Coronavirus: Raia wa Cameroon ni mtu wa pili kupatikana na virusi DR Congo

Afisa wa matibabu akivalia barakoi kujilinda dhidi ya virusi vya corona nchini Uganda

Chanzo cha picha, Getty Images

Kisa cha pili cha maambukizi ya ugonjwa wa coronavirus kimethibitishwa nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Mtu huyo anadaiwa kuwa raia wa Cameroon aliyewasili nchini humo kutoka Ufaransa kulingana na mwandishi wa BBC mjini Kinshasa .

Kwa sasa amelazwa hospitalini kwa matibabu. Wizara ya afya nchini humo imetoa wito kwa raia kuzingatia usafi wakati wowote.

Mgonjwa huyo ni raia wa umri wa miaka 46 ambaye anaishi DR Congo na familia yake .

Alirudi nchini humo kutoka Ufaransa mwezi Mei 8 na hakuonyesha dalili za virusi hivyo.

Mamlaka ya DR Congo inasema kwamba kufikia sasa imewatambua watu 117 waliogusana na wagonjwa wawili wa virusi hivyo.

Habari hiyo inajiri siku moja baada ya madaktari nchini DR Congo kuamua kurudi kazini wakisitisha mgomo wa miezi miwili.

Mwandishi wa BBC anasema kwamba muungano wa madaktari ulikubaliana na serikali kuimarisha mazingira yao ya kazi

Kisa cha kwanza cha virusi vya Corona

Afisa wa matibabu akivalia barakoi kujilinda dhidi ya virusi vya corona

Chanzo cha picha, Reuters

Kisa cha kwanza cha virusi vya Corona kilithibitishwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku ya Jumanne kulingana na msemaji wa wizara ya afya .

Mgonjwa huyo ni Mkongo wa miaka 52 aliye na kibali cha kuishi Ufaransa, ambaye aliingia nchini humo siku wikendi iliopita na alikuwa amewekwa karantini baada ya uchunguzi aliofanyiwa katika uwanja wa ndege wa Kinshasa kubaini kuwa ameambukizwa virusi hivyo.

Kwa sasa anapatiwa matibabu katika kituo cha zamani cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola mashariki mwa mji mkuu wa Kinshasa.

Wizara ya afya ya DRC imesema kuwa inajaribu kuwatafuta watu wengine waliyesafiri na mgonjwa huyo ili wawekwe karantini katika juhudi za kudhibiti maambukizi.

Waziri wa afya Eteni Longondo ametoa wito wa utulivu na kuzingatia usafi kwa kuosha mikono yao mara kwa mara.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya 11 ya Afrika kuthibitisha maambukizi ya ugonjwa hatari wa Covid-19.

Ugonjwa huo ambao ulianzia China umewaua zaidi ya watu 3 800.

DR Congo kwa sasa imeimarisha uchunguzi katika viwanja vyake vinne vikuu vya ndege kwa kuwakagua kwa makini wasafiri walio na viwango vya juu vya joto- hatua ambayo imekuwa ikichukuliwa kama sehemu ya kupambana na maambukizi ya virusi hatari vya Ebola.

Tunazidi kukupasha.....