'Nilitoa tattoo ili niimarishe uhusiano wangu wa kimapenzi'

Gucci
Maelezo ya picha, Gucci

Uchoraji wa chale mwilini au tattoo unazidi kupata umaarufu miongoni mwa vijana na hata wanawake. Wengi huchorwa tattoo kwa ajili ya urembo.

Kulingana na utafiti wa Global Tattoo unaonyesha asilimia 38 wa watu ulimwenguni mmoja ana tattoo moja.

Lakini si wote wanaofurahia uamuzi wao na baada ya kipindi fulani baadhi hutaka kuzifuta.

Gucci, kijana mwenye umri wa miaka, 27, anayeishi jijini Dar es Salaam alichorwa tattoo alipokuwa na umri wa miaka 19 na wakati huo alikuwa ameanza maisha yake ya mahusiano.

Katika safari hiyo Gucci alikutana na msichana kwa jina Rehema, na kama njia ya kumfurahisha na kumuonyesha upendo aliamua kuchora tatooo iliyokuwa na jina la mpenzi wake Rehema.

Aliamua kukoleza na kuirembesha zaidi kwa kuongeza nyota tano ndogo na moja kubwa iliyokuwa imeongezwa rangi nyekundu katika mkono wake wa kulia ili kumuonyesha jinsi anavyompenda.

Lakini baada ya muda uhusiano huo haukudumu na Gucci akaamua kuendelea na maisha yake kivyake.

Gucci akitolewa tattoo na mashine ya Laser
Maelezo ya picha, Gucci akitolewa tattoo na mashine ya Laser

Baada ya miaka kadhaa alimpata mchumba mwingine na tattoo hiyo ikawa kizingiti katika uhusiano wao. Hapo ndipo safari yake ya kutafuta usaidizi mitandaoni ikaanza na akagungudua sehemu ambayo ataweza kupata usaidizi.

''Niliandika jina Rehema kwani ilikuwa kipindi cha ujana na pia nilikuwa napitia vitu vingi na sasa hivi nakua na mipango pia inabadilika ndio maana nimeamua bora nitoe,''Gucci amesema.

Mwanahabari wa BBC Paula Odek, alikutana na Gucci na wakaandamana hadi katika kliniki moja cha uchoraji na utoaji wa Tattoo jijini Dar es Salaam ya Nira.

Lakini Gucci alionekana kuwa na matarajio makubwa kwamba ugomvi kuhusiana na tattoo hiyo utaisha.

"Kwa kweli najisikia vizuri kwa sababu ni kitu ambacho kwanza sikuwa na ndoto ya kwamba nitakuja kuweza kuitoa," Gucci anasema hayo kabla ya kuingia katika kliniki hiyo ya utoaji tattoo.

Gucci hakuwa na uhakika kwamba tattoo hutoka.

Gucci akiwa anatolewa tattoo
Maelezo ya picha, Gucci akiwa anatolewa tattoo

''Sina uhakika kwamba tattoo hiyo itatoka kwa sababu hadi niione na nishuhudie itokee kwangu, ndipo nitakapoamini.''

Katika kliniki hiyo Gucci alihudumiwa kwa umakini na swali kuu aliloulizwa na mtaalam Munira, ni iwapo yuko tayari kutolewa kwa kutumia mfumo wa laser, na iwapo huwa na matatizo yoyote ya kiafya.

Kulingana na mtaalamu Munira, iwapo mtu ana mzio wa aina yoyote au mtu anatumia vidonge vya uzio kwa takriban miezi sita huwa hawaruhusiwi kupata matibabu ya laser.

Munira amesema kuwa mtu mwenye kisukari au virusi vya HIV pia hastahili kutolewa tattoo kwa mfumo huo wa laser.

Tattoo hutolewa kwa mfumo wa laser ambao hutumia miale ya moto na kwa Gucci kutolewa tattoo hiyo ilibidi mtaalam Munira atumie laser mbili tofauti kwani tattoo yake ilikuwa imechorwa na wino mweusi na mwekundu na tattoo zenye rangi ya bluu, njano, kijani na nyekundi huhitaji laser tofauti na yenye miale yenye moto mwingi zaidi kuliko tattoo iliyochorwa na wino mweusi.

Gucci alilazwa katika kitanda katika chumba maalum kilichojaa baridi kwani mashine hiyo haihitaji joto hata kidogo.

Na kila mtu katika chumba hicho lazima avalie miwani maalum kwani mwanga huo una uwezo wa kumpofusha mtu papo hapo endapo utaingia machoni.

Mashine ya Laser
Maelezo ya picha, Mashine ya Laser

Mtaalam Munira anaanza kwa kujaribu mashine yake kwa kutumia sehemu ya boksi maalum kuona iwapo mashine hiyo iko sawa na moja kwa moja anavalia glavu zake na kuanza utaratibu huo.

Mfumo huo wa Laser huvunja vunja wino kwa vipande vidogo na baada ya muda hufanya wino huo kuanza kupotea.

Mtaalam Munira anatumia mashine hiyo inayotoa matone madogo madogo na miale ya rangi ya kijani na ngozi ya Gucci inaanza kuvimba.

Utolewaji wa tattoo kwa kweli si jambo rahisi. Anayetolewa anahitaji kuhimili maumivu lakini Gucci amesema uchungu huo sio mbaya sana kama alivyotarajia.

Mtaalam Munira
Maelezo ya picha, Mtaalam Munira

Baada ya dakika kumi hivi tattoo hiyo ilitolewa katika hatua ya kwanza na sehemu iliyokuwa na jina Rehema ikawa imevimba na kuwa nyeupe lakini mtaalamu Munira alimuhakikishia kwamba weupe huo utapotea baada ya wiki moja. Utoaji wa tattoo hutolewa kwa hatua tofauti kulingana na jinsi tattoo hiyo ilivyochorwa. Na mtu akitolewa tattoo mara ya kwanza haitoki kabisa bali wino hupungua tu.

Furaha ya Gucci ilidhihirika baada ya hatua hiyo ya kwanza ambayo ni hatua aliyoitamani kuitekeleza kwa muda mrefu ili uhusiano wake na mpenzi wake wa sasa uwe shwari.

Gucci alimpigia mpenzi wake simu wakati ule ule na kumuhakikishia kwa kumtumia picha kwa mtandao wa WhatsApp kwamba amefuta jina hilo na akamuahidi kuchora jina lake katika mkono wake wa kushoto.