Coronavirus: Baadhi ya sehemu za mji wa Wuhan zafunguliwa baada ya kufungwa kuzuia maambukizi China

Wengi wa raia waliokuwa wakiwasili mjini Wuhan siku ya Jumamosi walibeba mabegi makubwa wakirudi katika familia zao

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wengi wa raia waliokuwa wakiwasili mjini Wuhan siku ya Jumamosi walibeba mabegi makubwa wakirudi katika familia zao

Mji wa China ambapo mlipuko wa virusi vya corona ulianza , Wuhan umefungua baadhi ya sehemu zake baada ya kutengwa kwa miezi miwili.

Makundi ya abiria yalipigwa picha yakiwasili katika kituo cha treni cha Wuhan siku ya Jumamosi. Watu wanaruhusiwa kuingia lakini sio kutoka, kulingana na ripoti.

Wuhan ambao ndiiu mji mkuu wa jimbo la Hubei uliandikisha visa 50, 000 vya maambukizi .Takriban watu 3000 walifariki katika jimbo hilo kutokana na virusi hivyo.

Lakini idadi hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa , kulingana na takwimu za China.

Serikali siku ya Jumamosi iliripoti visa vipya 54 ambavyo inadai vilitoka nje ya nchi.

Huku ikiendelea kukabiliana na visa kutoka ughaibuni , China imetangaza marufuku ya muda kwa wageni wote hata iwapo wanamiliki Viza ama vyeti vya kuishi .

Pia imepunguza idadi ya ndege za China na zile za kigeni kusafirisha abiria mara moja kwa wiki, huku ndege hizo zikitakiwa kubeba asilimia 75 pekee ya abiria katika ndege moja.

Maelezo zaidi
Banner

Je kuna ishara gani kuonyesha kwamba mji wa Wuhan unafunguliwa?

Virusi hivyo vinadaiwa kuanzia katika soko moja la vyakula vya baharini ambalo lilikuwa likiuza wanyama pori kinyume na sheria.

Wakaazi milioni 11 wa mji huo walitengwa na ulimwengu tangu katikati mwa mwezi Januari , huku vituo vya kukagua magari vikiwekwa mbali na masharti makali yaliozuia maisha ya kawaida kuendelea.

Lakini barabara zilifunguliwa kuruhusu magari yanayoingia jioni siku ya Ijumaa kulingana na chombo cha habari cha Reuters.

Na vyombo vya habari vya serikali vilisema kituo cha ardhi cha treni kilifunguliwa siku ya Jumamosi na sasa treni zitaweza kuwasili katika vituo 17 vya reli mjini humo.

Mwanafunzi wa miaka 19 Guo Liangkai , ambaye alirudi mjini humo baada ya miezi mitatu , aliambia Reuters: Kwanza inanifurahisha kuona familia yangu tena.

''Tulitaka kukumbatiana lakini huu ni wakati maalum hatuwezi kufanya hivyo ama kufanya kitendo kama hicho''.

Raia waliovaa barakoa wakisubiri katika kituo cha treni mjini Wuhan siku ya Jumamosi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Raia waliovaa barakoa wakisubiri katika kituo cha treni mjini Wuhan siku ya Jumamosi

Wote waliowasili Wuhan wanalazimika kuonyesha programu ya kijani katika simu zao ili kuonyesha kwamba afya yao ni salama.

Maafisa wanasema kwamba masharti kwa watu wanaotoka mjini humo yataondolewa tarehe nane mwezi Aprili , wakati ambapo ndege zitaanza kufanya kazi.

Virusi hivyo vililipuka nchini China mwezi Disemba na zaidi ya watu 3,300 wamefariki kutokana na maambukizi - lakini sasa Itali na Uhispania ndizo zenye idadi kubwa ya waliofariki.

China sasa inakabiliana kudhibiti wimbi la visa vya raia wanaoingia nchini humo huku maambukizi yakisambaa katika mataifa mengine ya kigeni.

Wimbi hili la pili la maambukizi kutoka ugenini pia linaathiri mataifa kama vile Korea Kusini na Singapore , ambayo yalifanikiwa katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika wiki za hivi karibuni.

Mji wa Wuhan

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wuhan ilikuwa imetengwa tangu katikati mwa mwezi Januari.