Yahya Jammeh ameonywa dhidi ya kurejea Gambia

Yahya Jammeh (file photo)

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Yahya Jammeh aliongoza Gambia kwa miaka 22

Gambia imemuonya rais aliyeng'olewa madarakani Yahya Jammeh asijaribu kurejea nyumbani kutoka uhamishoni Equatorial Guinea.

Usalama wa Bwana Jammeh hauna uhakika iwapo atarejea bila ruhusa, msemaji wa serikali ameiambia BBC.

Msemaji wa chama cha Jammeh alisema kwamba anaweza akarejea muda wowote ule.

Nchi Jirani za Gambia zilimlazimisha Jammeh kwenda Equatorial Guinea baada ya kukataa kukubali matokeo ya uchaguzi uliofanyika Disemba 2016.

Alipoingia madarakani baada ya mapinduzi ya mwaka 1994, aliendeleza mfumo wa uchaguzi wa kawaida lakini baadaye akashutumiwa kwa unyanyasaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji ya kiholela mateso na kukamata watu kiholela.

Mrithi wake rais Adama Barrow, aliunda tume ya ukweli, maridhiano ya kusikiliza malalamiko ya umma dhidi yake lakini Jammeh amekataa kutoa ushirikiano.

Yahya Jammeh yuko wapi?

Bwana Jammeh ameonyesha nia ya kurejea nyumbani.

Lakini kwa taarifa tuliyo nayo mpaka sasa, bado yuko Equatorial Guinea, karibia kilomita 3,000 kutoka Gambia.

Kiongozi wa muda wa chama cha Jammeh, Ousman Rambo Jatta, alikataa kusema ni lini hasa kiongozi huyo anatarajiwa kurejea Gambia.

"Yuko njiani... Anaweza kurejea muda wowote tokea sasa," ameambiakipindi cha BBC cha Focus on Africa.

line

Yahya Jammeh ni nani?

  • Alizaliwa Mei 1965
  • Aliingia madarakani baada ya mapinduzi mwaka 1994
  • 2013, aliapa kuendelea kusalia madarakani ''miaka bilioni'' iwapo Mungu atampa Umri
  • Pia aliagiza hukumu ya kifo dhidi ya wahalifu na wapinzani wake wa kisiasa
  • Mwaka 2007, aliahidi kwamba anaweza kutibu ukimwi na ugumba kwa kutumia dawa za mitishamba.
  • 2008, alionya kwamba wapenzi wa jinsia moja watahukumiwa kifo
  • Pia alikanusha kwamba majajusi wake wa usalama walimuua Deyda Hydara, 2004
Yahya Jammeh

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Yahya Jammeh

Jatta alizungumza Jumamosi iliyopita baada ya mazungumzo yake ya bwana Jammeh kuvuja.

Katika mazungumzo hayo, kiongozi aliyeng'olewa madarakani alisikika akiunga mkono maandamano ya wafuasi wake yaliyopangwa kufanyika Januari 16.

"Sitaki mtu afanye ghasia wala kugusa chochote au kuharibu kitu," Bwana Jammeh amesema.

Je Jammeh anahaki ya kurejea?

Jammeh ana haki ya kurejea nyumbani.

Hilo liliwekwa wazi katika makubaliano ya Januari 2017, chini ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na mamlaka za kikanda kama vile, Ecowas, ambayo yalimshuhudia akikubali na ktia saini kwamba anakwenda uhamishoni chini ya shinikizo la vikosi vya Ecowas ambavyo tayari vilikuwa vimeingia Gambia.

Hatua hiyo ilimaanisha kwamba Jammeh angeondoka kwa muda na alikuwa na uhuru wa kurejea Gambia muda wowote ambao angependa kulingana na sheria ya kimataifa ya haki ya kibinadamu ya haki yake kama raia wa Gambia na pia kama aliyekuwa rais wa nchi hiyo.

Hata hivyo, msemaji wa serikali Ebrima Sankareh alisema hana ufahamu wa nyaraka zinazozungumziwa na kuongeza kuwa Rais Barrow hakutia saini makubaliano yoyote ya aina hiyo.

Iwapo atarejea bila ya kupewa ruhusa, Serikali ya Gambia haiwezi kumhakikishia usalama wake," Bwana Sankareh ameiambia BBC.

Kulingana na mtazamo wake, Jammeh ametamani nyumbani na kuongeza kuwa Equatorial Guinea na Gambia zina uhusiano wa mbali kiasi kwa misingi ya utamaduni.

Waandamanaji wa Gambia

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Raia wa Gambia wamekuwa wakitaka uchunguzi ufanyike kuhusu watu waliopotea chi ni ya utawala wa Jammeh

Nini Kinafuata?

Bwana Jatta, kiongozi wa muda wa chama cha Jammeh cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction party, amesema kwamba Jammeh anastahili kuruhusiwa kuishi Gambia kwa Amani badala ya kufunguliwa mashtaka kwa madai ya unyanyasaji wa haki za binadadamu.

Pia alionya kwamba jaribio lolote la kumkamata bwana Jammeh kunaweza kusababisha umwagikaji wa damu.

"Hakuna atakayejaribu kumkamata," amesema.

Bwana Barrow anatarajiwa kuwania tena urais mwaka ujao licha ya makubaliano ya awali ya kujiuzulu baada ya kipindi cha mpito cha miaka mitatu.