Virusi vya Corona: China yailaumu Marekani kwa kueneza 'taharuki' kuhusu virusi hatari

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya China imeishutumu Marekani kwa kusababisha taharuki kutokana na mapokezi yake ya mlipuko wa ugonjwa wa corona.
Hii inakuja baada ya Marekani kutangaza dharura ya kiafya na kukataza raia wa kigeni ambao walitembelea China wiki mbili zilizopita.
Zaidi ya watu 17,000 wamethibitika kuwa na virusi vya corona nchini China. Huku wengine 361 wakifariki kutokana na ugonjwa huo.
Nje ya China kuna watu 150 wamethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa corona huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki nchini Ufilipino.
Virusi hivyo vinadaiwa kuanza kwa dalili za homa kali na kufuatia na kikohozi kikavu.
Siku ya Jumatatu, mtaalamu wa afya nchini China alibainisha kuwa utafiti unaonyesha kuwa virusi hivyo vinahusishwa kuanzishwa na popo.
Hatua gani Marekani imechukua?
Januari 23, Marekani ilitoa agizo la dharura kwa raia wake wote kuondoka mjini Wuhan katika jimbo la Hubei , eneo ambalo virusi vya corona vilianzia.
Chini ya wiki moja baadae , Marekani ilikubali kupokea raia wake ambao walikuwa wanafanya kazi China kurudi kwa hiari.
Siku ya tarehe 30 Januari , shirika la afya duniani(WHO) ilitangaza kuwa na dharura ya kiafya ya dunia kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.
Kufuatia tamko hilo, Marekani ilitoa amri ya raia wote wa Marekani ambao wako chini ya miaka 21 kuondoka China.
Raia yeyote wa Marekani ambaye yuko jimbo la Hubei atapaswa kukaa siku 14 katika karantini kabla ya kurejea Marekani.
Mataifa mengine yanafanya jitihada gani kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo?
Siku ya Jumatatu, Hong Kong ilisema kuwa ilifunga mipaka yake 10 kati ya 13 inayoruhusu watu kuelekea China.
Mataifa mbalimbali yameweka zuio la kukataza watu kusafiri ikiwa ni hatua ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona.
- Marekani, Australia na Singapore: wamekataza wageni wote waliotembelea China hivi karibuni wasiingie nchini mwao.
- New Zealand, Israel : wamekataza raia wageni waliotoka China.
- Japan, South Korea: wamekataza wageni waliotokea jimbo la Hubei.
- Misri, Finland, Indonesia, Uingereza na Italia wamesitisha safari za ndege zao zote kwenda China:
- Mongolia, Urusi : wamefunga sehemu ya mpaka waChina:

China imepokeaje hatua ambazo Marekani imezichukua?
Siku ya Jumatatu, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Hua Chunying alisema kuwa hatua ya Marekani inaweza kueneza hofu badala ya kusaidia.
Alisema kuwa Marekani ndio nchi ya kwanza kuweka katazo la kuzuia watu wanaosafiri kutoka China kuingia nchi mwake na kupendekeza kuondoa wafanyakazi wake wa ubalozi nchini China.
"Kwa taifa lililoendelea kama Marekani, lina uwezo wa kuzuia maambukizi... lakini kuongoza kuweka makatazo wanakuwa ndivyo sivyo na kile ambacho shirika la afya duniani lilishauri," Bi. Hua alisema kwa mujibu wa ripoti ya Reuters.
Zuio la watu kusafiri linasaidia?
Maafisa wa afya duniani wanapinga makatazo ya aina hiyo.
Shirika la afya duniani, WHO lilitoa angalizo kuwa kufunga mipaka kutaweza kufanya maambukizi ya virusi hivyo kuenea zaidi, kama watu wataingia katika mataifa mengine kwa njia ambayo sio rasmi.
"Zuio la watu kusafiri linaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa sababu watu hawataweza kupata taarifa sahihi, madawa yatashindwa kusambazwa na kudumaza uchumi," kiongozi wa shirika la afya duniani, WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema hivyo wiki iliyopita.
Badala yake WHO ilishauri kuwa waanzishe mfumo wa kuwapima watu katika mipaka wanapovuka mpaka mmoja kwenda mwingine.
Siku ya Jumatatu, Dkt. Tedros alirudia kuisifu China kwa jitihada ambazo wamekuwa wakizifanya kukabiliana na virusi vya corona na kusisitiza kuwa nchi zote zinapaswa kushirikiana kukabiliana na changamoto ya ugonjwa huu mpya.
Virusi vya corona ni hatari kiasi gani?
Watu zaidi ya 75,000 wanaweza kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, katika mji wa Wuhan, wataalamu wameeleza.
Ingawa makadirio ya chuo kikuu cha Hong Kong yanasema kuwa inawezekana kuwa idadi ikawa kubwa zaidi ya takwimu zinazotajwa rasmi.
Ripoti zinasema kuwa kuna watu ambao walifariki wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza tu, jarida la afya la Lancet linasema kuwa wagonjwa wengi walikufa bila kufahamika kile kilichowauwa.
Ripoti imebaini kuwa wagonjwa 99 walihudumiwa katika hospitali ya Jinyintan huko Wuhan , 40 kati yao walikuwa na magonjwa ya muda mrefu kama magonjwa ya moyo au presha, wengine 12 walikuwa wana kisukari.














