Erdogan: EU haijatoa msaada wowote kuhakikisha wakimbizi wa Syria wanaishi ''maeneo salama'' nchini Syria.

Rais wa Uturuku ametoa tahadhari kuwa ''mamilioni'' ya wahamiaji na wakimbizi hivi karibuni wataelekea barani ulaya.

Recep Tayyip Erdogan alikuwa akizungumza baada ya kutangaza kuwa Uturuki haitatekeleza tena makubaliano ya mwaka 2016 na Umoja wa Ulaya kuwazuia wahamiaji kuingia Ulaya.

Polisi nchini Ugiriki wametumia gesi ya kutoa machozi kuwazuia maelfu ya wahamiaji kuingia nchini humo na kulitaka shirika la Frontex la umoja la Ulaya lililo mpaka kutoa msaada wa haraka kudhibiti hali hiyo.

Erdogan amesema Uturuki haiwezi kudhibiti wimbi jipya la wakimbizi kutoka Syria.

Karibu raia wa Syria milioni moja wamekimbilia kwenye mpaka Uturuki akitokea Idlib, wakikimbia mapigano makali kati ya waasi wanaoungwa mkono na Uturuki na vikosi vya kijeshi vya serikali ya Syria.

Uturuki tayari ina wakimbizi milioni 3.7 kutoka Syria, pia wahamiaji kutoka nchi nyingine kama vile Afghanistan- lakini awali waliwazuia kwenda Ulaya.

Katika taarifa iliyotolewa kwa njia ya Televisheni, Bwana Erdogan amesema EU haijatoa msaada wowote kuhakikisha wakimbizi wa Syria wanakaa katika ''maeneo salama'' nchini Syria.

Baada ya Uturuki kufungua milango kwa wahamiaji kuondoka kwenye himaya yake kwenda Ulaya juma lililopita, alisema, ''mamia wamevuka, na hivi karibuni watafika mamilioni''.

Kiongozi wa Uturuki hajatoa ushahidi wa takwimu zakehuku Ugiriki ikisema karibu wahamiaji 1,000 walifika mashariki mwa visiwa vya Aegean wakitokea Uturuki tangu Jumapili asubuhi.

Kwa kuongezea, Ugiriki imesema iliwazuia karibu wahamiaji 10,000 kuvuka ardhi yake ya mpakani kwa saa 24. Baadhi ya wahamiaji walirusha mawe na vipande vya chuma walipozuiwa, na waliznzi wa mpaka wa Ugiriki walifyatua gesi za kutoa machozi.

Mbali na raia wa Syria, kuna raia wa Afghanistan na Afrika Magharibi katika eneo la mpaka.

Unaweza pia kusoma

Rais wa baraza la EU Charles Michel na rais wa tume ya EU Ursula von der Leyen watakwenda kwenye eneo la mpaka na Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis siku ya Jumanne.

''Ama tuwaweke watu hawa katika mazingira mazuri katika ardhi yao, au kila mmoja apate sehemu ya mzigo huu. Sasa kipindi cha kujitoa kafara kimekwisha,'' Erdogan ameeleza.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, serikali ya Ugiriki imesema, ''Uturuki, badala ya kupambana na chaneli za wasafirishaji wa wahamiaji na wakimbizi, yenyewe ndio imekuwa msafirishaji.''

Ugiriki imezuia maombi mapya ya hifadhi kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao, kwasababu ya kile ilichokiita ''uratibu wa usafirishaji wa wahamiaji'' kutoka Uturuki.

Frontex imesema kuwa inatazama namna nzuri zaidi ya kuisaidia Uigiriki kwa kupeleka walinzi wa EU eneo la mpaka.

Frontex ina maafisa karibu 400 ndani na kuzunguka visiwa Ugiriki, maafisa 60 nchini Bulgaria na wengine katika mji wa Evros, katika eneo la mpaka wa Ugiriki na Uturuki.