Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Namna kizazi cha zamani na kipya vinavyopokezana kijiti CCM

Aliyekuwa katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinanana na rais John Pombe Magufuli
Maelezo ya picha, Aliyekuwa katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinanana na rais John Pombe Magufuli
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinaongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Tangu amalize Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) mwanzoni mwa miaka ya 1970, Jakaya hakuwahi kutoka ndani ya chama hicho - akipanda vyeo kuanzia kuwa ofisa wa ngazi ya chini hadi kada namba moja wa chama.

Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake, Pius Msekwa, alikuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa CCM wakati ikianzishwa mwaka 1977; kimsingi, akimpokea Kikwete kwenye chama zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Katibu Mkuu alikuwa Abdulrahman Kinana; askari ambaye tangu aingie CCM zaidi ya miaka 40 iliyopita, hajawahi kukaa mbali na chama chake.

Kinana anabaki kwenye historia kama mwana CCM pekee aliyepata kusimamia kikamilifu kampeni za marais watatu wa chama hicho; Benjamin Mkapa, Kikwete na John Magufuli.

Miaka mitano baadaye, picha imebadilika katika uongozi wa juu. Rais Magufuli alifanikiwa kuwashinda wapinzani wake ndani ya CCM mwaka 2015 kwa sababu ya kuwa kwake mbali na siasa za chama hicho wakati huo.

Makamu Mwenyekiti wake, Philip Mangula, ni mwana CCM mtiifu asiye na sifa mbaya za makundi ya chama hicho. Tofauti na Kikwete, Msekwa na Kikwete, Mangula hakuwa na bahati ya kuchaguliwa kuongoza na badala yake mara nyingi amekuwa akishika nafasi za kuteuliwa katika maisha yake ya uongozi.

Mrithi wa Kinana, Dk. Bashiru Ally, hana mizizi ndani ya chama hicho na uteuzi wake wa nafasi yake hiyo ndiyo wa kwanza kwake ndani ya chama hicho.

Mwanzoni mwa mwaka huu, kulikuwa na wasiwasi kwenye duru za CCM kuhusu ni kwa namna gani chama hicho kikongwe zaidi nchini kitashiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu ilhali kikiwa na viongozi wenye uzoefu mdogo wa siasa za ushindani.

Kama chama hicho kitaibuka na ushindi katika uchaguzi huu, ni wazi huu utakuwa mwanzo wa uongozi wa kizazi kipya cha viongozi wa chama hicho na mwisho wa zama za viongozi waliokuwepo wakati CCM ikianza au kuibuka katika wakati chama hicho kinazaliwa.

Umri haumngoji mtu

Wengi wa viongozi waliokuwa madarakani wakati CCM inazaliwa au waliojiunga na chama hicho wakati kingali kichanga, sasa wana umri wa kuanzia miaka 70 na kuendelea.

Kwa sababu ya umri wao, wengi ni watu walioamua kutulia nyumbani na kuachana na purukushani za kukimbia huku na kule kuomba kura.

Wengine wameanza kukumbwa na changamoto za kiafya za uzeeni na hawawezi tena kutoka kwenda kutafutia kura wagombea kama zamani.

Haijsaidia kwamba uchaguzi wa mwaka huu unafanyika katika tishio la ugonjwa wa Corona na watu wazee wenye magonjwa hatarishi wako katika hatari ya kuambukizwa endapo watajiweka kwenye mazingira hatarishi.

Kizazi kipya cha wapiga kura

Katika chaguzi zote zilizopita, CCM ilikuwa na utaratibu wa kuwatumia. viongozi wake wastaafu kuwafanyia kampeni wagombea wake. Hakuna mfano mzuri wa hili kama Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ambapo chama hicho kilimtumia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kumnadi Mkapa dhidi ya Augustine Mrema wa NCCR Mageuzi.

wanachama wa CCM

Kwa kawaida, CCM ilikuwa ikiwatumia wastaafu kama ,mawaziri wakuu, marais na viongozi wengine mashuhuri kushawishi wapiga kura wamchague mgombea wao.

Watu kama John Malecela, Cleopa Msuya, Ali Hassan Mwinyi, Mkapa na wengine walikuwa wakitumika sana kuzunguka mikoani kuiuza CCM kwa wananchi.

Hata hivyo, ushawishi wa wanasiasa wa kizazi hiki kwa kizazi kipya cha wapiga kura ni mdogo. Tanzania ni taifa la vijana ambapo zaidi ya nusu ya watu wake wamezaliwa baada ya mwaka 1999 kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali.

Hii maana yake ni kwamba vijana hawa hawajui kizazi hiki cha wanasiasa kiliwasaidia vipi au kina mchango gani kwenye maisha ya sasa.

Rais wa zamani wa Tanzania jakaya mrisho Kikwete

Wao, wanaweza kushawishiwa zaidi na wasanii au watu wengine mashuhuri wanaogusa maisha yao. Kwa sababu hiyo, wakongwe hao si watu wanaosaidia kuongeza kura kama ilivyokuwa miaka 20 au 30 iliyopita.

Ni muhimu kufahamu pia kwamba miaka 20 iliyopita walikuwepo Watanzania wengi zaidi waliokuwa hai wakati CCM inazaliwa au Tanganyika na Zanzibar zinapata Uhuru. Kizazi hiki kilihusisha mafanikio yao kimaisha na matamanio yao ya baadaye na chama. Watanzania wa kizazi hicho sasa wako wachache zaidi.

Mabadiliko ya CCM yenyewe.

Wakati wa utawala wa Kikwete, CCM ilifanya mabadiliko yaliyofanya kinachoendelea sasa kifanyike kwa urahisi. Chama kiliunda Baraza la Wazee kwa ajili ya wastaafu na kuwaondoa kushiriki kwenye vikao vya juu vya chama.

Uamuzi huo ulilalamikiwa na baadhi ya wanachama kwamba ulikuwa unaengua wazee wa chama kwenye vikao vya maamuzi. Kabla ya maamuzi hayo, viongozi wa juu wastaafu wa CCM na Serikali walikuwa ni wajumbe wa kudumu wa vikao vya Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya CCM.

Uamuzi wa CCM wakati wa Kikwete ulimaanisha kwamba kazi ya wazee sasa ingekuwa ni kushauri tu na si kushiriki katika vikao vya uamuzi. Mwenyekiti wa sasa wa Baraza hilo, Msekwa, amewahi kueleza kuhusu kukosa meno kwa baraza hilo kwa kusema kuwa maana ya ushauri ni mbili; kwamba kwanza ni lazima uombwe ushauri na pili, ni uamuzi wa aliyeomba ushauri kufuata au kukataa alichoambiwa.

Mwisho wa Zama

Katika uchaguzi wa mwaka huu, mstaafu pekee ambaye ambaye ameonekana kuzunguka kidogo ni Kikwete ambaye hata hivyo alikwenda Kusini mwa Tanzania ambako mkewe anawania ubunge kwa tiketi ya chama tawala, halikadhalika Mzee Ali Hassan Mwinyi Zanzibar ambako mtoto wake Dikta Hussein mwinyi anawania Urais.

Kumalizika kwa uchaguzi huu na CCM kushinda itamaanisha kwamba chama kiko tayari kuanza upya safari ya kujengwa upya. Kizazi kile cha CCM ya zamani sasa kitakuwa na watu wachache zaidi na wenye ushawishi mdogo zaidi.

CCM inaweza kabisa kuamua kufuata njia ya China ambapo viongozi wastaafu hawaruhusiwi hata kutoa maoni hadharani kuhusu mwenendo wa nchi. Ukimaliza muda wako wa uongozi unafunga mdomo wako na kusubiri kuombwa ushauri ambao utautoa katika mazingira ya usiri.

Na kwa sababu ya mkanganyiko wa kiitikadi uliopo, CCM ya baadaye haitahitaji tena kutengeneza makada wake kwa ajili ya nafasi za uongozi na badala yake itakuwa inangalia ni nani ambaye wapiga kura watakuwa tayari kumchagua miongoni mwa kundi la wafuasi wake.

Wanachama wa CCM

Katika kitabu chake End of History, Yoshihiro Francis Fukuyama, aliandika kuhusu mwisho wa zama za kihistoria kuhusu ugomvi wa Ujamaa na Ubepari. Yeye aliamini kufa kwa Ukomunisti kulimaanisha dunia sasa itabaki na mfumo mmoja tu Soko Huria na Demokrasia.

Hata hivyo, ambacho hakukijua ni kwamba mabadiliko ndiyo jambo la kudumu duniani kwa sababu sasa hata mfumo wa demokrasia na soko huria unapita katika changamoto.

Uchaguzi wa mwaka huu unahitimisha safari ya miongo minne ya kizazi cha miaka ya 1970.

Hata hivyo, unafunua uwanja kwa kizazi kingine kuziba nafasi iliyopo.