Uchaguzi wa Tanzania 2020: Je, vyama vya siasa vinafanana na kutofautiana kwenye mambo gani?

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais Tanzania
- Author, Uchambuzi
- Nafasi, Na, Markus Mpangala
Wakati chama tawala CCM kikikwepa ajenda ya Katiba mpya kwenye mikutano ya kampeni pamoja na sera zilizopo katika ilani ya uchaguzi 2020-2025, vyama vitatu vya upinzani vimekubaliana kuwa suala hilo ni muhimu kwa ustawi wa wananchi nchini Tanzania.
Vyama vya CCM, NCCR Mageuzi, ACT Wazalendo na Chadema ambavyo vimeonesha kujiandaa kwa ushindani vikiwa na ilani zinazotajwa kuwa bora hadi sasa kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu vimetofautiana na kukubaliana katika masuala mbalimbali kisera, mikakati, mbinu na ufanisi.
Masuala ya msingi ya kutofautiana na kukubaliana yametokana na ilani za vyama hivyo na yamejikita katika maeneo ya elimu, afya, uhuru wa vyombo vya habari, haki za wanawake, watoto,vijana na wazee, ulinzi wa rasilimali, ulinzi na usalama wa raia, haki za wafungwa, asasi za kiraia, biashara na uchumi, haki za kisiasa, diplomasia, ujirani mwema, uhuru wa kujieleza, utu, uzalendo, usawa wa uteuzi katika vyombo vya uamuzi, muafaka wa kitaifa, mahitaji muhimu kama vile umeme, mchakato wa katiba mpya, maji na vyakula pamoja na suala la muungano wa Tanzania.
Tangu kufunguliwa kwa mikutano ya kampeni Agosti 26 mwaka huu wagombea kutoka vyama vya Chadema, ACT Wazalendo, NCCR Mageuzi, CCM wamekuwa wakichuana vikali kunadi sera zao huku wakitamba Ilani hizo zimebeba suluhisho kwa maisha ya wananchi.
Vyama hivyo vinne vimekuwa katika kukubaliana na kutofautiana kwa wakati mmoja juu ya utekelezaji wa sera na mipango ya taifa.
Matunda ya kukubaliana na kutofautiana vikali ni taarifa ya serikali ya nchini humo hivi karibuni kutangaza kufunguliwa dirisha la nafasi za ajira takribani 13,000 kwa walimu wa shule za msingi kuanzia septemba 7 mwaka huu.
Si hilo tu, sekta ya afya nayo imepokea taarifa muhimu kutoka kwa mgombea wa CCM John Magufuli ambaye amedai bima ya afya kwa wote inatarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.

Mgombea wa chama kikuu cha upinzani Chadema, Tundu Lissu amekuwa akinadi sera za kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya afya kwa kuanzisha bima ya afya kwa wananchi wote, jambo ambalo linakubaliwa na mgombea wa NCCR Mageuzi, Yeremiah Maganja pamoja na John Magufuli wa CCM ambaye akiwa kwenye kampeni Misungwi, mkoani Mwanza, alieleza kuwa bima hiyo inakuja hivi karibuni na iwapo atachaguliwa ataharakisha utekelezaji.
Je, vyama hivyo vinakubaliana mambo gani?

Ajira: Vyama vyote vimetoa ahadi za kuzalisha ajira kwa wingi. Chadema kupitia ilani ya uchaguzi 2020-2025 wameahidi kuzalisha ajira 8,000,0000 endapo watachaguliwa kuingia madarakani.
Nao ACT Wazalendo wananadi ajira 10,000,000 ndani ya miaka mitano.
CCM kulinda ajira za watanzania kulingana na sheria namba 1 ya mwaka 2015 pamoja na kuzalisha ajira 7,000,000 kwa vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi (Kipengele cha 32, ukurasa wa 29).
Chadema wamepanga kuzalisha ajira milioni nane.
Uchumi wa Kiditali: CCM kimepanga kuielekeza serikali kutekeleza mpango wa uchumi wa kidigitali. Ukurasa wa 12, kifungu cha 18(a), "Kuendeleza uchumi wa kidigitali (Digital Economy) ili uweze kuchochea maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii nchini" (ix).
ACT Wazalendo wanasena watajenga uchumi wa watu kwa kuwapa wananchi uhuru na kuondoa urasimu katika kuanzisha na kuendesha biashara yoyote, pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kisera ili kuendesha biashara kwa njia ya mtandao yaani uchumi wa kidigitali.
Ni uchumi huo unaozifungamanisha ACT wazalendo na CCM.
Kwa upande wa Chadema, wanasema kwa kushirikiana na sekta binafsi itatunga sera za kuwezesha wananchi kushiriki na kunufaika na biashara ya masoko ya fedha inayotumia mitandao (4.1; a,b,c,d,f).

Uhuru wa vyombo vya habari: Chama cha ACT Wazalendo katika ilani yake kipengele cha 2.1.2(i) kinasema, "Itafuta sheria zote kandamizi na zinazopora uhuru wa vyombo vya habari na kutengeneza sheria, kwa kushirikiana na wadau, zitakazolenga kuleta uhuru na weledi na ukuaji wa sketa ya habari." Aidha inasema itaunda Kamisheni ya vyombo vya habari ambayo itaratibu habari na maadili ya vyombo hivyo.
Elimu bure: CCM, Chadema, ACT Wazalendo na NCCR Mageuzi vyote vinakubaliana sera ya kutoa elimu bure nchini.
CCM na NCCR Mageuzi wananadi sera ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Chadema wananadi elimu bure kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.
ACT Wazalendo inasema itaajiri walimu 20,000 kila mwaka ili kukidhi hitaji la ongezeko la wanafunzi na kusisitiza itatoa elimu bure kuanzia shule ya awali, msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vya utabibu.
Haki za wanawake: "Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha ushiriki wa 50 kwa 50 katika ngazi zote za uongozi hasa kwenye taasisi za kuteuliwa, "(ukurasa wa 10, kifungu I) na kifungu cha IX, kinasema, "Itapitia na kufuta sheria za kimila zinazomnyima mwanamke haki ya kumiliki mali na ardhi, shabaha ni kuwa na usawa wa kumiliki mali na ardhi kwa wanawake,".
Chadema wanasema, "kuhakikisha unyanyasaji wa wanawake katika masuala ya mirathi na talaka unakomeshwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile taasisi za dini na mashirika ya kijamii," (kipengele cha 6.3; kifungu cha A, ukurasa wa 45).

Upande wao NCCR Mageuzi wanasema, "Kuwa na idadi iliyo sawa ya wanaume na wanawake katika vyombo vya uwakilishi na kupanua mfumo wa uwakilishi wa uwiano yaani 50-50. Kuwa na meya wa jiji/mji au mwenyekiti wa halmashauri mwanamke na naibu meya au makamu mwenyekiti mwanamke au kinyume chake (Kipengele cha Sera ya usawa wa kijinsia, ukurasa wa 23).
Nao CCM wamejinadi kuwa watahakikisha wanalinda haki za wanawake, watoto, vijana na wazee kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa na wengine.
Ulinzi na usalama: Changamoto ya miaka mitano ni kudorora kwa hali ya usalama wa raia na viongozi wao.
Tanzania imeshuhudia matukio ya watu wasiojulikana pamoja na kushambuliwa kwa risasi aliyekuwa mbunge wa Singida mashariki na Mnadhimu wa Kambi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu.
Kwa muktadha huo, katika ilani za uchaguzi za 2020-2025 vyama vya siasa vimeonesha kutilia mkazo na kukubaliana mahitaji ya kuboresha usalama wa raia, mali na viongozi ni muhimu.
Akizungumza katika mkutano wa kufungua kampeni kwenye viwanja vya Zakheim, Jijini Dar es salaam na mikutano yake ya Kawe (Dar es salaam), Mbeya na Mwanza, Lissu alikumbusha tukio la kushambuliwa.
Ilani ya chama chake inasema, "Serikali ya Chadema itahakikisha kwamba utendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama unazingatia ustawi na uwepo wa usalama kwa wananchi na mali zao (ukurasa 93, kifungu H).
Diplomasia: Vyama vyote vya CCM, ACT Wazalendo, NCCR Mageuzi na Chadema kwenye ilani zao vinakubaliana kuendeleza mahusiano mema na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, mikataba ya kimataifa, ushirikiano na uhusiano mwema na taasisi za kifedha duniani kwa maslahi ya nchi hiyo.
"Kuwa na mahusiano mazuri na mashirika ya kimataifa duniani ili kuwezesha Tanzania kufaidika na fursa zinazopatikana katika fedha za kuendesha, uwekezaji mitaji, na masoko ya bidhaa za Tanzania," (kipengele cha 2.4.9, kifungu cha V, ukurasa wa 18, Ilani ya ACT Wazalendo).


Je ni mambo gani yanatofautisha vyama hivyo?
Mchakato wa Katiba mpya: Vyama vya ACT Wazalendo, Chadema, NCCR Mageuzi kupitia ilani zao na mikutano ya kampeni vyote vinanadi kurejesha mchakato wa katiba mpya kupitia Bunge la Katiba.
NCCR Mageuzi wameongeza kwa kusema watahakiisha wanaitisha muafaka wa kitaifa ili kutengeneza matakwa na kupatikana kwa katiba mpya.
Kwa upande wao chama tawala CCM hawanadi suala hili, licha ya serikali ya awamu nne kuanzisha mchakato huo na kuliweka katika ilani ya uchaguzi 2015-2020 pamoja na hotuba ya rais John Magufuli wakati akifungua Bunge la 11 alisisitiza kuendelezwa kwa mchakato wa katiba mpya.
Muundo wa muungano: CCM inasisitiza muundo wa Muungano wa serikali mbili za Tanzania na Mapinduzi Zanzibar.
Kwa upande wao Chadema wanataka muundo wa Shirikisho lenye serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na Muungano.
Pia inasema kila mshirika wa muungano atakuwa na mamlaka kamili katika kutumia rasilimali na maliasili (Kipengele cha 3.5; a,b,c, ukurasa wa 19). Hata hivyo vyama vyote vinakubaliana umuhimu wa kuheshimu, kudumisha mshikamano ulipo katika Jamhuri ya Muungano, lakini vinatofautiana katika muundo wake.
Sekta ya Afya: Chadema wamepanga kutoa bima ya afya kwa kuingia ubia na sekta binafsi. "Itajenga itaendeleza na kutumia miundombinu ya afya kwa kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi" (Kipengele cha 6(a) ukurasa wa 42).
Katika hatua nyingine Chadema wanataka bima ya afya maalumu kwa watumishi wa vyombo vya dola na usalama wawapo kazini na wanapostaafu.
NCCR Mageuzi inasema itaendeleza sera ya ubia baina ya sekta ya umma na binafsi katika kutoa huduma za afya.
Aidha, CCM katika kipengele cha 83 (e) wanasema "kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwemo mifuko ya bima za afya ili kufikia lengo la serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote. Pia kipengele cha 83(0) kinasisitiza kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupambana na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo ugonjwa wa corona.
Tume Huru ya Uchaguzi: Vyama vya upinzani vya ACT Wazalendo, NCCR Mageuzi na Chadema vyote vinataka kuanzishwa Tume huru ya uchaguzi nchini humo.
Kwa upande wao CCM hawaonekani kuelezea hili kokote iwe kwenye mikutano ya kampeni au ilani ya uchaguzi 2020-2025.
Serikali za Mitaa: kwa upande wa Chadema wamebainisha kuwa endapo watachaguliwa kuunda serikali wataipa mamlaka serikali za mitaa kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Namba 7 na 8 ya mwaka 1982.
Wanasema serikali kuu imepora mamlaka ya serikali za mitaa. Mathalani Mamlaka ya barabara Mijini na Vijijini (TARURA) haiwajibiki kwa Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri hivyo kukwaza utawala wa kisheria.

Chanzo cha picha, BBC
ACT Wazalendo wanakubaliana na hoja hiyo ambayo inaonesha jinsi tofauti zilivyo baina ya wagombea wanaonadi sera zao kwamba serikali ya CCM inaona ni sawa kunyang'anya mamlaka ya serikali za mitaa hali ambayo inainyima kufanya uamuzi wenye tija kwa masilahi ya wananchi. "Italeta mfumo bora wa kuendesha serikali hasa za mitaa-kwa kuwezesha ugatuaji madaraka zaidi kwa serikali za mitaa badala ya serikali kuu" (kipengele cha 2.4.1 kifungu cha V ilani ya ACT Wazalendo).
NCCR Mageuzi inasema itahamisha madaraka kutoka serikali kuu kwenda mamlaka ya serikali za mitaa.
Elimu na wanafunzi wajawazito: NCCR Mageuzi sera yao inasisitiza wanafunzi wote hata walio na mimba wanatakiwa kurejeshwa shuleni kuendelea na masomo, lakini pia wanasisitza elimu ya sekondari ya miaka miwili kama ilivyo kwa kidato cha tano na sita.
Ilani ya CCM 2015-2020 ilipendekeza wanafunzi waliopata mimba warejee shuleni, hata hivyo serikali yake haikutekeleza mpango huo na ikatupilia mbali.
Katika ilani ya 2020-2025 ya CCM suala la wanafunzi wajawazito kurejeshwa shuleni halizungumziwi popote na hata mikutano ya kampeni inaonena hilo si miongoni mwa ajenda zake za kuombea kura.
Mfumo wa utawala: Chadema wananadi sera yao ya utawala wa majimbo na mitaa.
Kwamba Chadema watahakikisha mfumo wa serikali za Majimbo na Mitaa unakuwa huru katika kubuni, kukusanya na kutumia mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani.
Ni tofauti na chama tawala CCM wanaonadi mfumo wa utawala wa mikoa na wilaya zake.












