Rais Erdogan wa Uturuki 'aitupa pipani barua ya Trump kuhusu Syria '

Rais Recep Tayyip Erdogan akiwa ofsini kwake Octoba 9, siku ambayo barua Donald Trump ilitumwa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Barua hiyo ilimshauri rais Erdogan asiwe "mpumbavu"
Muda wa kusoma: Dakika 2

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliitupa barua ya rais wa Marekani Donald Trump katika "pipa la taka", BBC imefahamishwa.

Katika barua hiyo ilioandikwa Octoba tarehe 9 na kutumwa baada ya vikosi vya Marekani kuondolewa Syria, Bw. Trump alimuambia Erdogan: "Usijifanye kuwa na nguvu. Usiwe mpumbavu!"

Vyanzo vya ofisi ya rais wa Uturuki vimeiambia BBC kuwa barua hiyo "ilimkasirisha sana" Rais Erdogan.

Siku ambayo barua hiyo ilipokewa, Uturuki ilianza operesheni yake dhidi ya vikosi vya Kikurdi katika eneo la mpakani.

"Wacha tufikie mpango mzuri! Bilashaka hutaki kuhusika na mauaji ya maelfu ya watu, na mimi pia sitaki kuhusika na uharibifu wa uchumi wa Uturuki - na nitafanya hivyo," Bw. Trump alisema katika barua hiyo.

"Historia itakuhukumu kwa haki ukishughulikia suala hili kwa njia ya kibinadamu. Itakuhukumu daima kama shetani kwa maovu."

Katika majibu yake, vyanzo katika ofisi ya rais wa Uturuki vilisema: "Rais Erdogan alipokea barua, na kupinga vikali yaliomo na kuitupa kwenye pipa la taka."

Barua ya Trump kwa Erdogan

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Trump alimwambia Bw. Erdogan: 'Wacha tufikia mpango mzuri!'
Presentational white space

Rais Trump amelaumiwa vikali kwa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria huku wakosoaji wakisema kuwa hatua hiyo iliipatia Uturuki nafasi ya kuanzisha mashambulizi ya kijeshi nchini humo.

Ukosoaji mkubwa umetoka ndani ya chama chake Bw.Trump.

Katika hatua isiokuwa ya kawaida, wabunge 129 wa chama cha Republican katika bunge la uwakilishi waliungana na wenzao wa chama cha Democratic kupiga kura ya kupinga uamuzi huo siku ya Jumatano.

Azimio hilo la pamoja ambalo pia lilimtaka rais Erdogan kukomesha mara moja oparesheni ya kijeshi dhidi ya vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji wa Kikurdi, lilipitishwa kwa kura 354 - 60.

Rais wa Marekani Donald Trump

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Rais Trump amekosolewa vikali kwa kuondoa majeshi ya Marekani nchini Syria

Spika wa bunge la Marekani, Nancy Pelosi pia alikutana na rais Trump, kujadili suala hilo katika mkutano uliokumbwa na majibizano makali yaliyochangia yeye na kiongozi wa wachache katika bunge la Seneti, Charles Schumer, kuondoka katika chumba cha mkutano huo.

Viongozi wa Republican walisema hatua ya Bi Pelosi ni ukosefu wa "nidhamu", na kumkosoa kwa "kuondoka katika mkutano huo".

Bi. Pelosi na Bw.Trump pia walilaumiana kwa kile "kilichotokea", na baadae Trump akaweka kwenye Twitter picha ya majibizano kati yao.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Presentational white space

Lakini picha hiyo imesifiwa na Wanachama wa Democrats, ambao walisema ni ya "kishujaa" na ilimuonesha Bi. Pelosi akiwa "katika ubora wake". Bi Pelosi pia aliifanya picha hiyo kuwa picha yake kuu katika mtandao wa Twitter.

Mapema siku ya Jumatano Rais Trump, alisema Marekani haitaingilia kati oparesheni ya kijeshi ya Uturuki nchini Syria, kwasababu nchi hiyo "sio mpaka wake", na kuongeza kuwa Wakurdi ambao walikuwa washirika wao wa zamani "sio malaika".

Ramani inayoonyesha hali halisi ya mzozo wa Syria
Maelezo ya picha, Ramani inayoonyesha hali halisi ya mzozo wa Syria