Wanamuziki: 'Salamu za Amani kutoka Afrika'

Muda wa kusoma: Dakika 3

Vurugu zinazoendelea Afrika Kusini dhidi ya raia wa kigeni ambao ni wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika zimewahamasisha wanamuziki mbalimbali barani Afrika kutunga tungo za kukemea vitendo vya chuki dhidi ya wageni.

Nigeria, Zambia, Msumbiji, Tanzania, Kenya ni miongoni mwa wageni nchini humo ambao wako hatarini na shambulio hilo ambalo limewafanya wengine kurudi katika nchi zao.

Mauaji, hofu na shughuli za wageni kusitishwa kutokana na uharibu mbaya uliofanywa na wenyeji ni miongoni mwa mambo yanayokemewa na wasanii mbalimbali barani Afrika.

Kufuatia hali hiyo, vita ya maneno imekuwa ikichukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii kutoka bara lote la Afrika kulaani vitendo hivyo vya kikatili.

Nchini Tanzania, wimbo wa Nash unaokemea chuki hizo umekuwa ukishirikishwa na wengi katika mtandao wa whatsapp na swali ni je, ujumbe huu unafika?

"Beti nakutuma mpaka Afrika ya Kusini waambie wazulu waweke silaha chini , kisha wasikilize neno lako kwa makini

Vurugu na mauaji ya waafrika wenzao, beti waeleze kwamba sisi ndugu zao, ajira haipatikani kwa kumuua mtanzania,msomali, mmalawi ama ndugu zangu kutoka Nigeria

Lini mtabadilika muwe na roho za kiutu...ninashangaa iweje mfike huku, mnauwa ndugu zenu utadhani mnauwa kuku...

TZ tunasema mgeni aje, mwenyeji apone, kwenu ni tofauti ni mgeni njoo nishike panga nikupige, nikukimbize, nikukamate nikumalize....hayo mambo ya kufanywa na watu wenye wazimu...." wimbo wa Nash unaopinga chuki dhidi ya wageni Afrika kusini.

BBC imezungumza na Mutalemwa Jason ambaye ni mwanamuziki kutoka nchini Tanzania ajulikanaye kama Maalim Nash au Nash Mc na kutaka kujua kwa nini aliamua kuimba wimbo huo.

Nash MC a nasema aliona kuwa kuna haja kutumia sanaa kufikisha ujumbe kukemea kile kinachoendelea Afrika Kusini.

"Muziki wa Hip pop unatuelekeza kutengeneza watu kifikra na kuhakikisha misingi ya kibinadamu na utu pia unafuatwa" Nash Mc a eleza.

Nyimbo hiyo ya Nash ameitaja kuwa ni ya ukombozi wa mwafrika na hivyo aliamua kutumia kipaji chake kufikisha ujumbe.

Kwa upande wake kuimba kiswahili na kutaka ujumbe uwafikie waafrika kusini amesema kuwa aliwahi kufika huko mwaka 2015, na kutokana na watanzania kuwa wengi huko kiswahili sasa wanajua.

Muziki huu wa hip pop unatuma ujumbe tena kutoka kwa kijana wa miaka 15, anayelisimulia maumivu aliyoyapata kwa kumpoteza rafiki yake kutoka Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo kwa sababu rafiki yake ilimlazimu ahame kutokana na shambulizi la chuki kwa wageni, nchini Afrika kusini .

Mtoto huyo alitoa hisia zake wakati wa mashindano ya vipaji nchini Afrika kusini, 'SA's Got Talent' na ujumbe wake kusambaa kwa wingi mitndaoni.

Mwanamuziki mwingine maarufu nchini Tanzania, RayVanny ameimba wimbo wa Afrika kwa lugha kwa kiingereza akisisita kuwa wasimuite mgeni, Afrika ni nyumbani na mama yetu ni mmoja.

Mungu ibariki Afrika, tuache kupigana na tukumbuke maneno ya Mandela aliyotufundisha kuhusu upendo.

Wanamuziki wengine wengi kutoka Afrika wameimba nyimbo kwa lugha ya Igbo, Kizulu,Tswana, Suthu, Shona na kiingereza wakisisitiza umoja wa Afrika.