Virusi vya corona: Bobi Wine ajitolewa kuwarejesha makwao waafrika 'wanaobaguliwa' China

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamuziki na mbunge wa Uganda Kyangulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine, amesema kuwa ameungana na mfanyibiashara wa Marekani kuwarejesha nyumbani waafrika wanaodaiwa kubaguliwa China.
Hii ni baada ya taarifa kuibuka kuwa mamia ya watu wenye asili ya kiafrika kufurushwa kutoka majumbani mwao katika mji wa China wa Guangzhou kutokana na hofu kuwa virusi vya corona vinasambazwa na jamii ya kiafrika.
Bobi Wine amesema yeye na mfanyibiashara wa Neil Nelson wako tayari kuwasafirisha makwao watu hao ikiwa mataifa yao yatakuwa tayari kuwapokea.
Wawili hao pia wana mpango wa kuwasafirisha Marekani watu walio na uraia wa nchi hiyo ama wale waliopewa hadhi ya mkazi wa kudumu Marekani.
"Tunatoa wito kwa serikali ya China kukomesha ubaguzi dhidi ya watu weusi," walisema katika taarifa ya pamoja.

Nigeria, kupitia ubalozi wake mjini Beijing, ilisema inajiandaa kuwaondoa raia wake nchini China.
Hali ya taharuki imetanda katika mji waGuangzhou kufuatia hofu inayozunguka maabukizi ya virusi vya corona.
Kwa mujibu wa kiongozi wa kijamii mamii ya Waafrika wameshindwa kurejea katika nyumba zao ama hoteli baada ya madai kuibuka kuwa jamii ya watu weusi inasambaza virusi hivyo hatari.
Mamlaka katika mkoa wa Guangdong imejibu madai ya ubaguzi dhidi ya waafrika na kuingeza kuwa China na Afrika ni marafiki wazuri, washirika na ndugu.
Ilisema "mataifa ya Afrika yana umuhimu mkubwa''... na kwamba juhudi zinafanywa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hiyo na Afrika".
Lakini mjini Guangzhou baadhi ya watu wanahoji jinsi wafrika wanavyotelekezwa.
Mwanafunzi mmoja kutoka nchini Nigeria ambaye hakutaka jina lake liytajwe ameiambia BBC KUWA alifurushwa kuroka nyumbani kwake , kukamatwa na kuwekwa karantini kwa lazima.
"Tafadhali tunaomba ulimwengi utuokoe. Jinsi serikali ya China inavyotufanyia haifai. Walinikamata na kunipeleka karantini na kunilazimisha [mimi] kulipa malazi katika hoteli," alisema.
Kanda za video zinazoonesha raia wa mataifa wa Afrika wakiwa barabarani zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii.
Moja ilionesha kundi dogo la wafanyibiashara wa kichina wakiandamana katika eneo ambalo wafanyibiashara wa kiafrika wamekuwa wakikusanyika kulalamikia hali yao. Wanadai biashara zao zimeathiriwa vibaya kwasababu waafrika wengi hawawezi kufanya biashara.
Video nyingine iliyoonekana na BBC inaashiria jinsi wenye nyumba ambao ni raia wa kichina wakiomba msamaha wapangaji.
"Raia wa kigeni hawawezi kuishi hapa tena,samahani kwa hilo. Tunazingatia kanuni ya usimamizi wa mamlaka ya kijamii. Sio vile mnavyofikiria. Mambo yatakuwa sawa," alisema.














