Utafiti: Dawa za presha 'hufanya kazi vizuri ikimezwa usiku'

Chanzo cha picha, Getty Images
Kupata manufaa ya matibabu ya shinikizo la damu, meza dawa ya muda mfupi kabla ya kulala, watafiti wanasema.
Huu ni ushauri ambao unaweza kuokoa maisha ya watu wengi, unasema utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Ulaya la masuala ya moyo.
Dawa hizo huwalinda wagonjwa dhidi ya mshtuko wa moyo na kiharusi zikimezwa kabla ya kulala badala ya asubuhi, utafiti huo mkubwa unapendekeza.
Wataalamu wanaamini miili yetu inaendeshwa na majira ya kimaumbile ya saa 24 ambayo inaathiri jinsi tunavyopokea tiba.
Kusawazisha matumizi ya dawa na maumbile ya mwili
Kuna ushahidi mkubwa unaoashiria kwamba dawa tofauti, zikiwemo za kutibu maradhi ya moyo, huenda ikafanya kazi vizuri ikimezwa kwa wakati maalum ya siku.
Jaribio hili la hivi punde kufikia sasa linaangazia zaidi dawa za kutibu shinikizo la damu, ambazo zilijaribiwa kwa watu 19,000 ambao wanatumia tiba hiyo.
Katika utafiti huo:
- Wagonjwa waliwekwa katika makundi mawili -kundi la kwanza lilimeza dawa asubuhi na kundi la pili lilimeza dawa hizo wakati wa kulala
- Watafiti waliwachunguza wagonjwa hao kwa miaka mitano au zaidi kubaini hali yao ilikuwaje.
- Wagonjwa waliomeza dawa nyakati za usiku walikuwa katika hatari ya kufariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo, kiharusi au moyo acha kufanya kazi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Shinikizo la damu huwa chini nyakati za usiku,watu wanapolala.
Na hata kama halishuki hubakia wastani, hali inayomweka mtu katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo na kiharusi, wataalamu wanasema.
Mtafiti mkuu Prof Ramon Hermida, kutoka chuo Kikuu cha Vigo, anasema madaktari wanatafakari hatua ya kuwapendekezea wagonjwa tiba hiyo: "Bila malipo. Huenda ikaokoa maisha ya watu wengi''
"Muongozo wa sasa wa tiba ya shinikizo la damu haupendekezi muda wa kumeza dawa. Nyakati za asubuhi zinapendekezwa sana japo kuna uwezekano huenda dhana ya kuwa wakati huo kiwango cha presha ya damu mwilini kiko chini ikawa inapotosha.
"Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa wagonjwa waliomeza dawa za kukabiliana na presha usiku wakati wa kulala wana uwezo wa kudhibiti hali hiyo na pia hatari kufariki kutokana na magonjwa yanayoathiri mishipa ya kusafirisha damu kwa moyo."
Anasema ni muhimu kufanyia utafiti makundi mengine ili kubaini ikiwa matokeo ya utafiti huu wa sasa unaweza kuwasaidia wagonjwa wote wa shinikizo la damu au ni kwa kikundi maalum cha wagonjwa.
Vanessa Smith, kutoka wakfu wa moyo wa Uingereza, alisema: "Japo utafiti huu unaunga mkono tafiti zilizopita, ipo haja ya kufanyia utafiti makundi mengine ya watu katika jamii ili kubaini ikiwa kumeza dawa za presha wakati wa usiku kuna manufaa zaidi kwa afya ya mgonjwa.
"Ikiwa unatumia dawa za presha, ni muhimu kufuata maagizo ya daktari kuhusu muda maalum wa kumeza dawa hizo. Kuna sababu ya msingi kwanini daktari amekuelekeza kumeza dawa wakati wa usiku au asubuhi ."
Mtundo wa maisha pia unaweza kuleta mabadiliko katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa shinikizo la damu.
- Unywaji wa pombe kupita kiasi
- Kuvuta sigara
- Uzani wa juu wa mwili kupita kiasi
- Kutofanya mazoezi
- Kutumia chumvi nyingi katika chakula













