Uholanzi: Familia iliyokuwa ikisubiri 'mwisho wa dunia' kwa miaka tisa yapatikana

Chanzo cha picha, EPA
Familia moja iliyoishi katika chumba cha chini ya ardhi kwa miaka tisa "ikisubiri mwisho wa dunia" imepatikana na polisi nchini Uholanzi, ripoti zinasema.
Mwanamume wa miaka 58, na watoto wake sita walio na umri kati ya miaka 16 hadi 25 - walikuwa wakiishi katika shamba lao katika mkoa wa kaskazini wa Drenthe.
Walipatikana baada ya kijana wake mkubwa kuenda kununua pombe katika baa moja karibu na kijiji cha Ruinerwold, na kumfahamisha mhudumu wa baa hiyo kwamba anataka usaidizi,Kituo cha Televisheni cha RTV kiliripoti.
Waliomuona kijana huyo wanasema alionekana kana kwamba amechanganyikiwa.
Familia yake imekuwa ikiishi kwa kujitenga ikisubiri mwisho wadunia, RTV iliripoti.
"Aliagiza chupa tano za bia na kunywa zote. Baada ya hapo nilisema nae kidogo ndipo alipofichua kuwa ametoroka na kwamba anaomba usaidizi... tukapiga simu polisi," mmiliki wa baa hiyo Chris Westerbeek alikifahamisha kituo cha RTV.
Aliongeza kuwa: "Alikuwa na nywele ndefu, ndevu chafu,nguo zilizochakaa na alionekana kana kwamba amechanganyikiwa. Alisema hajawahi kwenda shule na kwamba hajawahi kunyolewa nywele kwa miaka tisa ."

Chanzo cha picha, EPA
"Alisema ana ndugu na dada zake ambao wanaishi katika shamba hilo. Pia alisema anataka kukomesha jinsi familia yake inavyoishi."
Maafisa walitembelea makaazi hayo ya vijijini ili kufanya upekuzi zaidi. Waligundua ngazi iliokuwa nyuma ya kabati katika sebule ya nyumba hiyo ambayo inaelekeachumba cha chini ya ardhi ambako familia hiyo ilikuwa ikiishi.
Ruinerwold ni kijiji kilicho na wakazi chini ya 3,000. Shamba hilo lipo nje kidogo ya kijiji hicho ana inaweza kufikiwa tu kupitia daraja lililoko juu ya mfereji.
Shamba hilo ambalo kwa upande mmoja limefichwa na miti mingi pia limepandwa mboga nyingi.
Jirani aliviambia vyombo vya habari vya Uholanzi kuwa alimuona mtu huyo peke yake na kwa alifikiria hana watoto.
Watu katika eneo hilo walisambaza taarifa hiyo katika mtandao wa kijamii wa Twitter huku mwanahabari mmoja akiweka picha ya nyumba hiyo na ujumbe kwamba ameambiwa akae mbali na makazi hayo
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe

Polisi imethibitisha mjini Drenthe imethibitisha kuwa mwanamume huyo wa miaka 58 amekamatwa na kuongeza anafanyiwa uchunguzi-baada ya kukataa kushirikiana nao.













