Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Syria : Mashambulizi ya angani yavilenga vikosi vinavyoungwa mkono na Iran
Mashambulizi ya angani yamepiga maeneo ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran karibu na mpaka wa Syria na Iraq kulingana na wanaharakati.
Shirika la haki za kibinadamu la Syrian Observatory for Human Rights, lililo na makao yake nchini Uingereza limesema kwamba takriban wapiganaji 18 wa Iran na wale wanaoungwa mkono na Iran waliuawa.
Haijulikani ni nani aliyetekeleza mashambulio hayo usiku kucha ndani na nje ya mji wa Albu kamal.
Lakini Israel imetekeleza mamia ya mashambulizi dhidi ya kambi za Iran nchini Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Lengo la Israel ni kuangamiza kile inachokitaja kuwa uwezo wa kijeshi wa Iran nchini Syria mbali na usafirishaji wa silaha za Iran kwa makundi ya kijeshi kama vile Hezbollah nchini Lebanon.
Shirika hilo la haki za kibinadamu lilinukuu vyanzo vyake vikisema kwamba ndege hizo zisizojulikana zililipua kambi na hifadhi za zana na magari yanayomilikiwa na wapiganaji wa Iran katika eneo la al- Hizam al-Akhdar pamoja na maeneo mengine karibu na Albu Kamal.
Omar Abu Layla , mwanaharakati mwenye makao yake Ulaya kutoka kundi la DeirEzzor 24 , alisema kwamba milipuko mikubwa ilisikika katika mji huo na kwamba kulikuwa na ghasia na hofu miongoni mwa wapiganaji hao.
Kundi jingine kwa jina Sound and Pictures , lilinukuu maafisa wa afya waliosema kwamba takriban watu 21 waliuawa na kwamba wapiganaji walichukua mifuko yote ya damu katika hospitali ya Albu kamal ili kuwapona wapiganaji wao waliojeruhiwa'
Duru kutoka jeshi linaloungwa mkono na Iran ziliambia BBC kwamba ndege moja isio na rubani ililenga makao yake makuu katika mpaka wa Syria na Iraq takriban kilomita 6 kusini mwa Albu kamal.
Jeshi hilo lilituma magari kutoka mji uliopo karibu wa al-Qaim hadi katika eneo hilo ambalo lilikuwa na idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa duru hiyo iliongezea.
Je Israel inasemaje?
Jeshi la Israel halikutoa tamko lolote kuhusu kisa hicho , lakini liliripoti kwamba idadi kubwa ya mabomu ya roketi yalirushwa kuelekea Israel saa chache baadaye kutoka maeneo ya viungani vya mji mkuu wa Damascus.
Ilisema kuwa roketi hizo zilifeli kupiga maeneo ya Israel na kuwalaumu wapiganaji wanotekeleza operesheni zao chini ya jeshi la Iran Revolutionary Guard lakini ikasema kwamba inalaumu serikali ya Syria.
Wakati huohuo, Hezbollah imesema kwamba wapiganaji wake waliangusha ndege isiokuwa na rubani ya Israel katika anga ya kusini mwa Lebanon mapema siku ya Jumatatu na kuikamata.
Jeshi la Israel lilisema ndege yake moja ilianguka kusini mwa Lebanon wakati wa operesheni zake za kawaida, lakini haikutoa sababu , lakini ilisema kwamba hakuna hofu kwamba ujumbe iliokuwa ikikusanya utachukuliwa
Kwa nini Israel na Iran ni maadui
Israel imeshambulia kwa mabomu na makombora vikosi vya Iran nchini Syria na kuzua wasiwasi kwamba mataifa hayo mawili hasimu huenda yakapigana.
Lakini je, uhasama wao ulianza wapi na nini kinaweza kutokea?
Tangu kufanyika kwa Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, ambapo viongozi wa kidini wenye msimamo mkali walichukua mamlaka na kumaliza utawala wa Shah, Iran imekuwa ikiitisha kuangamizwa kwa Israel.
Iran husema taifa la Israel halina haki zozote za kuwepo, kwa sababu liliundwa kwenye ardhi ambayo ilitekwa kutoka kwa Waislamu.
Israel hutazama Iran kama tishio kuu dhidi ya kuwepo kwake. Taifa hilo la Kiyahudi limekuwa likisisitiza kwamba Iran haifai kuruhusiwa kuwa na silaha zozote za kinyuklia.
Viongozi wao wana wasiwasi sana kuhusu kuenea kwa ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati.
Syria inaingiaje katika mzozo huu?
Israel imekuwa ikifuatilia matukio katika taifa jirani la Syria kwa wasiwasi tangu vita vilipozuka mwaka 2011.
Israel imekuwa haishiriki katika vita hivyo kati ya serikali ya Bashar al-Assad na waasi.
Lakini Iran imeshiriki sana katika vita hivyo ambapo imetuma maelfu ya wapiganaji na washauri wa kijeshi kusaidia wanajeshi wa Bw Assad.
Israel ina wasiwasi pia kwamba Israel inajaribu kuwatuma wapiganaji na silaha kisiri nchini Lebanon - jirani mwingine wa Israel - ambayo pia huitishia Israel.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mara kwa mara amesisitiza kwamba taifa lake halitairuhusu Iran ijenge kambi Syria ambazo zinaweza kutumiwa dhidi ya Israel.
Kwa hivyo, kadiri Iran ilivyoendelea kujiimarisha nchini Syria ndivyo Israel ilivyodhidisha mashambulio dhidi ya kambi na wanajeshi wa Iran huko.
Iran na Israel zishawahi kupigana?
Hapa. Iran kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono makundi yanayoishambulia Israel - kwa mfano Hezbollah wa Lebanon na kundi la Hamas la Palestina.
Lakini mataifa hayo mawili hayajawahi kupigana moja kwa moja na inakadiriwa kwamba vita kama hivyo vinaweza kusababisha uharibifu mkubwa.
Iran ina shehena kubwa ya makombora ya masafa marefu na ina washirika walio na silaha kali pia wanaopakana na Israel.
Israel nayo ina jeshi lenye nguvu sana na inadaiwa kuwa na silaha za nyuklia.
Aidha, Israel huungwa mkono kikamilifu na Marekani.