Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya sodo kuondolewa kodi Rwanda
Hashtag #FreeThePeriod ndiyo mada kuu katika mtandao wa Twitter nchini Rwanda, lengo likiwa ni kusaidia wasichana wanaotoka familia maskini.
Hii ni kampeni iliyoanzishwa na wasichana 10 na wavulana 2 ya kumaliza ukosefu wa sodo(pads) miongoni mwa wasichana wasiojiweza nchini huko.
Mwezi uliopita serikali ya Rwanda ilitangaza "Tumeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa sodo ili kurahisisha upatikanaji wake kwa wanawake na wasichana ambapo pakiti moja inauzwa kwa karibia dola moja ya marekani.
"Hatua hii ni nzuri lakini gharama ya visodo bado iko juu kwa familia nyingi maskini kote nchini Rwanda, na kuhatarisha afya ya wasichana wengi kutoka familia maskini" Saidath Murorunkwere, mwanaharakati wa masuala ya kike nchini Rwanda ameiambia BBC.
Asilimia 35 ya watu nchini humo bado wanaishi chini ya dola mbili kwa siku kulingana na Benki ya Dunia, na sodo kwa wanawake na wasichana siyo jambo la msingi katika baadhi ya kaya.
Mnamo mwezi Septemba, Jeannine Kizima na rafiki zake walianza kampeni ya kutafuta sodo kutoka kwa wafadhili na kuzigawanya bila malipo kwa wasichana kutoka familia maskini ambazo haziwezi kununulia binti taulo la hedhi.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, juhudi zao zimefikia kiwango cha juu huku raia wakiahidi kile walichonacho kupitia mtandao wa Twitter.
Raia wa Rwanda wamekuwa wakiwahimiza rafiki zao kuunga mkono kampeni hiyo.
"Tulikuwa tumefikia shule mbili pekee eneo la kaskazini lakini kwasababu watu wengi wanatoa ahadi zao, nimatumaini yetu kwamba tutafikia idadi kubwa ya wasichana kadiri ya uwezo wetu" Bi Kizima ameiambia BBC.
Kampeni yao hailengi tu kugawanya sodo lakini pia kumaliza imani potovu na ukimya katika masuala ya afya ya uzazi na hedhi miongoni mwa familia na wasichana nchini Rwanda.
"Katika masuala ya afya ya uzazi kama vile hedhi, familia ziko kimya, wasichana wako kimya huku wanaume wengine wakilichukulia kama mwiko kulizungumzia".
"Tunapofikia wasichana hawa, hatugawanyi tu sodo tulivyokusanya, bali pia tunawafundisha na kuwafanya wazungumzie wazi masuala kama hayo mbayo bado ni mwiko" - Kizima amesema.
Bi.Kizima ameongeza kuwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita, wamepokea ahadi zaidi paketi 1000 ya visodo na bado zinaendelea kumiminika.
"Tunafuraha kupita kiasi na matumaini makubwa ya kufikia wasichana wengi zaidi mashuleni ambao familia zao haziwezi kununua pedi" amesema.
Pia unaweza kusoma: