Jinsi unyanyasaji wa kingono vyuoni unavyoathiri wanafunzi wa kike Kenya

Unyanyasaji wa kingono ni tatizo kubwa la kiafya na hata la kibinadamu linalomuathiri mtu kwa muda mrefu au mfupi hayo ni kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) .

Kulingana na utafiti uliofanywa nchini Kenya na Shirika la ActionAid pamoja na viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini Kenya asilimia 49 ya wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu hunyanyaswa kijinsia huku asilimia 24 ya wanafunzi wa kiume pia hunyanyaswa na wafanyikazi katika vyuo hivyo.

Viongozi wa wanafunzi wa vyuo hivyo wameanzisha kampeni ya kusitisha unyanyasaji wa kingono kwa kutumia #CampusMeToo, ambayo inawarai wanafunzi wanaopitia unyanyasaji wa kingono kuripoti visa hivyo bila uongo huku wakiwa na matumaini ya kupata saini elfu 50 ili kuisisitizia serikali ya Kenya kuwekeza mbinu zilizowazi za kukabiliana na visa hivyo.

Hii ni baada ya kipindi cha BBC Africa Eye kupeperusha taarifa ya jinsi wanafunzi wa Ghana na Lagos wanavyonyanyaswa kingono. Kulingana na takwimu za utafiti uliofanywa kwa miezi 4 miongoni mwa zaidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu 1000 ilionyesha kati ya wasichana wawili mmoja hunyanyaswa na kati ya wanaume wanne mmoja hupitia unyanyasaji.

Mwanafunzi mmoja kwa jina Mary ambalo si jina lake rasmi ameiambia BBC Kwamba alipitia unyanyasaji wa kingono pindi tu alipojiunga na chuo kikuu kimoja nchini Kenya.

Mary alikuwa na miaka 17 alipoanza masomo yake na alikuwa amechelewa kujiunga na zilikuwa zimesalia wiki mbili kabla ya mitihani ya kwanza kuanza. Mary alijaribu kuongea na wahadhiri tofauti ili aweze kuwafikia wenzake na hapo ndipo unyanyasaji ulipoanza bila yeye mwenyewe kugundua kwamba mhadhiri wake anamnyanyasa kigono.

Baada ya muda Mary alijikuta akiwa na mahusiano ya kimapenzi na muhadhiri wake.

Kulingana naye Mary anasema alikuwa na uwezo wa kukataa hilo lakini muhadhiri wake alijulikana kuwa mkali na hakutaka kuyahatarisha masomo yake na hakufahamu chochote wakati ule kuhusiana na maisha ya vyuo vikuu. Anadai hakuna aliyemuarifu kuhusiana na maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu.

''Nilipoanza masomo yangu muhadhiri huyo alianza kunizoea na siku mmoja baada ya darasa lake aliniambia nimtafute ili aweze kunipatia vitabu vya kozi ambayo niliyokuwa nikisoma kwa wakati ule.''

Mary alifika katika ofisi yake wakabadilishana nambari za simu.

'Nilipokuwa katika ofisi yake alifunga mlango na kuteremsha pazia na alinibembeleza na kunionyesha nia ya kushiriki mapenzi nami. Na nilihisi nililazimishwa hayo yote ya kumfurahisha kimapenzi.

''Nilipoondoka katika ofisi ile nilijihisi mjinga na nisiye na maana yoyote kwani hakunichukulia kwa njia nzuri'' Mary amesema.

Mary ameongeza kwamba hakuwa na uwezo wa kukataa lolote kutoka kwa muhadhiri wake.

''Nilikuwa na uoga mwingi na iwapo ningetamka lolote basi ingekuwa mwanzo wangu wa kuanguka mitihani yangu. Na kile nilichokithamini sana ilikuwa ni masomo yangu.''

Mary amesema muhadhiri huyo alizidi kumpigia simu na kumtumia arafa kwa mara akimtaka waende kupata kinywaji pamoja lakini wakati huo hakuweza kukutana na muhadhiri huyo na wiki iliyofuata muhadhiri huyo akapanga safari nje ya jiji la Nairobi na wakakutana kama ada yao.

Hali hiyo ilimsababishia Mary kujiona bure na hata akaanza kupatwa na msongo wa mawazo uliosababisha kujaribu kujitoa uhai mara kadhaa kwani hakujua la kufanya.

Baada ya yote kugonga mwamba, aliamua kubadili kozi yake katika chuo hicho hicho na akafanikiwa kwani aliogopa masomo yake kuathirika zaidi kwa kunyimwa alama.

''Nilizungumza na rafiki yangu mmoja akaniambia lazima nitafute mbinu yangu binafsi ya kujiokoa. Sikumwambia mama yangu kwa wakati ule.''

Mara ya pili kwa Mary, kunyanyaswa kigono ilikuwa alipokuwa na miaka 20 ambapo kiongozi mkuu mmoja katika chuo hicho alichokuwa akiendelea kuyapokea masomo yake alimtaka kushiriki ngono naye na alikuwa akiishi katika nyumba za wafanyakazi wa chuo hicho.

Mkuu huyo alikuwa akimlazimisha kwa kupitia simu na arafa amtembelee katika nyumba yake ilikuwa katika eneo la chuo hicho.

Na kwa mara nyingine alipatwa na msukumo wa kukutana na mkuu huyo lakini aliepuka kwa mara ya kwanza kwa kukata mawasiliano na mkuu huyo kwa kubadilisha laini yake.

''Bado nilizidi kupitia unyanysaji wa kingono.Nilitaka kusahihishiwa kazi zangu za chuo na wakati nilipotaka usaidizi kwa anayehusika aliniambia iwapo tungekutana kwani amekuwa akinitamani kwa muda mrefu. Na niliposema ninataka kutoka alipatwa na hasira.'' amesema Mary

Kwa Mary hayo hayakuishia hapo mkuu huyo alizidi kutuma arafa lakini akijikakamua na kusema hataweza kutimiza lengo lake.

Kulingana na mbunge anayewawakilisha vijana katika bunge la Afrika Mashariki Jilly Kaunda yeye pia alijikuta katika lindi hilo lakini aliweza kumchenga muhadhiri wake hadi akasahau matakwa yake. ''Nilikuwa namdanganya aliponiambia tukutane nje ya shule nilikuwa namwambia tukutane katika maktaba anakataa.''

Mwenyekiti wa vyuo vikuu binafsi nchini Kenya, Victor Kiprono amesema vijana hunyanyaswa kijinsia kama vile kwa wanafunzi wa kike.

Unyanyasaji wa kingono hutekelezwa kwa njia gani?

  • Kwa vitendo; Kumgusa, kumbusu, kumkubatia na hata kujamiiana bila hiari
  • Maneno; matamko ya matanio , kumuuliza mtu kuhusiana na maisha yake ya ngono, kumlazimisha mtu kukutana naye ikiwa na lengo la kumuonyesha mapenzi.
  • Mawasiliano ya kutumia ishara; kumuangalia mtu kwa muda mrefu , simu/arafa za mara kwa mara zilizo na mada ya ngono.

Viongozi wa wanafunzi wanataka katika kampeni yao kuhakikisha kila mwanafunzi anayejiunga na vyuo vikuu kuelimishwa kuhusiana na visa vya unyanyasaji wa kingono. Mafunzo kwa kila anayehudumiwa katika vyuo hivyo kila mwaka, sheria za unyanyasaji wa kingono kuimarishwa na kutekelezwa.