Shambulio la kigaidi: 'Abiria wangu ni sawa na kaka na dada zangu'

"Mimi sio shujaa, " anasema Raymond Juma kwa sauti ya upole.

Dereva huyu alizungumzia jinsi alivyowaokoa abiria 47 katika shambulio la wapiganaji Mashariki mwa kenya.

" Abiria wangu ni kama mama zangu, ndugu na dada zangu. Nilifanya tu kile mtu yeyote mwingine angeweza kukifanya angekuwa kwenye nafasi yangu, yaani kuyaokoa maisha yake na awapendao" aliiambia BBC.

Bwana Juma alikuwa akiendesha basi la kampuni ya Mombasa Raha iliyoshambuliwa na watu waliojihami vikali tarehe 2 Januari katika barabara kati ya miji ya pwani ya Mombasa na Lamu.

Alisema watu hao walikuwa wamevalia sare zilizofanana na za jeshi, walitokea ghafla nyuma ya daladala iliyokuwa imeegeshwa kando ya barabara na kuanza kufyatua risasi hewani, kabla ya kumuamuru kusimamisha basi.

" Ilikuwa ni kama sinema ya kuogofya, " alisema. Lakini aliendelea kuliendesha basi kwa kasi

" Nilipokataa kusimama, walilifyatulia basi risasi. Nilijuwa iwapo ningesimama, hiyo ingekuwa mwisho wa Maisha yangu na abiria wangu wote.

" Watu walikuwa wakipiga mayowe na kulia huku milio ya risasi ikiendelea. Nilipoangalia nyuma kupitia kioo, niliwaona wengine wakijirusha katika sakafu na kujificha"

Risasi hizo ziligonga upande wa basi lake na kutoboa tairi zote za mbele, na kulilazimisha kusimama kama mita 100 ( futi 330) kutoka eneo hilo.

" Nilipolisimamisha basi, watu walianza kutorokea kupitia madirisha ya basi wakijaribu kuyaokoa Maisha yao. Watu walikuwa wakikimbia kila mahali, ikiwemo katika msitu."

Dereva huyo mwenye umri wa miaka 46 ambaye ni baba wa watoto wanne, anasema aliendelea kukimbia kwa saa moja hivi kabla ya kusaidiwa na dereva wa basi lingine ambaye alimpa lifti.

" Sijwahi kupata mshutuko mkubwa maishani kama wakati huo," alisema sauti yake bado ikitetemeka

" Ni kwa neema za mwenyezi Mungu tu, ni bahati basi halikubingiria na sote tuu hai sasa"

Lakini dereva wa basi la pili, Aboubakar Hemed, hakuwa na bahati sawa na hiyo.

'Utingo(conductor) aliuliwa'

Bila kufahamu kilichokuwa kikiendelea mbele, alitii agizo la wapiganaji hao walipomuashira kusimama, akidhani ni maafisa wa polisi

Abiria wote 41 waliamurishwa kushuka katika basi.

" Waliwaamuru abiria kukariri Shahada za Kiislamu. Wale ambao hawakuweza walipigwa risasi papo hapo, " Bw Hemedi aliiambia BBC

Anasema kwamba alikuwa na hofu nyingi kiasi cha kupata kigugumizi alipokariri Shahada yeye mwenyewe.

Wanaume watatu katika basi hilo waliouwawa na wanamgambo hao wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la Al Shabab kutoka Somalia. Wengine kadhaa walijeruhiwa katika shambulio hilo na wanendelea kupokea matibabu hospitalini.

" Unawezaje kusahau jambo kama hili? Bw Hemed anauliza

" Kondakta wangu aliuwawa na wanamgambo hawa. Inafedhehesha sana hata siwezi kujielezea"

Anasema watu walikuwa wakitetemeka na kulia walipokuwa wakishuka kwenye basi huku wapiganaji hao wakiwasubiri chini.

Wengine walitoka na mara moja wakatoroka kuyaokoa Maisha yao huku wakifyatuliwa risasi, lakini kwa bahati nzuri hakuna aliyeguswa na risasi walipokuwa wakitoroka.

" Kama dereva mara kwa mara utasikia habari kama hizi za mashambulio ya Al Shabab katika barabara hii, lakini hakuna kinachoweza kukutayarisha kwa jambo kama hili, " anasema Hemed ambaye amekuwa akifanya kazi katika barabara hii kwa miaka mitano sasa.

Al Shabab haijasema ilihusika na shambulio hilo la basi wiki jana, lakini kundi hilo limetekeleza mashambulio sawa na hayo katika barabara hii katika miaka ya hivi karibuni.

Kenya ina wanajeshi nchini Somalia, chini ya vikosi vya Muungano wa Afrika AU vinavyotoa usaidizi kwa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa katika vita dhidi ya Al Shabab.

Kundi hili la wanamgambo limepoteza baadhi ya maeneo iliyokuwa ikishikilia lakini imeendelea kutekeleza mashambulio upande mwingine wa mpaka, ikiwemo shambulio katika kambi ya pamoja ya kijeshi ya Kenya na Marekani mnamo January 5 ambapo raia watatu wa Marekani walifariki.

Kwa jumla, mamia ya raia wameuwawa au kujeruhiwa katika mashambulio hayo.

Tangu mwaka wa 2015, katika juhudi za kukabiliana na Al Shabab, maafisa wa usalama wamekuwa wakifanya operesheni katika msitu wa Boni, unaoaminika kuwa maficho na eneo la kufanya mazoezi kwa wapiganaji wa Al Shabab.

Visa hivyo vimeathiri pakubwa eneo hilo.