Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Burundi: Mgombea wa chama tawala Everiste Ndayishimye ashinda urais
Tume ya uchaguzi nchini Burundi imemtangaza mgombea wa chama tawala Evariste Ndayishimiye kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika juma lililopita.
Jenerali mstaafu ameshinda kwa 68.72% ya kura zilizopigwa, wakati Agathon Rwasa, kutoka chama kikuu cha upinzani akipata 24.19% ,matokeo yaliyotangazwa na tume hiyo hii leo.
Kwa kuwa Ndayishimiye amepata zaidi ya 50% ya kura, ameepuka kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.
Haya ni matokeo ya awali ya uchaguzi , ambapo matokeo ya mwisho yatatangazwa na mahakama ya kikatiba tarehe 4 mwezi Juni.
Jenerali Ndayishimiye liteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha CNDD-FDD katika kikao kisicho cha kawaida kilichofanyika Gitega, mji mkuu wa kisiasa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu ya chama tawala cha CNDD-FDD.
Bwana Ndayishimiye ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri katika siasa za Burundi walio karibu na Pierre Nkurunziza, ambaye uamuzi wake wa kuwania madaraka kwa muhula wa tatu kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ulisababisha mzozo na mgomo wa upinzani.
Wagombea wengine waliochuana kwenye kinyang'anyiro hicho ni pamoja na;
Gaston Sindimwo (Uprona) - 1.64%
Domitien Ndayizeye (Kira Burundi) - 0.57%
Léonce Ngendakumana (FRODEBU) - 0.47%
Nahimana Dieudonné - 0.42%
Francis Rohero - 0.20%
Tangu Jumamosi usiku, siku ya uchaguzi, matokeo ya kura zilizopigwa kutoka wilaya na majimbo mbali mbali nchini humo yalianza kutangazwa.
Kufikia Ijumaa Chama cha Waandishi wa Habari nchini Burundi kilitangaza kuwa mgombea wa chama tawala cha CNDD-FDD anaonekana kushinda kwa kiwango cha 80% kwa asilimia 60% ya matokeo yaliyotolewa katika wilaya
Ushindi wa Bwana Evariste Ndayishimiye ulionekana mapema kulingana na matokeo yaliyokua yakitangazwa kutoka mikoani yaliyotangazwa mwishoni mwa Juma.
Wiki iliyopita Agathon Rwasa, mgombea wa chama cha upinzani cha CNL, alisema: uchaguzi huu ni 'jambo la aibu' lililotutokea
Bwana Rwasa aliwaambia waandishi wa habari nchini Burundi kuwa "matokeo ni gishi na hayaaminiki ".
Wiki iliyopita pia Chama cha CNL kilitangaza kuwa kina ushahidi kuwa mgombea wa chama tawala aliibiwa kura.
Wagombea wakuu Evariste Ndayishimiye kutoka kwa chama tawala na Agathon Rwasa wa upinzani , waliomba utulivu huku akisubiri matokeo yanayotarajiwa tarehe 25 mwezi Mei.
Tofauti na uchaguzi uliokuwa ukifanyika miaka ya nyuma , wakati huu ni tume ya uchaguzi pekee yenye uwezo wa kutangaza matokeo.
Bwana Rwasa aliambia waandishi kwamba upinzani unashutumu kukamatwa kiholela kwa zaidi ya wachunguzi kumi katika vituo vya kupiga kura na makosa mengine ya uchaguzi.
Chama chake cha National Freedom Council CNL kilikilaumu wanachama wa chama tawala cha CNDD-FDD kwa udanganyifu unaoshirikisha , kupiga kura zaidi ya mara moja, kupiga kura kwa watu waliofariki pamoja na wakimbizi.
Tume ya uchaguzi au chama tawala hawajatoa tamko lao kuhusiana na madai hayo.
Mitandao ya Twitter, Whatsapp na Facebook ilizimwa nchini humo, wakati wa uchaguzi, BBC ilithibitisha.
Wagombea saba waligombea urais kumrithi Pierre Nkurunziza, hata hivyo wagombea wawili ndio waliopigiwa upatu zaidi, kutoka chama cha upinzani CNL Agathon Rwasa na chama tawala CNDD-FDD Evariste Ndayishimiye.
Siku ya leo inakamilisha utawala wa bwana Nkurunziza ambaye aliingia madarakani katika taifa hilo la Afrika Mashariki miaka 15 iliyopita.
Uchaguzi huo pia ulihusisha nafasi za ubunge na madiwani.
Ijapokuwa anaacha madaraka ya urais, Nkurunziza sasa atakuwa na cheo rasmi kipya cha "mshauri wa ngazi ya juu wa uzalendo."
Pia atapokea malipo ya $540,000 (£440,000) na makazi ya kifahari. Lakini haijawa wazi ikiwa atatoweka hadharani na kutumia muda wake zaidi kwa mambo mengine mfano mchezo wa soka anaoupenda.
Mchakato wa kuelekea uchaguzi- ambao wagombea saba wamejitokeza kuchua nafasi ya rais- umetawaliwa na gasia na shutuma kwamba uchaguzi hautakua wa haki na huru.
Lakini yoyote kwa atakayeshinda atatakiwa kisheria kupata ushauri kutoka kwa Bwana Nkurunziza juu ya masuala ya usalama na umoja wa kitaifa. Kama watafuata ushauri wake bado halijawa wazi.
Ingawa anaweza kuwashawishi kwa kuonesha mafanikio yake, kama vile kuanzisha elimu ya msingi bure, huduma bure za matibabu kwa wanawake na watoto, na kujenga barabara na hospitali.
Miaka mitano iliyopita, muhula watatu wa Bwana Nkurunziza ulianza wakati taifa hilo likiwa katika kipindi cha ghasia za kisiasa. Tangazo lake kwamba angegombea kuwa rais kwa miaka mitano zaidi mamlakani lilichochea hasira ambapo baadhi walihoji uhalali wa hatua hiyo kisheria.
Kulikua na jaribio la mapinduzi, mamia ya watu walikufa katika makabiliano na maelfu wakalazimika kuikimbia nchi yao . Kuchaguliwa kwake mwezi Julai 2015, ambapo alipata karibu 70% ya kura, kulielezewa kama ''mzaha'' na kiongozi wa upinzani nchini humo Agathon Rwasa, ambaye alisusia uchaguzi.
Wakati huu , Bwana Nkurunziza aliruhusiwa, baada ya kubadili katiba kugombea tena, lakini anaonekana kuchagua kuishi maisha ya ukimya.
Uchaguzi wakati wa virusi
Uchaguzi wa Jumatano pia umekosolewa kwa kuendeshwa wakati wa janga la virusi vya corona.
Burundi imerekodi visa zaidi ya 40 vya maambukizi ya virusi vya corona, ikiwa na kifo kimoja, lakini busara ya kuendesha mikutano ya kisiasa ya umati wa watu imekua ikihojiwa.
Msemaji wa serikali alisema mwezi Machi kwamba, wakati hakuna visa vilivyokua vimerekodiwa, kwamba nchi imelindwa na Mungu.
Burundi imekataa kuweka sheria kali, huku serikali ikiwashauri tu watu kuzingatia kanuni za usafi na kuepuka mikusanyiko pale inapowezekana-isipokua bila shaka mikutano ya kampeni za kisiasa.
Serikali ilitangaza kuwa waangalizi wa kigeni wa uchaguzi watalazimishwa kutengwa kwa siku 14 kuanzia siku watakapowasili nchini, jambo linaloonekana kama njia ya kuwazuwia kwenda Burundi kabisa.
Serikali ilisema kuwa waangalizi wa kigeni wa uchaguzi watalazimishwa kutengwa kwa siku 14 kuanzia siku watakapowasili nchini, jambo linaloonekana kama njia ya kuwazuwia kwenda Burundi kabisa.
''Kile tulichokiona katika miezi michache iliyopita ni kwamba fursa ya kisiasa nchiniBurundi ni ndogo " Nelleke van de Walle, anayefanyakazi katika taasisi ya utatuzi wa migogoro ya Afrika - Central Africa for the Crisis Group think-tank, aliiambia BBC.
"Kwahivyo uchaguzi unaibua maswali juu ya ikiwa utakua wa haki na huru.
Matumaini ya mwanzo mpya
Tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1962, Burundi imeshuhudia wimbi baada ya wimbi la ghasia baina ya kabila la Wahutu walio wengi na la Watutsi walio wachache
Haijawahi kuwa na kipindi cha kudumu cha amani baada ya mabadiliko ya kiongozi wake.
Melchior Ndadaye, ambaye ni Muhutu, alichaguliwa kua rais katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1993.
Lakini matumaini ya kukita mizizi ya demokrasi yaliondoshwa miezi mitatu tu ya urais wake, wakati kundi cha askari walioongozwa na jeshi la kabila la Watutsi kumuua pamoja na mawaziri kadhaa na washirika wake wa kisiasa.