Virusi vya corona: ''Dawa'' ya Madagascar inayoaminiwa kutibu virusi itachunguzwa zaidi

Prof. Paramagamba Kabudi ambaye alikwenda madagascar kuchukua ''dawa'' amesema :''Hatujachukua dawa kutoka kwa sangoma''

Chanzo cha picha, Wizara ya mambo ya nchi za nje Tanzania/Twitter

Maelezo ya picha, Prof. Paramagamba Kabudi ambaye alikwenda madagascar kuchukua ''dawa'' amesema :''Hatujachukua dawa kutoka kwa sangoma''

Baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Paramagamba Kabudi kwenda Madagascar kuichukua dawa ya mititishamba inayoaminiwa kuwa inaweza kukinga na kutibu Covid-19, Tanzania imesema dawa hiyo itachunguzwa zaidi.

Akielezea kuhusu ''dawa'' hiyo leo. Mkuu wa Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) chini humo Profesa Yunus Mgaya amesema kuwa dawa hiyo itafanyiwa uchunguzi wa kikemiana wa kibaiolojia kubaini utendaji wake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Paramagamba Kabudi ambaye alikwenda madagascar kuchukua dawa hiyo amesema:''Hatujachukua dawa kutoka kwa sangoma'' na kuongeza kuwa:''Nilikwenda Madagascar kwa ndege ya rais kupokea zawadi kutoka nchini Madagascar ''

Rais Magufuli aliniruhusu niende na wataalam, na tulipofika kule walikua na mkutano wa saa nne wa kuzungumza na wenzao kuhusiana na dawa hii '', amesema Profesa Kabudi.

Alipokua akipokea dawa ya mitishamba iliyotolewa na Madagascar kwaTanzania Ijumaa , alisema kuwa Tanzania haijalegalega katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

Waziri wa mambo ya nje Prof. Palamagamba Kabudi anasema dawa hizo ni kwa ajili ya Utafiti, na sio za kugawanywa kwa Watanzania.

'' Dawa zimekuja chupa mbili kwa ajili ya utafiti na kuna fomula ambazo zimetolewa kwa wataalamu wetu'', amesema Profesa Kabudi na kuongeza kuwa Vilevile kuna box kwa ajili ya raia wa Madagascar ambao wamepewa zawadi kutoka kwa ndugu zao huko Madagascar.

Sera ya Tanzania kuzingatiwa

Mkemia mkuu wa serikali anasema Dkt. Fidelice Makumiko amesema : ''Dawa hizi ni msaada, na hawawezi kukataa kitu ambacho wamepewa...dawa hii tumeipokea kama msaada na sio kwa ajili ya kugawa kwa wananchi ... dawa hii tumeipokea kama zawadi kwa ajili ya kufanya utafiti wakatuonyesha kuwa ni salama na haina madhara kwa wananchi wao''

''Sera ya Tanzania ilivyo lazima kuipima na kuangalia ubora wa hii dawa na kuona kuwa ina usalama unaohitajiwa. Tumepanga kuwa na makundi matatu ya wagonjwa kwa hiari yao'', amesisitiza Dkt. Fidelice Makumiko.

Akipokea msaada huo Jumamosi, Prof. Palamagamba John Kabudi alisema ''Madai yanayotolewa kuwa Tanzania imelegalega ama kujitenga katika kupambana na ugonjwa wa COVID -19 si ya kweli kwa kuwa Tanzania imetoa uongozi madhubuti katika eneo iliyopewa dhamana ya uongozi ya Uenyekiti wa nchi SADC na imeifanya na inaendelea kuifanya kwa heshima na bidii zote.'',

Bwana Kabudi aliongeza kuwa Tanzania imetoa uongozi madhubuti katika kuratibu na kuunda timu ya wataalamu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kuandaa muongozo na utaratibu wa kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za kupunguza nguvu ama kuleta tiba ya COVID - 19.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva alizitaka nchi za Afrika kuungana kwa pamoja kupata suluhisho la maradhi ya COVID 19 ambayo pia itakuwa suluhisho na faraja kwa dunia nzima, imesema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini Tanzania.

Waziri wa mambio ya nje waTanzania Paramagamba Kabudi(kulia) akionja dawa ya mititshamba kutoka Madagascar

Chanzo cha picha, WIZARA YA MAMBO YA NJE, TANZAN

Maelezo ya picha, Waziri wa mambio ya nje waTanzania Paramagamba Kabudi (kulia) akionja dawa ya mititshamba kutoka Madagascar

meongeza kuwa kila nchi Barani Afrika inawajibu wa kutekeleza ili kuupatia ufumbuzi ugonjwa huo na ni faraja kwa Madagascar kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kufika nchini humo kwa ajili ya kujionea dawa hiyo jambo ambalo anaamini kukiwa na nguvu ya pamoja ndani ya SADC mafanikio makubwa yatafikiwa.

'Dawa' ya madagascar

Tanzania leo imepokea msaada wa dawa zinazofubaza Virusi vya Corona kutoka Serikali ya Madagascar

Dawa hizo zimewasili Tanzania wakati ambapo nchini Madagascar kwenyewe idadi ya wagonjwa wa corona inaripotiwa kuongezeka licha ya kuwa na dawa hiyo ya mitishamba.

Kufikia sasa taifa hilo lina jumla ya watu 195 walioambukizwa corona licha ya kutangaza kuwa na dawa ya mitishamba iliyo na uwezo wa kutibu ugonjwa huo.

Mnamo Mei 3, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alisema kuwa atatuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa ya hiyo mitishamba.

Wakati huo Bw. Magufuli alisema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.

Shirika la Afya Duniani limesema ni muhimu dawa zinazosemekana kuwa na uwezo wa kutibu kufanyiwa majaribio kwanza na kuonya kuwa huenda watu wakaona wamepata tiba na kujihisi kuwa salama ikiwa watakuwa na imani na dawa ambazo hazijafanyiwa majaribio.

Wizara ya Afya Tanzania inasema nini?

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amewataka raia wa nchi hio kuondoa hofu baada ya serikali kukaa kimya kwa muda wa wiki moja na siku kadhaa bila kutoa takwimu za mwenendo ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu Covid19.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo, katika uzinduzi wa kituo cha huduma za simu ambacho kazi yake itakuwa ni kutoa elimu sahihi kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya ikiwamo magonjwa milipuko, waziri Ummy amesema ukimya hu umetokana na maboresho yanayoendelea katika maabara ya taifa.

"Kumekuwa na taarifa kuhusu utoaji wa taarifa za mwenendo wa covid19 nchini. Niseme tu ndugu wanahabari kama mnavyofahamu kwa kipindi cha takriban siku saba au wiki moja, hatukuweza kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa Covid19, kutokana na kuwa sasa hivi tunafanya zoezi la maboresho ya kudumu za maabara ya taifa ya afya ya jamii, kama mnavyofahamu kuna kazi za kiufundi zinaendelea kwa hivyo niwatoe watu hofu tu kwamba ndani ya siku chache kazi itakuwa imekamilika na hivyo tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara," amesema Waziri Ummy

Wakati huo huo, waziri amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ambazo zimetolewa na wataalamu wa afya na kusema Covid19 bado ipo, na itaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa ijayo.

coronavirus
Life under lockdown divider

Mara ya mwisho kwa Tanzania bara kutoa takwimu za maambukizi ilikuwa ni wiki iliyopita ambapo kulikuwa na jumla ya watu 480 waliopata Covid19.

Hata hivyo, idadi hiyo itakuwa imeongezeka baada ya Serikali ya Zanzibar jana kutoa takwimu mpya zinazoonyesha kuongezeka kwa maambukizi visiwani Unguja na Pemba.

Itakumbukwa kwamba, mwishoni mwa juma lililopita, akimwapisha waziri mpya wa Katiba na Sheria, Rais Magufuli alionyesha kutilia shaka majibu ya vipimo yanayotoka katika Maabara ya Taifa, hasa baada ya kusema kuwa wamepeleka sampuli za matunda na wanyama na majibu kuonyesha kuwa yana Covid19.

Mbali na kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa mkurugenzi wa Maabara hiyo ili kupisha uchunguzi, maboresho yanayoendelea katika maabara hiyo, inaonyesha ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.

Maelezo ya video, Virusi vya corona:Vidokezo tano ya jinsi ya kuimarisha afya yako ya kiakili

Unaweza pia kutazama: