Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Chanjo ya kwanza kutoa kinga kwa asilimia 90
Ufanisi wa chanjo ya virusi vya corona inasemekana kwamba inaweza kuzuia zaidi ya asilimia 90 ya watu kupata ugonjwa wa Covid-19, uchunguzi wa awali unaonesha.
Wavumbuzi wa chanjo hiyo kampuni ya Pfizer na BioNTech - wanaielezea kama "siku muhimu kwa wanasayansi na binadamu".
Chanjo hiyo imefanyiwa majaribio kwa watu 43,500 katika nchi sita na hakuna wasiwasi wowote kuhusu suala la usalama ambalo limeibuliwa.
Kampuni hizo zinapanga kuomba kupata idhinisho la dharura la kuanza kutumika kwa chanjo hiyo kufikia mwisho wa mwezi huu.
Hakuna chanjo ambayo imewahi kutoka hatua ya kwanza na kuidhinishwa kuwa yenye ufanisi katika kipindi kifupi namna hiyo.
Hata hivyo bado kuna mabadiliko makubwa mbele yetu lakini tangazo hilo limefurahiwa na wasayansi waliolielezea kama lenye kufurahisha na kwamba kuna matumaini kuwa hali ya maisha huenda ikarejea kama kawaida.
Je chanjo hiyo inaweza kuwa na ufanisi kiasi gani?
Chanjo hiyo kando na kuwa tiba inaonekana kama matumaini ya kuondokana na vikwazo vilivyowekwa na nchi mbalimbali kama njia moja ya kukabiliana na virusi vya corona.
Data inaonesha kuwa dozi mbili ambazo zinaachana kwa wiki tatu ni muhimu mno.
Majaribio ya chanjo hiyo nchini Marekani, Ujerumani Brazil, Argentina, Afrika Kusini na Uturuki - zinaonesha kuwa kwa silimia 90, mtu anaanza kuwa na kinga baada ya kupata dozi ya pili.
Hata hivyo, data hiyo sio utafiti wa mwisho kwasababu umetokana na watu 94 tu waliojitokeza katika majaribio ya chanjo hiyo kwahiyo huenda ufanisi ukabadilika wakati matokeo kamili yamefanyiwa uchunguzi.
Dkt. Albert Bourla, mwenyekiti wa kampuni ya Pfizer, alisema: "Tunakaribia hatua muhimu ya kutoa kile ambacho kimekuwa kikihitajika kote duniani na kusaidia kumaliza janga hili la afya linalokumba dunia."
Je chanjo hiyo itaanza kupatikana lini?
Watu kadhaa wanaweza kuipata mwaka huu.
Kampuni za Pfizer na BioNTech zinasema zitakuwa na data salama na za kutosha kufikia wiki ya tatu Novemba na kupeleka chanjo hiyo kwa wadhibiti.
Lakini hadi itakapoidhinishwa haitawezekana kwa nchi kuanza kampeni za chanjo hiyo.
Kampuni hizo mbili zinasema zitaweza kusambaza dozi milioni 50 kufikia mwisho wa mwaka huu na karibu bilioni 1.3 kufikia mwisho wa 2021.
Je chanjo hiyo itaanza kupatikana lini?
Je nani atapata chanjo yenyewe?
Sio kila mmoja atapata chanjo hiyo moja kwa moja kwasababu kila nchi inaamua nani wa kumpa kipaumbele.
Wafanyakazi wa hospitali na wahudumu wa nyumbani huenda wakapewa kipaumbele kwasababu ni miongoni mwa walio katika hatari pamoja na wazee.
Watu wenye umri wa chini ya miaka 50 na wasio na matatizo ya kiafya huenda wakawa wa mwisho katika orodha hiyo.
Bado kuna maswali ambayo bado hayajapata majibu kwasababu hii ni data ya muda tu.
Haijajulikana ikiwa chanjo hiyo itasitisha usambaaji wa virusi vya corona au kutokea kwa dalili. Au kama ifanyakazi vivyo hivyo hata kwa watu wenye umri mkubwa.
Swali kubwa ni je kinga itadumu kwa muda gani? Itakuwa miezi au miaka?
Pia kuna changamoto nyingi za utengenezaji na usafirishaji wa dawa hiyo hadi kufikia idadi kubwa ya watu kwasababu inatakiwa kuhifadhiwa katika sehemu baridi chini ya nyuzi joto 80 hasi.
Hadi kufikia sasa chanjo hiyo imejitokeza kuwa salama kwa asilimia kubwa katika kipindi cha majaribio lakini hakuna dawa ambayo ni salama kwa asilimia 100.
Je inafanya vipi kazi?
Kuna chanjo kadhaa zilizo katika hatua ya mwisho ya majaribio - lakini hii ndio ya kwanza kuonesha matokeo yenye kuleta matumaini.
Majaribio ya awali yanaonesha chanjo hiyo inafundisha mwili kutengeneza kinga ya mwili na sehemu nyingine ya mfumo wa kinga inayojulikana kama chembe saidizi za T kukabiliana na virusi vya corona.
Je watu wameipokea vipi?
Mshauri mkuu Uingereza Profesa Chris Whitty amesema kuwa matokeo yameonesha "nguvu ya sayansi" na "sababu ya matumaini" kwa mwaka wa 2021.
Rais aliyeteuliwa Joe Biden alisema kwamba "hizo ni taarifa za kutia moyo".
"Ni muhimu kujua kuwa mwisho wa mapambano dhidi ya virusi vya corona bado kuna miezi kadhaa mbele yetu," aliongeza.