Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Surua Samoa : Familia ambazo hazijapewa chanjo zaombwa kutundika bendera nyekundu mlangoni
Familia ambazo hazijapewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua nchini Samoa zimeombwa kutundika bendera nyekundu nje ya nyumba zao ili kusaidia kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa surua au ukambi.
Bendera hiyo itawasaidia maafisa wa afya kuenda nyumba moja hadi nyingine kuwapa chanjo wananchi.
Serikali inasema zaidi ya watu 4,000 kati ya 200,000 nchini humo wameathiriwa na ugonjwa wa surua
Watu sita wamefariki kufikia sasa, wengi wao watoto walio na miaka chini ya mitano.
Samoa ilitangaza hali ya dharura mwezi Novemba ili kukabiliana na mlipuko wa magonjwa na sasa chanjo ni lazima kwa watu wote.
Shule zote zimefungwa na watoto walio na umri wa chini ya miaka 17 wamepigwa marufuku kuenda sehemu zilizo na mkusanyiko wa watu.
Maafisa nchini Samoa wanasema viwango vya chanjo kwa sasa vimefikia 55%. Waziri mkuu wa Tuilaepa Sailele Malielegaoi ameapa kuongeza idadi hiyo hadi zaidi ya 90%.
"Watoto wetu hawatawahi kuwa na kinga kamili dhidi ya magonjwa siku zijazo hadi pale tutakapofikia 100% ya chanjo,"alisema wakati alipowatembelea waliolazwa hospitali siku ya Jumatano.
Shirika la watoto la Umoja wa mataifa Unicef limetuma chanjo nchini humo, nayo New Zealand imetuma dawa, wauguzi na vifaa vya matibabu - japo inaendelea kupambana na ugonjwa huo.
Chanjo huchukua kati ya siku 10 hadi wiki mbili kuanza kufanya kazi. Baathi ya watu wameripotiwa kusambaza dawa ghushi kutibu ugonjwa huo.
Mfanyibiashara mmoja aliliambia shirika la utangazaji la Australia ABC kuwa ''maji yake ya Kangen'' ambayo kwa uhalisia ni maji ya bomba - yanaweza kumkinga na dalili za surua.
Tonga na Fiji pia zimetangaza hali ya dharura ili kukabiliana na mlipuko wa surua mwezi uliopita.
Hata hivyo mataifa yote mawili yamefikia viwango vya juu vya chanjo- zaidi ya 90% katika nchi zote mbili - na kufikia sasa hayajatangaza visa vyovyote vya kifo.
Timu ya raga ya wanawake kutoka Tonga iliwekwa chini ya uangalizi maalum siku ya Alhamisi baada ya mlipuko wa surua kutangazwa nchini humo.
Je surua ni nini?
Surua ni virusi vinavyosababisha mtoto kuwa na mafua , kuchimua mara kwa mara na kuwa na joto mwilini.
Siku chache baadaye mgonjwa anapata vipele mwili mzima ambavyo vinaanza usoni na kusambaa mwilini.
Wengi hupona , lakini surua inaweza kusababisha ulemavu wa muda mrefu. Inaweza kusababisha kifo hususan iwapo utasababisha homa ya mapafu ama uvimbe katika ubongo.
Inakadiriwa kwamba jumla ya watu 110,000 duniani hufariki kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.
Viwango vya maambukizi ya surua vimeongezeka duniani.
Shirika la Afya Duniani (WHO) mwezi Aprili mwaka huu lilitangaza kuwa idadi ya visa vya ugonjwa huo vimeongezeka mara nne zaidi duniani katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu ilkilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka 2018.
Dalili za surua
- Kuhisi baridi na kupiga chafya
- Homa kali,uchovu,kukosa hamu ya kula na misuli kuuma
- Macho kuwa na rangi nyekundu na majimaji kama unataka kulia
- Kuwa na rangi ya kijivu mdomoni
- Kuwa na vipele vyenye rangi nyekundu ambavyo vinaweza kusambaa kutoka kwenye kichwa,shingoni mpaka kwenye mwili wote.
Karibia watu 5,000 wameaga dunia kwasababu ya ugonjwa wa surua au ukambi huko Jamuhuri ya kidemokrasi na wengine takriban robo milioni wameathirika.
Shirika la Afya Dunia-WHO limesema mlipuko huo umesambaa kwa haraka sana na ndiyo mkubwa zaidi kuwahi kutokea.