bobi Wine ana umri wa miaka 38, ambao kwa nchi kama Tanzania, asingeruhusiwa hata kuwania urais kwa vile Katiba inataka mtu afikishe miaka 40 kwanza ndipo awe na sifa ya kuwania nafasi hiyo.
Ushindi wa Bobi utatoa nguvu na mwamko mkubwa kwa vijana wa Afrika kuhusu mambo wanayoweza kuyafanya katika umri wao mdogo. Kwa nchi zenye masharti kama ya Tanzania, zinaweza kuanza kujiuliza kama kuna ulazima wa kuweka vikwazo na ubaguzi wa umri kwa vijana.
Uchaguzi wa Uganda utakuwa unafuatiliwa na vijana wengi barani Afrika si kwa sababu Bobi ni kijana mwenzao wanayemfahamu, lakini kwa sababu ushindi wake unaweza kufungua fursa nyingi zaidi kwa wengine.












