Coronavirus: Fahamu kwanini idadi ya vifo vya coronavirus iko juu Italy?

Pia makanisa yamenyunyiziwa dawa ya kuuwa virusi vya corona Itali.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Pia makanisa yamenyunyiziwa dawa ya kuuwa virusi vya corona Itali.

Mlipuko wa virusi vya corona unaendelea kuliathiri pakubwa taifa la Italy, huku hospitali zikishindwa kumudu idadi ya maambukizi mbali na kuwekwa kwa sheria ya kutotoka nje.

Lakini wataalam wana wasiwasi kuhusu kiwango cha juu cha vifo huku idadi ya watu waliofariki ikiipiku ile ya China.

Kati ya visa 86,500 vya maambukizi vilivyothibitishwa nchini Italy , watu 9,134 kufika sasa wamekufa.

Taarifa zaidi kuhusu coronavirus

Cha kushangaza ni kwamba China ilikuwa na visa vingi zaidi lakini ni watu 3,274 pekee waliofariki.

Hii inamaanisha kwamba asilimia tisa ya visa vya corona vilivyothibitishwa nchini Italy wamefariki , ikilinganishwa na asilimia nne nchini China.

Kwa kiwango hicho Ujerumani , ambayo kufikia sasa imebaini visa 50,871 na vifo 351 ina asilimia 0.5 ya viwango vya vifo.

Hivyobasi tunauliza ni kwanini viwango vya vifo nchini Itali viko juu?

Raia wote wa Italy wametakiwa kusalia majumbani mwao kwa takriban wiki mbili

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Raia wote wa Italy wametakiwa kusalia majumbani mwao kwa takriban wiki mbili

Kulingana na Profesa Prof Walter Ricciardi, ambaye ni mshauri wa kisayansi wa wizara ya afya nchini Itali, vifo nchini humo ni vingi kwa kuwa taifa hilo ndilo lenye watu wazee zaidi duniani mbali na jinsi hospitali zinavyorekodi vifo.

''Umri wa wagonjwa wetu hospitalini uko juu, huku umri wa wastani ukiwa 67 ikilinganishwa na China ambauo umri wao wa wastani ni miaka 47'', anasema Profesa Ricciardi.

Wagonjwa wengi ni wazee ndio maana viwango vya vifo viko juu.

Utafiti mmoja uliofanywa nchini humo ulibaini kwamba asilimia 40 ya visa vya maambukizi na asilimia 87 ya vifo nchini humo vimekuwa katika wagonjwa walio na zaidi ya umri wa miaka 70.

Na kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya Imperial mjini London, idadi kubwa ya watu wenye umri huo watahitaji uangalizi wa karibu.

Profesa Ricciardi pia amesema kwamba viwango vya vifo nchini Itali vinaweza kuwa vya juu kutokana na jinsi madaktari wanavyovirekodi .

"Jinsi tunavyorekodi visa vyetu vya vifo ni kwamba watu wote wanaofariki wakati wa janga hili wanafariki kutokana na virusi vya corona''.

Taasisi ya kitaifa ya afya ilisema kwamba umri wa wastani wa wale waliofariki ni miaka 81 , huku idadi kubwa yao wakiwa wanaugua magonjwa mengine.

Idadi ya watu waliofariki kutokana na via virusi vya corona imeongezeka na kuipita idadi ya China
Maelezo ya picha, Idadi ya watu waliofariki kutokana na via virusi vya corona imeongezeka na kuipita idadi ya China

Asilimia 72 ya wale waliofariki kutokana na virusi hivyo ni wanaume. Kulingana na data, asilimia 4.25 ya watu waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona wamefariki , ikiwa ndio kiwango cha juu duniani.

Ni asilimia 12 pekee ya vibali vya vifo ambavyo vimeonyesha waathiriwa wa moja kwa moja wa virusi vya corona .

Hiyo haimaanishi kwamba covid 19 haikuchangia vifo vya wagonjwa hao bali inaonyesha kwamba Itali inaongoza kwa watu waliokuwa wakiugua maradhi mengine

Je nini kinachoendelea Itali?

Serikali wiki iliopita iliagiza kufungwa kwa shule zote kwa siku 10 wakati ambapo inajaribu kukabiliana na maambukizi ya coronavirus.

Michezo yote zikiwemo mechi za ligi ya Serie A zitachezwa bila mashabiki uwanjani kwa mwezi mmoja.

Mwandishi wa BBC mjini Rome Mark Lowen alichapisha ujumbe wa twitter kwamba mkaazi mmoja katika mji uliotengwa wa Codogo nchini Itali alimwambia kwamba kitu kinachowaudhi wengi katika eneo hilo ni kwamba mazishi ya waathiriwa wa ugonjwa wa coronavirus hayaruhusiwi kutokana na umuhimu wa kupunguza mikutano ya watu wengi.