Vita Yemen: Waasi wa Houthi wanadai kuwakamata kwa wingi wanajeshi wa Saudi Arabia

Chanzo cha picha, Reuters
Waasi wa Houthi nchini Yemen wanasema wamewakamata sehemu kubwa ya wanajeshi wa Saudi Arabia baada ya shambulio kubwa karibu na mpaka kati ya mataifa hayo mawili.
Msemaji mmoja wa Houthi ameileza BBC kwamba vitengo vitatu vya jeshi la Saudia vilijisalimisha karibu na mpaka na mji wa Saudia wa Najran.
Amesema maelfu ya wanajeshi walikamatwa na wengine wengi kujeruhiwa. Maafisa nchini Saudia hawajathibitisha taarifa hizi.
Operesheni hiyo ilikuwa kubwa ya aina yake angu kuzuka mzozo, msemaji huyo ameeleza.
Kanali Yahiya Sarea amesema vikosi vya Saudi Arabia vilikabiliwa na hasara kubwa kwa 'kupoteza maisha na mashine pia'.
Wote waliokamatwa wataonyeshwa hadharani katika televisheni ya kundi hilo la waasi Al Masirah TV Jumapili, aliongeza.
Waasi wa Houthi wanasema walishambulia vituo vya mafuta vya Saudia kwa makombora na ndege zisizokuwa na rubani mnamo Soetmba 14 hatua iliyoathiri masoko ya kimataifa.
Lakini Saudia inasema - na kuungwa mkono na Marekani, Uingereza Ufaransa na Ujerumani - ambazo zote zimeituhumu Iran kuhusika na mashambulio hayo, tuhuma ambazo Tehran inakana.
Mzozo ulianzia wapi?
Yemen imekuwa katika vita tangu 2015, wakati rais Abdrabbuh Mansour Hadi na baraza lake la mawaziri lilipolazimishwa na waasi wa Houthi kutoroka mji mkuu Sanaa - ambao wanadhibiti sehemu kubwa za eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.
Saudi Arabia inamuunga mkono rais Hadi, na imeongoza muungano wa mataifa ya kieneo katika mashambulio dhidi ya waasi hao wanaungwa mkono na Iran.
Muungano huo hufyetua makombora karibu kila siku, wakati waasi wa Houthi hurusha makombora dhidi ya Saudia.
Vita hivyo vya kiraia vimesababisha janga baya duniani la kibinaadamu, huku 80% ya idadi ya watu - ambayo ni zaidi ya watu milioni 24 - wakihitaji usaidizi wa kibinaadamu au ulinzi, wakiwemo watu milioni 10 wanaotegemea chakula cha misaada ili kuendelea kuishi.
Zaidi ya watu 70,000 wanaaminika kufariki tangu 2016 kutokana na mzozo huo, Umoja wa mataifa unakadiria.

















