Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maajabu! Tumbili aiba simu na kujipiga selfie
Mwanamume mmoja raia wa Malaysia amepata picha za selfie za tumbili na video katika simu yake iliyokuwa imepotea karibu na msitu uliyo nyuma ya nyumba yake.
Picha hizo - zilizojumuisha kanda ya video inayomuonesha tumbili akijaribu kula simu imesambazwa sana katika mitandao ya kijamii tangu Zackrydz Rodzi ilipoiweka kwenye Twitter.
Mwanafunzi huyo anasema alikuwa anadhani simu yake iliibiwa akiwa amelala.
Lakini hakubainisha jinsi simu hiyo ilivyopotea.
Pia ilikuwa vigumu kuthibitisha mazingira ya jinsi picha hizo na video zilivyonaswa katika simu yake.
Bwana Zackrydz, 20, ameiambia BBC kwamba aligundua simu yake imepotea alipoamka usingizini karibu saa tano asubuhi ya Jumamosi.
"Hakukua na ishara ya wizi. Kile kilichosalia katika mawazo yangu ni kwamba huenda ni mazingaombwe flani," alisema mwanafunzi huyo wa sayansi ya kompyuta kutoka Batu Pahat katika jimbo la kusini la Johor.
Saa kadhaa baadae, katika kanda ya video iliyowasilishwa kwa BBC ilionesha picha hizo zilipigwa siku hiyo hiyo saa nane na dakika moja mchana, ikimuonesha tumbili akijaribu kula simu hiyo. Mnyama huyo anaonekana akiangalia ndani ya kamera karibu na majani ya kijani akizungukwa na ndege wengi.
Pia kulikuwa na msururu wa picha za tumbili, miti na picha za sehemu ya simu kwa upande mwingine,
Bwana Zackrydz anasema hakufanikiwa kuipata simu yake hadi Jumapili mchana baada ya baba yake kumuona tumbili karibu na nyumba yao.
Alipojaribu kupiga simu yake aliisikia ikilia katika kichaka karibu na ua lao, na hapo ndipo aliona simu iliyokuwa kwenye matope chini ya mti wa mnazi.
Mjomba wake alimtania huenda kuna picha ya mwezi kwenye simu, alisema, baada ya kuisafisha aliangia kwenye sehemu ya picha na hapo ndipo "alikutana na picha nyingi za tumbili".
Tofauti na maeneo mengine ambako tumbili wanaishi karibu na maeneo ya mijini, hakujashuhudiwa visa vya tumbili kuiba vitu ndani ya nyumba katika mtaa huo, alisema mwanafunzi huyo. Ansashuku huenda tumbili huyo aliingia ndani ya nyumba kupitia dirisha la chumba cha ndugu yake iliyokuwa wazi.
"Vitu vingine huenda ukaviona mara moja nadani ya karne," aliandika ujumbe kwenye Twitter yake siku ya Jumapili na kuweka picha za tumbili huyo ambayo ilisambazwa mara zaidi ya elfu moja, kisa ambacho pia kilangaziwa na vyombo vya habari mjini humo.
Hii sio mara ya kwanza selfie ya nyani kugonga vichwa vya habari. Mwaka 2017, mpiga picha wa Uingereza alishinda mzozo wa kisheria wa miaka miwili ya dhisi ta kundi la kutetea haki ya wanyama kufuatia picha iliyopigwa na mnyama huyo.
2011, Naruto, nyani katika msitu wa Indonesia, alichukua kamera ya David Slater na kujipiga picha kadhaa za "selfie".
Bw. Slater alisema yeye ndiye mmiliki wa picha hizo ambazo zilisambazwa sana mitandaoni, lakini wanaharakati wa kutetea haki za wanyama, Peta walisema mnyama huyo alistahili kunufaika kutokana na picha hizo kwa sababu ni yeye aliyepiga picha.
Mahakama ya Marekani iliamua kuwa haki miliki haijumuishi nyani na kutupilia mbale kesi ya Peta, lakini Bw. Slater alikubali kutoa msaada wa 25% wa faida ya siku zijazo zitakazotokana na picha hizo kwa shirika hilo kulinda Naruto na wanyama wengine katika msitu wa Indonesia.