Albert Nabonibo: Msanii wa muziki wa kiinjili aliyekiri kushiriki mapenzi ya jinsia moja Rwanda

Albert Nabonibo anasema wakati umewadia kwa Warwanda kukubali ni jambo la kawaidi kushiriki mapenzi ya jinsia moja

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha, Albert Nabonibo anasema wakati umewadia kwa Wanyarwanda kukubali kuwa ni jambo la kawaidi kushiriki mapenzi ya jinsia moja

Msanii wa muziki wa kiinjili nchini Rwanda amekuwa raia wa kwanza wa nchi hiyo kukiri hadharani kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja.

Albert Nabonibo mwenye umri wa miaka 35 ameiambia BBC kuwa anatarajia kukosolewa vikali kufuatia hatua huyo lakini yuko tayari kukabiliana na changamoto hizo.

Anasema kuwa utamaduni wa Wanyarwanda unapinga vikali mapenzi ya jinsia moja- na kwamba uamuzi wa kuweka wazi suala hilo umewagutusha mashabiki wake.

Sheria ya Rwandan haijapiga marufuku uhusiano wa wapenzi wa jinsia moja lakini ndo ya ya watu wa jinsia moja hairuhusiwi na makanisa mengi nchini humo yanahubiri kuwa ni dhambi kushiriki mapenzi ya ya jinsia moja.

Hii inamaanisha kuwa Nabonibo ameficha mahusiano yake kwa muda mrefu -lakini hatimae ameamua kuvunja kimya chake.

"Ukweli ni kwamba kuna watu wengi kama mimi makanisani ni vile tu wanafanya siri mahusiano yao kwa sababu ya kuhofia kuhukumiwa na waumini wengine na jamii nzima kwa ujumla. Pia wanahofia usalama wao ," Nabonibo aliiambia BBC.

Lakini Nabonibo ambaye amezaliwa Kacyiru viungani mwa mji mkuu wa Kigali, anasema wakati umewadia kwa Wanyarwanda kukubali kuwa ni jambo la kawaida kushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Maelezo ya sauti, Msanii awagutusha mashabiki kwa kukiri hadharani anashiriki mapenzi ya jinsia moja

"Nawahurumia wenzangu wanaoishi kwa uwoga. Ni vyema nao wapaze sauti ili nao wasikike, kwa sababu wana haki ya kujiamulia wanachotaka," alisema.

Tayari ameanza kupokea ujumbe wa matusi tangu alipotangaza hadharani kuhusu mahusiano yake siku ya jumatatu kupitia mtandao wa Youtube wa shirika moja la kidini.

"Baadhi ya watu wananitukana na wengine wananiita mjinga. Lakini kuna wale wanaonielewa - kwa mfano ndugu yangu ananitia moyo na kunishauri nijikubali nilivyo."

Licha ya changamoto anazopitia, Nabonibo anasema kuwa ataendelea kumtukuza Mungu kwa "Kumuimbia".

"Nitaishi na wale wanaonikubali na wale wanaonipinga pia - Najua kitakuwa kibarua kigumu."