Coronavirus: Serikali zinavyolazimika kupiga marufuku raia wake na je, hilo ni muhimu?

Kadri siku zinavyosonga mbele, ndivyo dunia inavyoingia katika mapambano zaidi dhidi ya virusi vya corona.

Ndani ya saa 24 zilizopita, nchi za Mauritius, Uingereza na Afrika Kusini zimetangaza marufuku ya watu kutoka nje, ama 'lockdown'.

Kwingineko ni Senegal na Ivory Coast wamechukua hatua ya kutangaza dharura ya kitaifa na kuweka marufku ya watu kutembea usiku.

Hizi ni baadhi ya hatua za juu zaidi katika kupambana na virusi vya corona, baada ya ushauri wa watu kujitenga na kufanyia kazi nyumbani kutoleta matokeo tarajiwa.

Mpaka sasa zaidi ya watu 300,000 (laki tatu) wameambukizwa virusi vya corona na watu 16,100 tayari wameshapoteza maisha.

WHO imetoa tahadhari juu ya kasi ya kuenea kwa janga hilo.

Nchini Mauritius serikali ya visiwa hivyo imechukua hatua hiyo kali baada watu wawili kufariki na wengine 28 kukutwa na ugonjwa wa Covid-19.

Nchi hiyo ambayo inategemea utalii kwa kiasi kikubwa ina raia milioni 1.2 tu, na marufuku imewekwa kwa wiki moja kwanza kuangalia hali ya mambo itakavyokuwa.

Rais wa Afrika Kusini Cyrill Ramahosa jana usiku ametangaza marufuku ya wiki tatu, na watu wataruhusiwa kwenda kununua chakula na mahitaji maalumu tu.

Kwa sasa Afrika kusini ina wagonjwa 402.

Rais Cyril Ramaphosa alitangaza amri ya watu kutokutoka nje Afrika Kusini kwa muda wa wiki tatu kuanzia usiku wa alhamisi ili kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.

Nchini Uingereza tayari marufuku ya watu kutokutoka nje inafanya kazi. Watu pekee wanaoruhusiwa kutoka ni wahudumu wa afya, maafisa wa usalama. Maduka ya chakula na vitu muhimu nayo yapo wazi.

Amri hiyo ilitangazwa jana na waziri mkuu Borris Johnson.

Rais Macky Sall wa Senegal amesema hali ya dharura kwa taifa itaanza usiku wa Jumanne saa sita usiku .

Wanajeshi na polisi wametakiwa kusimamia amri hiyo.

"Tangu mgonjwa wa kwanza kubainika nchini serikali inapaswa kuweka mipango kuharakisha mipango ya kukabiiana na ugonjwa huo. Iko wazi kuwa tuna safari ndefu," alisema.

Senegal imethibitisha kuwa na wagonjwa 79 wa Covid-19, ambapo 11 wamethibitika kupona ugonjwa huo.

Kwa nini hatua hizi ni muhimu

Virusi vya corona vinasambaa haraka kwenye msongamano wa watu.

Pale mtu mwenye mambukizi anapopiga chafya ama kukuhoa, virusi hutapakaa kwenye hewa na vitu vilivyo karibu.

Watu watakaokuwa karibu naye watapata maambukizi kwa kuta hewa yenye virusi ama kusika vitu ambavyo vijidudu viliangukia na kisha kushika nyuso zao hususani mdomo, macho na pua.

Pale watu watakapotangamana kwa muda mchache, ndio uwezekano wa maambukizi huwa mdogo zaidi.

Kwa mujibu wa wataalamu, endapo watu watakapojitenga ama mikusanyiko ya watu ikizuiliwa, basi kasi ya maambukizi itashuka na kudhibitiwa.

"Mataifa ambayo yalichukua hatua kali tangu mwanzoni wanaonekana kuwa mbali katika jitihada za kukabiliana na maambukizi haya ya ugonjwa wa corona," ameeleza rais Ramaphosa na kuongeza: "Inatupasa kufanya kila kitu kilicho chini ya uwezo wetu ili kupunguza idadi ya maambukizi ya virusi vya corona."

Waziri Mkuu wa Mauritius Pravind Jugnauth amesema kinachoendelea ni sasa ni "vita" na ni muhimu kwa hatua stahiki kuchukuliwa.

Bwana Jugnauth amesema kuwa awali watu hawakuheshimu ushauri wa awali wa kujitenga.

"Hali inaweza kuwa mbaya pale watu wajinga (ambao hawataheshimu marufuku) na kuhatarisha ya watu wote."

Hatua za kuzuia mikusanyiko ya watu zimepigwa katika shughuli za burudani na mashindano kadhaa ya michezo ikiwemo Ligi ya England kuahirishwa.

Hata shughuli za kidini zimetatizika huku nchi kadhaa ulimwenguni zikifunga misikiti na makanisa.