Mzozo wa mpakani kati ya Rwanda na Uganda wazidi kufukuta

Uhusiano baina ya Rwanda na Uganda unaendelea kuwa mbaya huku upande wa Rwanda katika maeneo ya mpakani na Uganda mikakati ya kuzuiya raia wa Rwanda wanaotaka kuingia Uganda ukiimarishwa.

Wananchi wa Rwanda kwenye mpaka wa Gatuna wanasema kwamba mikakati hiyo ni pamoja na kuwapiga risasi wanaojaribu kuvuka na kujihusisha na biashara haramu.

''Angalia huu mfereji wa maji hapa hapa.....ukivuka hivi unaingia Uganda. angalia yule mtu anayepanda akija hapa yuko upande wa Rwanda,soko la kimataifa lilikuwa pale....'' anasema mmoja wa waraia wachache wanaokubali japo kisiri kuzungumza na waandishi wa habari karibu na mpaka wa Gatuna.

Sehumu mtu huyo anamuonesha mwandishi wa BBC Yves Bucyana na 'Mukensiyona' jina la soko lililopo kwenye mpaka ,upande wa Uganda, zamani lilikuwa linawajumuisha wananchi wa pande mbili.

Lakini sasa hakuna raia wa Rwanda anayeweza kuthubutu kukanyaga kwenye soko hilo.

''Natokea karibu tu ya hapa sitoki Uganda kwani siku hizi tulikatazwa kwenda huko'' anasema Mama aliyekutana na mwandishi wetu barabarani akiwa begi tupu la kubebea chakula.

Aliongeza kuwa hawezi kuthubutu kukanyaga huko tena kwasababu ''niliingiwa na uoga baada ya kwenda huko niliporudi nikanyang'anywa unga wangu na kutupwa kizuizini kwa siku mbili''

BBC ilifika eneo lenye njia haramu zinazotumiwa na wanaotaka kuvuka kuingia Uganda na kugundua kuwa kwa sasa ni hatari.

''Wanaothubutu kwenda huko wanapigwa risasi. nawafahamu watu kama 4 hivi waliopigwa risasi hivi karibuni wakitaka kuvuka na kwenda Unganda'' alisema mmoja wa wakaazi katika eneo la mpakani.

Anasisis tiza kuwa ni wazi kwamba watu hao hawapigwi risasi na raia kwasababu raia hawana silaha.

''Hapa Rubaya nawafahamu watu wawili waliopigwa risasi''

Hapo nyuma polisi ya Rwanda ilitangaza kwamba mtu yeyote atakayekiuka sheria za mpakani hatavumiliwa.

Mwezi uliopita polisi ilipiga risasi na kuwauwa watu 2 raia wa Uganda karibu na mpaka wa Kagitumba ambao waliokuwa wameingia Rwanda.Polisi ilisema kwamba waliingiza biashara haramu na kwa kutumia mabavu dhidi ya polisi.Msemaji wa polisi John Bosco Kabera akaonya kwamba serikali haitavumilia yeyote atakayekiuka sheria za mpakani:

Ni dhahiri kwamba mikakati ya kuzuia wanaotaka kwenda Uganda imeimarishwa sana katika maeneo haya ya karibu na mpaka wa Uganda.

''(Mtu anayezungumzia kwa simu) Hello Mzee.......sawa sawa hamna tatizo....achana naye tutamshika.......''

Ninayezungumzia ni mtu ambaye alituponyoka akavuka na kwenda Uganda lakini naelezwa kwamba alirudi hapa kwa kujificha juzi usiku'' anasema mwandishi wa BBC Yves Bucyana.

Kumekuwa na taarifa kwamba Rwanda imerundika majeshi na zana za kivita hapa karibu na mpaka lakini BBC haijathibitisha taarifa hizo,

''Mimi naishi hapa nayajua maeneo yote ya hapa ,sijaona askari katika maeneo haya ya karibu na mpaka.kilichopo sisi wenyewe raia tunafanya doria pamoja na askari wastaafu ambao pia wanatembea bila silaha.lengo letu ni kuzuiya wanaotaka kuvuka na pia wafanyabiashara haramu''

Mkutano wa pili uliopangwa kukutanisha wajumbe wa nchi mbili mjini Kampala chini ya upatanishi wa Angola uliahirishwa na haijafahamika utafanyika lini ili kusuluhisha mgogoro huu.