Mkufunzi wa zamani wa Man United Louis Van Gaal na mwanamuziki wa Marekani Neyo wahudhuria tamasha la kuwapatia majina sokwe Rwanda

Rwanda imewapa majina watoto wa sokwe 25 ikiwa ni desturi inayofanyika kila mwaka kwa ajili ya kuvutia ulimwengu kutembelea sokwe hao .
Wakati huo huo serikali ya nchi hiyo imetangaza kwamba idadi ya sokwe hao iliongezeka kwa kiwango cha asilimia 26 tangu mpango kabambe wa kuwahifadhi ulipoanza mwaka 2003.Mwandishi wa BBC nchini Rwanda Yves Bucyana ametuandalia taarifa ifwatayo:
Huyo ni Luis Van Gaal, Mkufunzi wa zamani wa Uholanzi na timu kadhaa za ulaya alitoa jina lake kwa mtoto wa sokwe kama alivyolitaja mwenyewe kuwa ''Indongozi'' ……maanake kwa Kinyarwanda ni kiongozi shupavu. ….maelezo yake Van Gaal amesema kwamba alichagua jina hilo kutokana na historia mbaya iliyolisibu taifa la Rwanda mwaka 94 na hatua ya sasa ya maendeleo makubwa.

Rais Paul Kagame ametangaza kwamba serikali imetoa kipaumbele kwa swala la kuimarisha juhudi za kuhifadhi sokwe wa volcano ambao huingizia taifa fedha nyingi za kigeni.
Rais amesema kwamba serikali iliamua kuongeza pesa zinazogawiwa kila mwaka wananchi majirani wa mbuga ya Volcano, kama kuwavutia kuchangia juhudi za kuhifadhi sokwe:
''Tuliamua kuwagawia wananchi kiasi cha asimilia 10 ya pesa zinazoingia kila mwaka ili kuwasaidia kujiendeleza.Wananchi majiraji wa mbuga ya sokwe ndio washirika wetu wakubwa.hii itatuwezesha sote kusaidiana kuhifadhi sokwe hawa na sote kuendeleza taifa letu''

Watu wengine mashuhuri walliohudhuria sherehe hizo na kutoa majina yao kwa sokwe ni pamoja na waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Amina Mohamed, mwanamitindo wa Uingereza Naomi Campbell na mwanamuziki Ne-Yo kutoka Marekani ,miongoni mwa wengine.
Kulingana na bodi ya maendeleo ya Rwanda, sokwe waliotangazwa kuwa adimu duniani wanazidi kuongezeka tangu mikakati ya kuwahifadhi ilipoanza mwaka 2003.
Idadi hiyo ya sokwe iliongezeka kutoka sokwe 318 na kufikia 618 hivi sasa.
Kiongozi wa bodi hiyo Bi Clare Akamanzi amesema utalii wa sokwe uliifanya Rwanda kutembelewa sana:
''Wanaotalii Rwanda kupitia angani au barabarani wanazidi kuongezeka .nakumbuka kwamba mwanzo walikuwa watalii kama laki 5 tu lakini mwaka jana tulipokea watu wapatao milioni 1,7 kutokana na kuwa Rwanda ni nchi salama na yenye miundo mbinu, taifa letu sasa linaorodheshwa la pili barani Afrika katika kupokea mikutano ya kimataifa nyuma ya Afrika kusini.''
Kulingana na bodi hiyo sekta ya utalii Rwanda iliingiza dolla milioni 438 mwaka jana kutokana na shughuli za utalii, lengo likiwa ni kutinga dolla milioni 800 kwa mwaka.













