Coronavirus: Jinsi raia wa China wanavyobaguliwa Kenya

Huku dunia ikiendelea kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona katika mataifa tofauti, raia wa China na bara Asia wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi.

Nchini Kenya , wafanyakazi wa China wamefukuzwa kutoka vituo viwili vya ujenzi huku wengine wakitukanwa kuhusiana na virusi vya corona.

Wachina ambao wamekuwa wakiendesha biashara wame torokwa na wateja hatua inayosababisha kufutwa kazi kwa baadhi ya wafanya kazi wa bishara hizo.

Kanda moja ya video ambayo imekua ikisambaa nchini Kenya kuhusu raia wawili wa China wanaobaguliwa kwasababu ya hofu ya ugonjwa wa virusi vya corona katika mtaa wa mabanda imezua hisia kali katika mitandao ya kijamii.

Wengine wameambia BBC kwamba hata madereva wa teksi wamekuwa wakikataa kuwabeba kwa hofu ya maambukizi ya virusi hivyo vilivyoanza mjini Wuhan huko China.

Hatua hii inajiri baada ya baadhi ya raia wa China kufukuzwa katika viwanda vya ujenzi huku wiki iliopita wengine wao wakivamiwa na kutishwa kufurushwa majumbani mwao.

Guu Shajar , raia wa China ambaye ameishi Kenya miaka sita alikuwa nchini China kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita lakini alipokuwa katika safari yake ya ndege kutoka Ghana amedai kwamba alibaguliwa na kunyanyaswa na maafisa katika uwanja wa ndege wa JomoKenyatta Nairobi licha ya kutimiza maagizo yote aliopewa.

''Kulikuwa na majibizano makali, mwanamke aliyekuwa katika kituo cha afya alisema hawezi kukiachilia cheti changu cha afya huku abiria wengine wakisalia katika foleni kwani waliamua kubishana badala ya kufanya kazi yake. Walinipigia kelele wakisema kwamba hii ni Kenya'', alisema.

''Najua mimi sio wa kwanza na wa mwisho kubaguliwa kwasababu raia wengi wa bara Asia wanaoishi katika mataifa ya Afrika hawapendi fujo''.

Lakini maafisa katika uwanja huo wamepinga madai hayo ya ubaguzi wakisisitiza kuwa wasafiri wote huchukuliwa na kuhudumiwa sawa pamoja na kupewa heshima.

Vilevile migahawa na biashara zinazomilikiwa na raia wa China zimekuwa na wakati mgumu kupata wateja kutokana na hofu hatua inayowafanya watu wengi kukataa kwenda katika maeneo hayo.

Huku safari zote za moja kwa moja kati ya Kenya na China zikisimamishwa , wateja wa kawaida kutoka bara Asia wamekuwa nadra kupatikana.

Huwei ni mmiliki wa hoteli nchini Kenya kwa zaidi ya miaka sita na sasa anasema kwamba anatafakari iwapo anaweza kuwafuta wafanyakazi wake kutokana na biashara mbovu.

''Tumepoteza miezi miwili bila wageni kutoka bara Asia, Tumepoteza wageni kutoka Ulaya na Marekani na baada ya kuwapoteza wageni hao soko la nchini limekuwa likiyumba yumba'', aliongezea.

Februari 27, ujumbe ulisambaa katika mtandao wa Facebook, ukidai kuwa mbunge mmoja wa Kenya ametaka wananchi wa jimbo lake kuepuka kuwa na muingiliano na raia wa China ambao wamerejea kutoka kwao baada ya sherehe za mwaka mpya wa China.

Ujumbe huo ulionya kuwa kama serikali haitawalinda raia wake, basi watalazimika kuwaweka raia wote wa China katika karantini.

Na vilevile wananchi watakuwa na ruhusa ya kumkimbiza yeyote kwa mawe katika jimbo lao.

Ubalozi wa China' ulijibu madai hayo haraka kwenye kurasa ya Twitter kutaka jumuiya za watu kutoka China kulindwa na watu kuacha ubaguzi.

Si Kenya peke yake ambayo ilionyesha chuki ya aina hiyo bali kuna mataifa mengine ya angwa la sahara ambayo yanahusisha wasafiri waliotoka China.

Huku kukiwa hakuna unyanyapaa wa aina hiyo kwa wageni kutoka ulaya.

Kabla ya Kenya haijarekodiwa kwa kesi hiyo lakini chanzo cha hayo yote ni hofu na mchanganyiko wa unyanyapaa.