Bilionea Mzimbabwe anayeishi Uingereza amaliza mgomo Zimbabwe

Madaktari Zimbabwe

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Madaktari wakiandamana Zimbabwe

Madaktari nchini Zimbabwe wamekubali kurejea kazini, kwa kuumaliza mgomo ambao umedumu kwa zaidi ya miezi minne. Mgomo huo ni miongoni mwa iliyodumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya nchi hiyo na umeathiri vibaya mno sekta ya afya Zimbabwe.

Madaktari hao wamekubali kurejea kazini baada ya bilionea Mzimbabwe anayeishi Uingereza Strive Masiyiwa kufikia maafikiano na madaktari hao kuwa atamlipa kila mmoja wao marupurupu ya takriban dola mia tatu kwa mwezi na kugharamia usafiri wao wa kwenda kazini kupitia mfuko wa hazina utakaoanzishwa kushughulikia hilo kwa niaba ya Strive Masiyiwa.

Wengi wa madaktari waliokuwa wanagoma hupokea mshahara wa chini ya dola mia moja kwa mwezi. Bilionea huyo atagharamia mahitaji hayo ya madaktari kwa miezi sita. Haijabainika wazi ni kipi kitafuata baada ya kipindi hicho.

Askari wakiwa barabarani (Mwezi Septemba)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Askari wakiwa wamewazuia madaktari

Mgomo huo ulianza mwezi Septemba 2019, na baada ya kushindwa kufikia makubaliano na serikali ya Zimbabwe madaktari zaidi ya 200 walifukuzwa kazi kwa kosa la kufanya mgomo.

Madaktari waliofutwa kazi walikutwa na hatia ya kutokuwepo kazini bila likizo wala sababu muhimu'' kwa siku tano zaidi kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya huduma za afya (HSB)

Madaktari hao wamekuwa wakidai malipo mazuri ya mishahara.

Mgomo huo umesababisha kuzorota kwa huduma katika hospitali kubwa, ambapo huduma za dharura pekee ndizo zimekuwa zikitolewa.

Mwandishi wa BBC, Harare, Shingai Nyoka, amezungumza na msemaji wa Chama cha Madaktari nchini humo Dr. Tawanda Zvakada na kumuuliza hali ilikuwaje wakati anaingia hospitali baada ya karibia miezi mitano bila kutoa huduma.

'' Nilipoingia kwenye wodi ya hospitali kwa mara ya kwanza nilikuwa na hisia mchanganyiko. Nimefurahi kurejea lakini hakukuwa na vifaa vya kutosha kwetu sisi kutoa huduma bora'', amesema Zvakada.

Kulingana na daktari Zvakada, hali ilikuwa ya kuridhisha kwasababu madaktari wamerejea, wodi zimefunguliwa na sehemu za kuona madaktari ambazo zilikuwa zimefungwa, zimefunguliwa tena.

Madaktari wamesema kwamba walitaka suluhu ya kudumu lakini hawakuweza kufikia makubaliano na serikali na kurudi kwao sasa kumetokana na makubaliano na wakfu wa Higherlife Foundation unaoongozwa na Strive Masiyiwa.

''Watu wamepoteza maisha wengine wamepata ulemavu ambao hauwezi kurekebishika'', amesema daktari Zvakada.

Aidha madaktari hao wana matumaini kwamba watafikia makubaliano ya kudumu na serikali na kutoa wito wa kuangaliwa kwa madai yao ambayo bado hayaja badilika.