Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Familia, wafanyakazi wenza waeleza machungu ya miaka miwili bila Azory Gwanda
Tarehe 21, Novemba 2017, yaani siku kama ya leo miaka miwili iliyopita, mwanahabari Azory Gwanda kutoka nchini Tanzania, alitoweka kwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Mtu wa karibu wa mwisho kumuona alikuwa mke wake Ana Pinoni. Bw Gwanda alikwenda shambani na kumkabidhi ufunguo wa nyumba Bi Pinoni na kumueleza kuwa anaenda kazini.
Bw Gwanda alikuwa ameongozana na watu wanne waliokuwa kwenye gari ambayo Bi Pinoni anaitaja kuwa nia aina ya Toyota Land Cruiser yenye rangi nyeupe.
Toka hapo, Azory Gwanda hajaonekana tena mpaka hii leo.
Baadhi ya wadadisi wamedai kuwa watu waliomchukua mwanahabari huyo ni maafisa usalama, jambo ambalo serikali ya Tanzania imelipinga
Familia ya Azory inasemaje?
Hivi karibuni mke wa Bi Penoni aliongea kwa kirefu na BBC kuhusu hatima ya mume wake na kueleza kwa kiasi gani amekuwa akibeba mzigo mgumu wa majukumu ya malezi akiwa peke yake.
"Ninajaribu kuongea lakini sijui hata niongee nini. Sijui la kusema kwa sababu wajibu nilionao kwa sasa ni mzito sana kiasi kwamba huwa kila mara nafikiria mume wangu na msaada ambao angekuwa ananipa. Lakini ninaendelea kuhangaika na maisha kwani sina chaguo.
"Mmoja wa watoto wangu yuko katika chuo cha sheria kwa sasa na ndiye aliyeathirika zaidi. Kila wakati anapowaona watu wengi wakinitembelea, anafikiri kuwa ninaficha ukweli kwamba baba yake amekufa. Ninajaribu kumliwaza lakini inaniumiza sana," Bi Penoni ameileza BBC.
Gazeti la Mwananchi hii leo limemnukuu mama wa mwanahabari huyo Bi Eva Mpulumba ambaye amesema: "Tunaishi maisha ya shida na ufukara mkubwa tangu Azory alipotoweka. Familia haina msaada na hatujui kama yupo hai au alikufa, tunaomba rais (Magufuli) atusaidie mtoto wetu apatikane."
Wafanyakazi wenzake Azory wanamuelezaje?
Mpaka anatoweka Bw Gwanda alikuwa anaripotia gazeti la Mwananchi ambao kwa miaka miwili iliyopita wamekuwa wakiendesha kampeni mbalimbali za kutaka kurejeshwa kwa mwanahabari huyo.
Hii leo, wafanyakazi mbalimbali wa Mwananchi wamemuelezea mwenzao wakiongozwa na mhariri mkuu wa gazeti hilo Bakari Machumu.
"Mwandishi aliyejitoa, jasiri na mwenye maono, Azory ameganda katika akili zetu kama mfanyakazi mwenzetu, rafiki ambaye aliipenda kwa dhati kazi yake. Tunatarajia siku moja tutaungangana naye katika kazi hii ya uadilifu ya kuitumikia jamii katika njia bora aliyoifahamu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuifariji na kuisimamia familia yake," ameandika Machumu katika tangazo lililotolewa na gazeti hilo.
Mwandishi mwingine aitwaye Benard James ameeleza kuwa aliwasiliana na Azory siku moja kabla hajatoweka. "Namlilia Azory kila siku...Alitamani sana watu wa Rufiji wapate amani lakini waliomteka hawajali hili. Naomba Mungu ategue kitendawili cha wapi alipo mpendwa wetu.
Unaweza pia kutazama mazungumzo yake na BBC
Je, Azory yupo wapi?
Hili ni swali tata ambalo limekosa jibu kwa miaka miwili sasa. Imekuwa pia ni kampeni ya mashirika kadhaa ya kutetea haki za wanahabari na haki za binaadamu.
Mwezi Septemba mwaka huu, Azory Gwanda alitajwa kuwa miongoni mwa visa kumi vya dharura vya tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari duniani.
Orodha inayochapishwa kila mwezi na One Free Press Coalition, iliidhinishwa na muungano wa mashirika kadhaa likiwemo TIME kwa lengo la kuwalinda waandishi habari wanaoshambuliwa kutokana na kazi zao.
Mwezi Juni ilizuka suitafahamu kubwa juu ya alipo mwanahabari huyo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi kusema katika mahojiano na BBC jijini London kuwa "amepotea na kufariki," hata hivyo waziri huyo baadae alikanusha vikali kuwa amethibitisha kuwa amefariki na kudai kuwa kauli yake ilitafsiriwa vibaya.
Bw Gwanda alikuwa anaishi na kuripoti kutoka mji mdogo uitwao Kibiti, ambao upo kilomita kama 130 hivi kusini mwa Dar es Salaam.
Alikuwa ni mmoja wa waaandishi wa kwanza kabisa kuripoti kwa kina juu ya mfululizo wa mauwaji yaliyokuwa yakitekelezwa na watu wasiojulikana yaliyowalenga polisi na viongozi wa mji huo.