Uchaguzi Tanzania 2020: Bernard Membe kuwania urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo

Membe alipokelewa rasmi ACT-Wazalendo tarehe 16 Julai.

Chanzo cha picha, MEMBE/TWITTTER

Mshauri Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo Bernard Membe ameidhinishwa kuwa mpeperusha bendera wa chama cha ACT- Wazalendo kwa nafasi ya urais, upande wa Tanzania bara katika uchaguzi Mkuu wa Tanzania utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe amepata kura za NDIO 410 sawa na asilimia 97.61 ya kura zilizopigwa , huku kura za HAPANA zikiwa 10 sawa na asilimia 2.39 za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Uanachama wa membe katika ACT- Wazalendo ulitangazwa Mwezi Julai na kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe katika mkutano wa wanahabari wadau wengine kutoka ulimwenguni kote uliofanyika katika mtandao wa Zoom.

Bernard Membe (kulia) na mpeperusha bendera ya urais kupitia CHADEMA, Tundu Lissu (kushoto)

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Membe alisema amejiunga kama mwanachama wa kawaida lakini yuko tayari kutumikia chama hicho kwa ngazi na namna yoyote ile.

"Kilichonivutia katika chama cha ACT-Wazalendo ni katiba ya chama hicho na itikadi yake ya kutaka kuleta mabadiliko," alisema Membe

Seif Sharif Hamad, mgombea urais visiwani Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Mkutano Mkuu wa ACT - Wazalendo pia umemtangaza Ndugu Seif Sharif Hamad kuwa mgombea urais visiwani Zanzibar kupitia chama hicho.

Ameahidi kutowaangusha wanachama wa chama chake.

''Ndugu zangu naomba niseme tunakwenda kuwapangusa machozi ndugu zenu wa Zanzibar, ambao mwaka 2015 walinichagua kuwa rais wao. ninakwenda kushinda, si kushinda tu , kushinda ushindi mnono.'' alisema Seif Sharif Hamad.

''Wazanzibari wategemee kurudishwa heshima ya utii wa katiba na utawala wa sheria, utengamano, Umoja wa wazanzibari kwa kurudisha maridhiano kwenye malengo na misingi yake, nitaunda serikali ya umoja wa kitaifa kulingana na masharti ya katiba ya Zanzibar.'' alisema

Mwenyekiti wa chama hicho amesema pia atasimamia haki za Zanzibar ndani ya muungano kwa kuhakikisha kuwa Zanzibar inaheshimiwa kama mshirika sawa wa muungano.